Book of Common Prayer
Watu Wamsifu Mungu Mbinguni
19 Baada ya hili nikasikia kitu kilichosikika kama kundi kubwa la watu mbinguni. Walikuwa wakisema:
“Haleluya![a]
Ushindi, utukufu na nguvu ni vyake Mungu wetu.
2 Hukumu zake ni za kweli na za haki.
Mungu wetu amemwadhibu kahaba.
Ndiye aliyeiharibu dunia kwa uzinzi wake.
Mungu amemwadhibu kahaba kulipa kisasi cha vifo vya watumishi wake.”
3 Pia, watu hawa walisema:
“Haleluya!
Anaungua na moshi wake utasimama milele na milele.”
4 Ndipo wazee ishirini na nne na viumbe wenye uhai wanne wakaanguka chini kusujudu wakamwabudu Mungu, akaaye kwenye kiti cha enzi. Wakasema:
“Amina! Haleluya!”
5 Sauti ikatoka kwenye kiti cha enzi na kusema:
“Msifuni Mungu wetu,
ninyi nyote mnaomtumikia!
Msifuni Mungu wetu,
ninyi nyote mlio wadogo na wakubwa mnaomheshimu!”
6 Kisha nikasikia kitu kilichosikika kama kundi kubwa la watu. Kilikuwa na kelele kama mawimbi ya bahari au radi. Watu walikuwa wakisema:
“Haleluya!
Bwana Mungu wetu anatawala.
Ndiye Mwenye Nguvu, Mungu Mwenyezi.
7 Tushangilie na kufurahi na
kumpa Mungu utukufu!
Mpeni Mungu utukufu, kwa sababu arusi ya Mwanakondoo imewadia.
Na bibi arusi wa Mwanakondoo amekwisha jiandaa.
8 Nguo ya kitani safi ilitolewa kwa bibi arusi ili avae.
Kitani ilikuwa safi na angavu.”
(Kitani safi inamaanisha mambo mazuri ambayo watakatifu wa Mungu waliyatenda.)
9 Kisha malaika akaniambia, “Andika hili: Heri ni kwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwanakondoo!” Kisha malaika akasema, “Haya ni maneno ya Mungu mwenyewe.”
10 Kisha nikaanguka chini mbele miguuni pa malaika ili nimwabudu. Lakini malaika akaniambia, “Usiniabudu! Mimi ni mtumishi kama wewe na ndugu zako na dada zako walio na ushuhuda kuhusu Yesu Kristo. Hivyo mwabudu Mungu! Kwa sababu ushuhuda kuhusu Yesu ndiyo roho ya unabii.”
Amua Ikiwa Unaweza Kunifuata
(Mt 10:37-38)
25 Watu wengi walikuwa wanasafiri pamoja na Yesu. Akawaambia, 26 “Ikiwa unakuja kwangu na hauko tayari kuiacha familia yako, huwezi kuwa mfuasi wangu. Ukimpenda zaidi baba yako, mama yako, mke wako, watoto wako, kaka na dada zako na hata maisha yako zaidi yangu huwezi kuwa mwanafunzi wangu. 27 Yeyote ambaye hatauchukua msalaba atakaopewa na akanifuata, hawezi kuwa mfuasi wangu.
28 Ikiwa unataka kujenga nyumba, kwanza utakaa na kuamua ili kujua itakugharimu kiasi gani. Ni lazima uone ikiwa una pesa za kutosha kumaliza kazi ya ujenzi. 29 Usipofanya hivyo, unaweza ukaanza kazi, lakini ukashindwa kumaliza kujenga nyumba. Na usipoweza kuimaliza, kila mtu atakucheka, 30 Watasema, ‘Mtu huyu alianza kujenga, lakini alishindwa kumalizia.’
31 Ikiwa mfalme anakwenda kupigana vita na mfalme mwingine, atakaa chini kwanza na kupanga. Ikiwa ana askari elfu kumi, ataamua ikiwa ana uwezo wa kumshinda mfalme mwenye askari elfu ishirini. 32 Akiona hawezi kumshinda mfalme mwingine, atatuma baadhi ya watu kwa mfalme mwingine ili wapatane akiwa bado yuko mbali.
33 Ndivyo ilivyo kwa kila mmoja wenu. Lazima uache kila kitu ulichonacho. La sivyo, huwezi kuwa mfuasi wangu.
Msipoteze Umuhimu Wenu
(Mt 5:13; Mk 9:50)
34 Chumvi ni kitu kizuri; lakini chumvi ikipoteza ladha yake, huwezi kuitengenezea ladha tena. 35 Haifai. Huwezi hata kuitumia kama uchafu au mbolea. Watu huitupa tu.
Mnaonisikiliza, sikilizeni!”
© 2017 Bible League International