Book of Common Prayer
Matatizo Mengi kwa waamini
12 Katika wakati huu huu, Mfalme Herode akaanza kuwatesa baadhi ya waamini waliokuwa sehemu ya kanisa. 2 Aliamuru Yakobo aliyekuwa kaka yake Yohana, auawe kwa upanga. 3 Herode alipoona kuwa Wayahudi wamelifurahia jambo hili, aliamua kumkamata Petro pia. Hii lilitokea katika kipindi cha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. 4 Alimkamata Petro na kumfunga gerezani, ambako alilindwa na kundi la askari kumi na sita.[a] Herode alipanga kumleta Petro mbele ya watu ili ahukumiwe, lakini alisubiri mpaka baada ya sikukuu ya Pasaka. 5 Hivyo Petro aliwekwa gerezani lakini kanisa lilikuwa likiomba kwa Mungu bila kuacha kwa ajili yake.
Petro Atolewa Nje ya Gereza
6 Wakati wa usiku kabla ya siku ambayo Herode alipanga kumhukumu mbele ya watu, Petro, akiwa amefungwa minyororo miwili, alikuwa amelala katikati ya askari wawili. Na askari waliokuwa nje ya mlango walikuwa wanalinda gereza. 7 Ghafla malaika wa Bwana alikuwa amesimama pale, na chumba kilijaa mwanga. Malaika akamwamsha Petro kwa kumpiga upande, akasema, “Amka haraka!” Minyororo ikaanguka kutoka mikono mwa Petro. 8 Malaika akasema, “Vaa nguo na viatu vyako.” Petro alifanya kama alivyoambiwa. Kisha malaika akasema, “Vaa koti lako na unifuate.”
9 Hivyo malaika akatoka nje na Petro alimfuata. Hakujua kama kweli malaika alikuwa anafanya hili. Alidhani alikuwa anaona maono. 10 Petro na malaika wakavuka lindo la kwanza na lindo la pili. Kisha walifika kwenye lango la chuma lililowatenganisha na mji. Lango likafunguka. Baada ya kuvuka lango na kutembea umbali wa kama mtaa mmoja, malaika akatoweka ghafla.
11 Ndipo Petro akatambua kuwa haikuwa ndoto. Akawaza moyoni akisema, “Sasa ninajua kwamba Bwana hakika alimtuma malaika wake kwangu. Ameniokoa kutoka kwa Herode na kutoka kwenye mabaya yote ambayo Wayahudi walidhani yatanipata.”
12 Petro alipotambua hili, alikwenda nyumbani kwa Mariamu, mama yake Yohana, aliyeitwa Marko. Watu wengi walikuwa wamekusanyika pale wakiomba. 13 Petro alibisha kwenye mlango wa nje. Mtumishi wa kike aliyeitwa Rhoda alikuja ili afungue mlango. 14 Alipoitambua sauti ya Petro, alifurahi sana hata akasahau kufungua mlango. Akakimbilia ndani na kuliambia kundi, “Petro yuko mlangoni!” 15 Waamini wakamwambia, “Wewe una kichaa!” Lakini alipoendelea kusema kwamba ni kweli Petro yuko mlangoni. Waamini walisema, “Lazima atakuwa malaika wa Petro.”
16 Lakini Petro aliendelea kubisha mlangoni. Waamini walipoufungua mlango na kumwona, wakashangaa. 17 Petro akawafanyia ishara kwa mkono wake kuwaambia wanyamaze. Akawaeleza namna Bwana alivyomtoa nje ya gereza. Akasema, “Mwambieni Yakobo na ndugu wengine kilichotokea.” Kisha akawaacha na kwenda sehemu nyingine.
33 Wakamjibu, “Sisi ni wazaliwa wa Ibrahimu. Na hatujawahi kamwe kuwa watumwa. Sasa kwa nini unasema kuwa tutapata uhuru?”
34 Yesu akasema, “Ukweli ni huu, kila anayefanya dhambi ni mtumwa wa dhambi. 35 Mtumwa hakai na jamaa yake siku zote. Lakini mwana hukaa na jamaa yake siku zote. 36 Hivyo kama Mwana atawapa uhuru, mtakuwa mmepata uhuru wa kweli. 37 Najua kuwa ninyi ni wazaliwa wa Ibrahimu. Lakini mmekusudia kuniua, kwa sababu hamtaki kuyakubali mafundisho yangu. 38 Nawaambia yale ambayo Baba yangu amenionyesha. Lakini ninyi mnayafanya yale mliyoambiwa na baba yenu.”
39 Wakasema, “Baba yetu ni Ibrahimu.”
Yesu akasema, “Kama mngekuwa wazaliwa wa Ibrahimu kweli, mngefanya yale aliyofanya Ibrahimu. 40 Mimi ni mtu niliyewaambia ukweli niliousikia kutoka kwa Mungu. Lakini Ibrahimu hakufanya kama hayo mnayotaka kufanya. 41 Mnafanya yale aliyofanya baba yenu.”
Lakini wakasema, “Sisi sio kama watoto ambao hawajawahi kumjua baba yao ni nani. Mungu ni Baba yetu. Ni baba pekee tuliye naye.”
42 Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu kweli, mngenipenda. Nilitoka kwa Mungu, na sasa niko hapa. Sikujileta kwa mamlaka yangu mwenyewe. Mungu alinituma. 43 Hamuyaelewi mambo ninayosema, kwa sababu hamuwezi kuyakubali mafundisho yangu. 44 Baba yenu ni ibilisi. Ninyi ni wa kwake. Nanyi mnataka kufanya anayotaka. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo. Siku zote alikuwa kinyume na ukweli. Hakuna ukweli ndani yake. Yuko kama uongo anaousema. Ndiyo, ibilisi ni mwongo. Na ni baba wa uongo.
45 Nawaambieni ukweli, na ndiyo maana hamniamini. 46 Kuna mtu miongoni mwenu anayeweza kunishuhudia kuwa mimi nina hatia ya dhambi? Kama nawaeleza ukweli, kwa nini hamniamini? 47 Yeyote aliye wa Mungu huyapokea anayosema. Lakini ninyi hamuyapokei anayosema Mungu, kwa sababu ninyi si wa Mungu.”
© 2017 Bible League International