Book of Common Prayer
Paulo Akiwa Efeso
19 Apolo alipokuwa katika mji wa Korintho, Paulo alikuwa anatembelea baadhi ya sehemu akiwa njiani kwenda Efeso. Alipofika Efeso waliwakuta baadhi ya wafuasi wa Bwana. 2 Akawauliza, “Mlimpokea Roho Mtakatifu mlipoamini?”
Wafuasi hao wakamwambia, “Hatujawahi hata kusikia kuhusu Roho Mtakatifu!”
3 Paulo akawauliza, “Kwa hiyo ni mlibatizwa kwa ubatizo gani?”
Wakasema, “Kwa ubatizo aliofundisha Yohana.”
4 Paulo akasema, “Yohana aliwaambia watu wabatizwe kuonesha kuwa walidhamiria kubadili maisha yao. Aliwaambia watu kuamini katika yule atakaye kuja baada yake, naye huyo ni Yesu.”
5 Wafuasi hawa waliposikia hili, wakabatizwa katika jina la Bwana Yesu. 6 Kisha Paulo akawawekea mikono, na Roho Mtakatifu akaja juu yao. Wakaanza kuzungumza na kutabiri katika lugha tofauti. 7 Walikuwepo wanaume kama kumi na mbili katika kundi hili.
8 Paulo akaingia katika sinagogi na akazungumza kwa ujasiri. Aliendelea kufanya hivi kwa miezi mitatu. Alizungumza na Wayahudi, akijaribu kuwashawishi kukubali alichokuwa anawaambia kuhusu ufalme wa Mungu. 9 Lakini baadhi yao wakawa wakaidi, wakakataa kuamini. Waliikashifu Njia[a] ya Bwana mbele ya kila mtu. Hivyo Paulo aliwaacha Wayahudi hawa na kuwachukua wafuasi wa Bwana pamoja naye. Alikwenda mahali ambapo mtu aitwaye Tirano alikuwa na shule. Hapo Paulo alizungumza na watu kila siku. 10 Alifanya hivi kwa miaka miwili na kila mtu aliyeishi Asia, Wayahudi na Wayunani alilisikia neno la Bwana.
34 Kisha Yesu akaliita kundi lote pamoja na wanafunzi wake kwake, akawaambia, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, lazima ajikane yeye mwenyewe, na ni lazima auchukue msalaba wake mwenyewe kisha anifuate. 35 Kwa kuwa kila anayetaka kuusalimisha uhai wake, ataupoteza, na yeyote atakayeupoteza uhai wake kwa ajili yangu na kwa ajili ya injili atausalimisha. 36 Itampa mtu manufaa gani akiupata ulimwengu wote kisha akaupoteza uhai wake? 37 Mtu anaweza kuubadilisha uhai wake na kitu gani? 38 Hiki ni kizazi chenye dhambi na kisichokuwa na uaminifu. Hivyo, mtu yeyote atakayenionea haya mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Adamu naye atamwonea haya mtu huyo siku ile atakaporudi katika utukufu wa Baba yake akiwa na malaika wake watakatifu.”
9 Naye Yesu aliwaambia, “Ninawaambia Ukweli: baadhi yenu mnaosimama hapa mtauona ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu kabla ya kufa kwenu.”
© 2017 Bible League International