Book of Common Prayer
Upendo Hutoka kwa Mungu
7 Wapenzi rafiki, tunatakiwa tupendane sisi kwa sisi, kwa sababu upendo watoka kwa Mungu. Yeyote apendae amefanyika mwana wa Mungu. Na kila apendae anamfahamu Mungu. 8 Kila asiyependa hamfahamu Mungu, kwa sababu Mungu ni Pendo. 9 Hivi ndivyo Mungu alivyo tuonyesha pendo lake sisi: Alimtuma mwanawe wa pekee ulimwenguni kutupatia sisi uzima katika yeye. 10 Upendo wa kweli ni upendo wa Mungu kwa ajili yetu, si upendo wetu kwa Mungu. Alimtuma mwanawe kama njia ya kuziondoa dhambi zetu.
11 Hivyo ndivyo Mungu atupendavyo, rafiki wapenzi! Kwa hiyo tupendane sisi kwa sisi. 12 Hakuna aliyemwona Mungu. Ila tukipendana sisi kwa sisi, Mungu anaishi ndani yetu. Kama tukipendana sisi kwa sisi, Upendo wa Mungu unafikia shabaha yake na unafanywa kamili ndani yetu.
13 Twatambua kuwa tunaishi katika Mungu na mungu ndani yetu. Twalitambua hilo kwa sababu ametupa Roho wake. 14 Tumeona kuwa Baba alimtuma mwanaye aje kuwa Mwokozi wa ulimwengu, na hili ndilo tunalowaambia watu sasa. 15 Yeyote anayesema, “Naamini kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu,” huyo ni mtu anayeishi ndani ya Mungu, na Mungu anaishi ndani ya mtu huyo. 16 Hivyo twalifahamu pendo alilonalo Mungu kwetu, na tunalitumainia pendo hilo.
Mungu ni pendo. Kila anae ishi katika pendo anaishi ndani ya Mungu, na Mungu ndani yao. 17 Kama pendo la Mungu limekamilishwa ndani yetu, tunaweza kuwa bila hofu siku ambayo Mungu atahukumu ulimwengu. Hatutakuwa na hofu, kwa sababu katika ulimwengu huu tunaishi kama Yesu.[a] 18 Palipo na upendo wa Mungu, hakuna hofu, kwa sababu upendo wa Mungu ulio kamili unaondoa hofu. Ni hukumu yake ndiyo inayomfanya mtu kuwa na hofu. Hivyo pendo lake halikamilishwi kwa mtu ambaye ndani yake kuna hofu.
19 Tunapenda kwa sababu Mungu alitupenda sisi kwanza. 20 Kama tukisema kuwa tunampenda Mungu na tunamchukia mmojawapo wa kaka na dada zetu katika familia ya Mungu, basi sisi tu waongo. Kama hatuwezi kumpenda mtu tunayemwona, tutawezaje kumpenda Mungu, ambaye hata hatujamwona. 21 Mungu ametupa amri hii: Kama tunampenda Mungu, Ni lazima pia tupendane sisi kwa sisi kama kina kaka na kina dada.
30 Yesu hakuwa amefika kijijini. Alikuwa bado yupo pale pale Martha alipomkuta. 31 Wayahudi waliokuwepo nyumbani hapo wakimfariji Mariamu walimwona akiinuka na kuondoka ghafla. Walifikiri alikuwa anaenda kaburini kuomboleza. Hivyo wakamfuata. 32 Mariamu alienda pale Yesu alipokuwa. Naye baada ya kumwona, aliinama miguuni pake Yesu na kusema, “Bwana, kama ungekuwa hapa, kaka yangu asingekufa.”
33 Ndipo Yesu alipomwona Mariamu na watu waliokuwa pamoja naye wakilia, akahuzunika na kusikitika sana. 34 Akawauliza, “Mmemweka wapi?”
Wakasema, “Bwana, njoo uone.”
35 Yesu akalia na kutoa machozi.
36 Na Wayahudi wakasema, “Angalia! Alikuwa anampenda sana Lazaro!”
37 Lakini wengine wao wakasema, “Yesu aliyeyaponya macho ya yule mtu asiyeona kwa nini hakumsaidia Lazaro na kumzuia asife?”
Yesu Amfufua Lazaro Kutoka Mautini
38 Akiwa bado ana uchungu na kusikitika sana, Yesu akaenda kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa ni pango lenye jiwe kubwa lililofunika pa kuingilia. 39 Yesu akasema, “Lisogezeni pembeni hilo jiwe.”
Martha akasema, “Lakini, Bwana, ni siku nne[a] sasa tangu Lazaro alipofariki. Kutakuwa na harufu mbaya.” Martha alikuwa ni dada wa marehemu.
40 Kisha Yesu akamwambia Martha, “Unakumbuka jinsi nilivyokuambia? Je, sikukuambia kwamba kama ukiamini, ungeuona utukufu wa Mungu?”
41 Kwa hiyo wakalisogeza lile jiwe kutoka kwenye sehemu ya kuingilia. Kisha Yesu akatazama juu na kusema, “Baba, Nakushukuru kwa kuwa ulinisikia. 42 Najua kuwa siku zote unanisikia. Lakini nimeyasema mambo haya kwa ajili ya watu walioko hapa. Nataka kwamba waweze kuamini kuwa ni wewe uliyenituma.” 43 Baada ya Yesu kusema hivi akaita kwa sauti kubwa, “Lazaro, toka nje!” 44 Yule mtu aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono na miguu yake ilikuwa imefungwa sanda. Uso wake ulikuwa umefunikwa kwa kitambaa.
Yesu akawaambia watu, “Mfungueni hizo sanda na kumwacha aende.”
© 2017 Bible League International