Book of Common Prayer
Mwana wa Mungu yu sawa na Mungu
15 Hakuna anayeweza kumwona Mungu,
lakini Mwana anafanana kabisa na Mungu.
Anatawala juu ya kila kitu kilichoumbwa.
16 Kwa uweza wake, vitu vyote viliumbwa:
vitu vya angani na ardhini, vinavyoonekana na visivyoonekana,
watawala wote wa kiroho, wakuu, enzi, na mamlaka.
Kila kitu kiliumbwa kupitia Yeye na kwa ajili yake.
17 Mwana alikuwapo kabla ya kuumbwa kitu chochote,
na vyote vinaendelea kuwepo kwa sababu yake.
18 Yeye ni kichwa cha mwili,
yaani kanisa.
Yeye ni mwanzo wa maisha yajayo,
ni wa kwanza miongoni mwa wote watakaofufuliwa kutoka kwa wafu.[a]
Hivyo katika mambo yote yeye ni mkuu zaidi.
19 Mungu alipendezwa kwamba ukamilifu wa uungu wake
uishi ndani ya Mwana.
20 Na kupitia Yeye, Mungu alifurahi
kuvipatanisha tena vitu vyote kwake Yeye mwenyewe;
vilivyoko mbinguni na vilivyoko duniani.
Mungu alileta amani kupitia sadaka ya damu ya Mwanaye msalabani.
21 Hapo mwanzo mlitengwa na Mungu, na mlikuwa adui zake katika fikra zenu, kwa sababu ya maovu mliyotenda kinyume naye. 22 Lakini sasa amewafanya kuwa marafiki zake tena, kupitia kifo cha Kristo katika mwili wake. Ili kwa njia hiyo awalete kwake mkiwa watakatifu, msio na lawama na msiohukumiwa jambo lolote mbele zake; 23 na hiki ndicho kitatokea mkiendelea kuiamini Habari Njema mliyoisikia. Mwendelee kuwa imara na kudumu katika imani. Jambo lolote lisiwafanye mkaliacha tumaini lenu mlilopokea mlipoisikia Habari Njema. Habari Njema ile ile ambayo imehubiriwa kwa kila mtu duniani, ndiyo kazi ambayo mimi, Paulo, nilipewa kufanya.
Yesu Azungumza Juu ya Roho Mtakatifu
37 Siku ya mwisho ya kusherehekea sikukuu ikafika. Nayo Ilikuwa siku muhimu zaidi. Katika siku hiyo Yesu alisimama na kusema kwa sauti kubwa, “Yeyote aliye na kiu aje kwangu anywe. 38 Kama mtu ataniamini, mito ya maji yenye uzima itatiririka kutoka ndani ya moyo wake. Ndivyo Maandiko yanavyosema.” 39 Yesu alikuwa anazungumza juu ya Roho Mtakatifu ambaye alikuwa hajatolewa kwa watu bado, kwa sababu Yesu naye alikuwa bado hajatukuzwa. Ingawa baadaye, wale waliomwamini Yesu wangempokea huyo Roho.
Watu Wanabishana Juu ya Yesu
40 Watu waliposikia maneno aliyosema Yesu, baadhi yao wakasema, “Hakika mtu huyu ni nabii.”[a]
41 Wengine wakasema, “Huyu ni Masihi.”
Na wengine wakasema, “Masihi hawezi kutoka Galilaya. 42 Maandiko yanasema kwamba Masihi atatoka katika ukoo wa Daudi. Na wanasema kwamba atatoka Bethlehemu, mji alimoishi Daudi.” 43 Kwa jinsi hiyo watu hawakukubaliana wao kwa wao kuhusu Yesu. 44 Baadhi yao wakataka kumkamata. Lakini hakuna aliyejaribu kufanya hivyo.
Baadhi ya Viongozi wa Kiyahudi Wakataa Kuamini
45 Walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Makuhani na Mafarisayo wakawauliza, “Kwa nini hamjamleta Yesu?”
46 Walinzi wa Hekalu wakajibu, “Hatujawahi kumsikia mtu akisema mambo ya ajabu kiasi hicho!”
47 Mafarisayo wakajibu, “Kwa hiyo Yesu amewadanganya hata ninyi? 48 Hamuoni kuwa hakuna kiongozi yeyote wala sisi Mafarisayo anayemwamini? 49 Lakini watu hao walio nje wasiojua sheria wamo katika laana ya Mungu.”
50 Lakini Nikodemu alikuwa katika kundi lile. Naye ndiye yule aliyekwenda kumwona Yesu pale mwanzo.[b] Naye akasema, 51 “Sheria yetu haitaturuhusu kumhukumu mtu na kumtia hatiani kabla ya kumsikiliza kwanza na kuyaona aliyotenda?”
52 Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Wewe nawe utakuwa umetoka Galilaya. Jifunze Maandiko. Hutapata lolote kuhusu nabii[c] anayetoka Galilaya.”
© 2017 Bible League International