Book of Common Prayer
27 Ninyi nyote kwa pamoja ni mwili wa Kristo. Kila mmoja wenu ni kiungo cha mwili huo. 28 Na Mungu ameweka katika kanisa, kwanza, baadhi kuwa mitume, pili manabii, na tatu walimu. Kisha Mungu ametoa nafasi kwa wale wanaofanya miujiza, wenye karama ya uponyaji, wanaoweza kuwasaidia wengine, wanaoweza kuwaongoza wengine na wale wanaoweza kuzungumza kwa lugha zingine. 29 Je, wote ni mitume? Je, wote ni manabii? Je, wote ni walimu? Je, wote hufanya miujiza? 30 Si wote wenye karama ya uponyaji. Si wote wanaozungumza kwa lugha zingine. Si wote wanaofasiri lugha. 31 Endeleeni kuwa na ari ya kuwa na karama za Roho mnazoona kuwa ni kuu zaidi. Lakini sasa ninataka kuwaonesha njia iliyo kuu zaidi.
Upendo Uwe Dira Yenu
13 Ninaweza kusema kwa lugha zingine, za wanadamu au za malaika. Lakini ikiwa sina upendo, mimi ni kengele yenye kelele na tuazi linalolia. 2 Ninaweza kuwa na karama ya unabii, ninaweza kuzielewa siri zote na kujua kila kitu kinachopaswa kujulikana, na ninaweza kuwa na imani kuu kiasi cha kuhamisha milima. Lakini pamoja na haya yote, ikiwa sina upendo, mimi ni bure. 3 Ninaweza kutoa kila kitu nilichonacho ili niwasaidie wengine na ninaweza hata kuutoa mwili wangu ili niweze kujisifu.[a] Lakini siwezi kupata chochote kwa kufanya haya yote ikiwa sina upendo.
4 Upendo huvumilia na ni mwema. Upendo hauna wivu, haujisifu na haujivuni. 5 Upendo hauna kiburi, hauna ubinafsi na haukasirishwi kirahisi. Upendo hautunzi orodha ya mambo waliyoukosea. 6 Upendo haufurahi wengine wanapokosa, lakini daima hufurahia ukweli. 7 Upendo kamwe haukati tamaa kwa watu. Kamwe hauachi kuamini, kamwe haupotezi tumaini na kamwe hauachi kuvumilia.
8 Upendo hautakoma. Lakini karama zote hizo zitafikia mwisho, hata karama ya unabii, karama ya kusema kwa lugha zingine na karama ya maarifa. 9 Hizi zitakoma kwa sababu maarifa haya na nabii hizi tulizonazo sasa hazijakamilika. 10 Lakini ukamilifu utakapokuja, mambo ambayo hayajakamilika yatakoma.
11 Nilipokuwa mtoto, nilizungumza kama mtoto, niliwaza kama mtoto, na kufanya mipango kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima, niliziacha njia za kitoto. 12 Ndivyo ilivyo hata kwetu. Kwa sasa tunamwona Mungu kwa taswira tu kama ilivyo katika kioo. Lakini, baadaye, tutamwona uso kwa uso. Kwa sasa ninajua sehemu tu, lakini wakati huo nitajua kila kitu, kama ambavyo Mungu amenijua mimi. 13 Hivyo mambo haya matatu yanaendelea; imani, tumaini na upendo. Na lililo kuu zaidi ya haya yote ni upendo.
Simulizi Kuhusu Msamaha
21 Kisha Petro akamwendea Yesu na kumwuliza, “Bwana, ndugu yangu akiendelea kunikosea, ninapaswa kumsamehe anaponikosea mara ngapi? Mara saba?”
22 Yesu akamjibu, “Ninakwambia, ni lazima umsamehe zaidi ya mara saba. Ni lazima uendelee kumsamehe hata kama atakukosea saba mara sabini.[a]
23 Ninawaambia kwa sababu ufalme wa Mungu unafanana na mfalme aliyetaka kupata taarifa kutoka kwa watumishi wake. 24 Mtumishi aliyekuwa anadaiwa na mfalme tani 300[b] za fedha aliletwa kwake. 25 Hakuwa na fedha za kutosha kulipa deni lake. Hivyo mfalme aliamuru kila kitu anachomiliki mtumishi yule kiuzwe ikiwa ni pamoja na mke na watoto wake.
26 Lakini mtumishi alipiga magoti na kumsihi mfalme akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’ 27 Mfalme alimhurumia. Hivyo akamsamehe yule mtumishi deni lote na akamwacha aende akiwa huru.
28 Lakini mtumishi huyo alipoondoka, alimwona mtumishi mwingine aliyekuwa anamdai sarafu mia za fedha. Akamkaba shingo yake na akasema, ‘Nilipe pesa ninayokudai!’
29 Mtumishi anayedaiwa akapiga magoti na kumsihi akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’
30 Lakini mtumishi wa kwanza alikataa kumvumilia. Alimwambia hakimu kuwa alikuwa anamdai pesa, na mtumishi yule alitupwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa deni lake. 31 Watumishi wengine walipoona hili, walimhurumia mtumishi aliyefungwa gerezani. Hivyo walienda na kumwambia mfalme kila kitu kilichotokea.
32 Ndipo mfalme alimwita msimamizi wa kwanza na kumwambia, ‘Wewe ni mbaya sana! Ulinisihi nikusamehe deni lako, na nilikuacha ukaondoka bila kulipa kitu chochote! 33 Hivyo ulipaswa kumpa mtu yule mwingine anayetumika pamoja nawe rehema ile ile niliyokupa mimi.’ 34 Mfalme alikasirika sana. Hivyo alifungwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa kila kitu anachodaiwa.
35 Mfalme huyu alifanya kama ambavyo Baba yangu wa mbinguni atawafanyia ninyi. Ni lazima umsamehe ndugu au dada yako kwa moyo wako wote, usipofanya hivyo, Baba yangu wa mbinguni hatakusamehe wewe.”
© 2017 Bible League International