Book of Common Prayer
22 Sikuona hekalu ndani ya mji. Bwana Mungu Mwenye Nguvu na Mwanakondoo ndiyo waliokuwa hekalu la mji. 23 Mji haukuhitaji jua wala mwezi kuung'arizia. Utukufu wa Mungu uliupa mji mwanga. Mwanakondoo ndiye alikuwa taa ya mji.
24 Mataifa watatembea katika mwanga unaotoka katika mji ule.[a] Watawala wa dunia wataleta utukufu wao katika mji. 25 Milango ya mji haitafungwa hata siku moja, kwa sababu hakutakuwa usiku huko. 26 Ukuu na heshima ya mataifa vitaletwa katika mji. 27 Kilicho najisi hakitaingia katika mji. Atendaye mambo ya kuchukiza na mwongo hawataingia katika mji huo. Walioandikwa kwenye kitabu cha uzima cha Mwanakondoo tu, ndiyo watakaoingia katika mji huo.
22 Malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima, ulikuwa anga'avu kama kioo. Mto hutiririka kutoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo. 2 Hutiririka kupitia katika mtaa mkuu wa mji. Mti wa uzima[b] uko kila upande wa mto, na huzaa tunda kila mwezi, mara kumi na mbili kwa mwaka. Majani ya mti ni kwa ajili ya kutibu mataifa.
3 Katika mji ule hakuna mtu au kitu kitakachokuwa chini ya laana ya Mungu tena. Kiti cha ufalme cha Mungu na Mwanakondoo vitakuwa ndani ya mji. Watumishi wa Mungu watamwabudu yeye. 4 Watauona uso wake. Jina la Mungu litaandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao. 5 Hakutakuwa usiku tena. Watu hawatahitaji mwanga wa taa au mwanga wa jua. Bwana Mungu atawapa mwanga. Watatawala kama wafalme milele na milele.
Mariamu Amtembelea Elizabeti
39 Mariamu akajiandaa na kwenda haraka katika mji mmoja ulio vilimani katika jimbo la Yuda. 40 Alikwenda nyumbani kwa Zakaria, alipofika akamsalimu Elizabeti. 41 Elizabeti aliposikia salamu ya Mariamu, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akirukaruka, na Elizabeti akajazwa Roho Mtakatifu.
42 Kisha akapaza sauti na kumwambia Mariamu, “Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na mtoto utakayemzaa amebarikiwa. 43 Lakini jambo hili kuu limetokeaje kwangu, hata mama wa Bwana wangu aje kwangu? 44 Kwa maana sauti ya salamu yako ilipofika masikioni mwangu, mtoto aliye ndani yangu amerukaruka kwa furaha. 45 Umebarikiwa wewe uliyeamini kuwa mambo aliyokuambia Bwana yatatokea.”
Mariamu Amsifu Mungu
46 Mariamu akasema,
“Moyo wangu unamwadhimisha Bwana,
47 kwa maana, Yeye, Mungu na Mwokozi
wangu amenipa furaha kuu!
48 Kwa maana ameonesha kunijali,
mimi mtumishi wake, nisiye kitu.
Na kuanzia sasa watu wote
wataniita mbarikiwa.
48 Kwa maana ameonesha kunijali,
mimi mtumishi wake, nisiye kitu.
Na kuanzia sasa watu wote
wataniita mbarikiwa.
49 Kwa kuwa Mwenye Nguvu amenitendea mambo makuu.
Jina lake ni takatifu.
50 Na huwapa rehema zake wale wamchao,
kutoka kizazi hadi kizazi.
51 Ameonesha nguvu ya mkono wake;
Amewatawanya wanaojikweza.
52 Amewaangusha watawala kutoka katika viti vyao vya enzi,
na kuwakweza wanyenyekevu.
53 Amewashibisha wenye njaa kwa mambo mema,
na amewatawanya matajiri bila ya kuwapa kitu.
54 Amemsaidia Israeli, watu aliowachagua ili wamtumikie.
Amekumbuka kuonesha rehema;
55 Maana ndivyo alivyowaahidi baba zetu,
Ibrahimu na wazaliwa wake.”
56 Mariamu alikaa na Elizabeti kwa muda wa kama miezi mitatu, kisha alirudi nyumbani kwake.
© 2017 Bible League International