Book of Common Prayer
6 Kisha malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kweli na ya kuaminiwa. Bwana, Mungu awavuviaye manabii, amemtuma malaika wake kuwaonesha watumishi wake mambo ambayo lazima yatokee hivi karibuni: 7 ‘Sikiliza, Naja upesi! Heri anayetii maneno ya unabii yaliyo katika kitabu hiki.’”
8 Mimi ni Yohana. Mimi ndiye niliyesikia na kuyaona mambo haya. Baada ya kuyasikia na kuyaona, niliinama chini kusujudu miguuni pa malaika aliyeyaonesha kwangu. 9 Lakini malaika aliniambia, “Usinisujudie mimi! Mimi ni mtumishi kama wewe na ndugu zako manabii, ni mtumishi kama wale wote wanaoyatii maneno yaliyo katika kitabu hiki. Msujudie Mungu!”
10 Kisha malaika akaniambia, “Usiyafanye siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, wakati umekaribia kwa mambo haya kutokea. 11 Kila atendaye mabaya aendelee kutenda mabaya. Yeyote aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Atendaye mema aendelee kutenda mema. Aliye mtakatifu aendelee kuwa mtakatifu.”
18 Ninamwonya kila mtu anayesikia maneno ya unabii wa kitabu hiki: Ikiwa mtu yeyote ataongeza chochote kwa haya, Mungu atampa mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. 19 Na ikiwa mtu yeyote akitoa sehemu yoyote ya maneno ya kitabu hiki cha unabii, Mungu ataondoa sehemu ya urithi wa mtu huyo katika mti wa uzima na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.
20 Yesu ndiye anayesema kwamba haya yote ni kweli. Sasa anasema, “Ndiyo, naja upesi.”
Amina! Njoo, Bwana Yesu!
Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji
57 Wakati ulipotimia kwa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto wa kiume. 58 Majirani na jamaa zake waliposikia jinsi Bwana alivyokuwa mwema kwake, walifurahi pamoja naye.
59 Mtoto alipofikisha umri wa siku nane, walikuja kumtahiri.[a] Walipotaka kumwita mtoto Zakaria kutokana na jina la baba yake. 60 Mama yake akasema, “Hapana, mtoto ataitwa Yohana.”
61 Lakini wao wakamwambia, “Hakuna jamaa yako hata mmoja mwenye jina hilo.” 62 Ndipo wakamfanyia ishara baba yake wakimwuliza jina alilotaka kumpa mtoto.
63 Zakaria akataka ubao wa kuandikia,[b] Kisha akaandika, “Jina lake ni Yohana.” Wote wakashangaa. 64 Mara hiyo hiyo mdomo wake ulifunguliwa na ulimi wake ukaachia, akaanza kuzungumza na kumsifu Mungu. 65 Majirani zao wakajawa hofu na watu katika sehemu zote za vilima katika jimbo la Yuda wakawa wanazungumza kuhusu jambo hili. 66 Watu wote waliosikia kuhusu mambo haya walijiuliza, wakisema, “Mtoto huyu atakuwa wa namna gani?” Kwa kuwa nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.
© 2017 Bible League International