Book of Common Prayer
Tuishi kwa Kusaidiana Sisi kwa Sisi
6 Ndugu zangu, ikiwa mmoja wenu atakosea, ninyi mnaomfuata Roho mnapaswa kumwendea yule anayetenda dhambi. Msaidieni mtu huyo awe mwenye haki tena. Mfanye hivyo kwa njia ya upole, na muwe waangalifu, kwa maana nanyi pia mnaweza kujaribiwa kutenda dhambi. 2 Msaidiane ninyi kwa ninyi katika kubeba mizigo yenu. Mnapofanya hivi, mtakuwa mnatimiza yote ambayo sheria ya Kristo imewaagiza kufanya. 3 Maana mtu akijiona kuwa yeye ni wa muhimu sana na kumbe sio wa muhimu, anajidanganya mwenyewe. 4 Kila mmoja aipime kazi yake mwenyewe kuona ikiwa kuna chochote cha kujivunia. Kama ndivyo, uyatunze hayo moyoni mwako wala usijilinganishe na mtu mwingine yeyote. 5 Maana sisi sote tunawajibika kwa yale tunayofanya.
Msiache Kutenda Mema
6 Yule anayefundishwa neno la Mungu anapaswa kumshirikisha mwalimu wake mambo mema aliyonayo.
7 Ikiwa mnadhani mnaweza kumdanganya Mungu, mtakuwa mnajidanganya wenyewe. Mtavuna yale mnayopanda. 8 Yule anayepanda kwa kuiridhisha nafsi yake ya dhambi, mavuno yatakayopatikana ni uharibifu kabisa. Lakini mkipanda kwa kuiridhisha Roho, mavuno yenu katika Roho yatakuwa uzima wa milele. 9 Hatupaswi kuchoka katika kutenda mema. Tutapata mavuno yetu kwa wakati sahihi, tusipokata tamaa. 10 Tunapokuwa na nafasi ya kumtendea mema kila mtu, tufanye hivyo. Lakini tuzingatie zaidi kuwatendea mema wale walio wa familia ya waamini.
Yesu Awakaribisha Watoto
(Mt 19:13-15; Mk 10:13-16)
15 Baadhi ya watu waliwaleta hata watoto wao wadogo kwa Yesu ili awawekee mikono kuwabariki. Lakini wafuasi walipoona hili, waliwakataza. 16 Lakini Yesu aliwaalika watoto kwake na kuwaambia wafuasi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu. Msiwazuie, kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wa watu walio kama watoto wadogo hawa. 17 Ukweli ni kwamba, ni lazima uupokee ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo anavyopokea vitu, la si hivyo hautauingia.”
Mtu Tajiri Akataa Kumfuata Yesu
(Mt 19:16-30; Mk 10:17-31)
18 Kiongozi wa dini akamuuliza Yesu, “Mwalimu Mwema, ni lazima nifanye nini ili niweze kuupata uzima wa milele?”
19 Yesu akamwambia, “Kwa nini unaniita mwema? Mungu peke yake ndiye mwema. 20 Na unazijua amri zake: ‘Usizini, usiue, usiibe, usiseme uongo, na ni lazima uwaheshimu baba na mama yako.’”(A)
21 Lakini yule kiongozi akasema, “Nimezitii amri zote hizi tangu nilipokuwa mdogo.”
22 Yesu aliposikia hili, akamwambia, “Lakini kuna jambo moja unatakiwa kufanya. Uza kila kitu ulichonacho na uwape maskini pesa. Utakuwa na utajiri mbinguni. Kisha, njoo unifuate.” 23 Lakini yule mtu aliposikia Yesu anamwambia kutoa pesa zake, alihuzunika. Hakutaka kufanya hivi kwa sababu alikuwa tajiri sana.
24 Yesu alipoona kuwa amehuzunika, akasema, “Itakuwa vigumu sana kwa matajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. 25 Ni rahisi kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
26 Watu waliposikia hili, wakasema, “Sasa ni nani anayeweza kuokolewa?”
27 Yesu akajibu, “Lisilowezekana kwa wanadamu, linawezekana kwa Mungu.”
28 Petro akasema, “Tazama! Tumeacha vyote tulivyokuwa navyo na kukufuata.”
29 Yesu akasema, “Ninaahidi kuwa kila aliyeacha nyumba, mke, ndugu, wazazi, au watoto kwa ajili ya ufalme wa Mungu, 30 atapokea zaidi ya kile alichoacha. Atapokea mara nyingi zaidi katika maisha haya. Na katika ulimwengu ujao atapata mara nyingi zaidi.”
© 2017 Bible League International