Book of Common Prayer
Yesu Kristo Ndiye Kuhani Wetu Mkuu
14 Tunaye kuhani mkuu sana ambaye ameenda kuishi na Mungu kule mbinguni. Yeye ni Yesu Mwana wa Mungu. Hivyo tuendelee kuitamka imani yetu katika yeye. 15 Yesu, kuhani wetu mkuu, anaweza kuuelewa udhaifu wetu. Yesu alipoishi duniani, alijaribiwa katika kila njia. Alijaribiwa kwa njia hizo hizo tunazojaribiwa, lakini hakutenda dhambi. 16 Tukiwa na Yesu kama kuhani wetu mkuu, tunaweza kujisikia huru kuja mbele za kiti cha enzi cha Mungu ambako kuna neema. Hapo tunapata rehema na neema ya kutusaidia tunapokuwa tunahitaji.
5 Kila kuhani Mkuu wa Kiyahudi alichaguliwa kutoka miongoni mwa watu. Kuhani huyo anapewa kazi ya kuwasaidia watu katika mambo wanayopaswa kumfanyia Mungu. Anapaswa kumtolea Mungu sadaka na sadaka za dhambi. 2 Kuhani mkuu anao udhaifu wake binafsi. Hivyo anapaswa kuwa mpole kwa wale wanaokosea kwa sababu ya kutokujua. 3 Hutoa sadaka kwa ajili ya dhambi zao, lakini kutokana na udhaifu wake anapaswa pia kutoa sadaka kwa ajili dhambi zake mwenyewe.
4 Kuwa kuhani mkuu ni heshima. Lakini hayupo anayejichagua mwenyewe kwa ajili ya kazi hii. Mtu huyo anapaswa kuwa amechaguliwa na Mungu kama alivyokuwa Haruni. 5 Ndivyo ilivyo hata kwa Kristo. Hakujichagua mwenyewe kuwa na heshima na kuwa kuhani mkuu. Lakini Mungu alimchagua. Mungu akamwambia:
“Wewe ni mwanangu.
Leo nimekuwa baba yako.”(A)
6 Na katika sehemu nyingine ya Maandiko Mungu anasema:
“Wewe ni kuhani mkuu milele;
kama Melkizedeki alivyokuwa kuhani.”(B)
Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya
(Mt 17:1-8; Mk 9:2-8)
28 Baada ya siku kama nane tangu Yesu aseme maneno haya, aliwachukua Petro, Yohana na Yakobo, akapanda mlimani kuomba. 29 Yesu alipokuwa akiomba, uso wake ulianza kubadilika. Nguo zake zikawa nyeupe, zikang'aa. 30 Kisha watu wawili walikuwa pale, wakiongea naye. Walikuwa Musa na Eliya; 31 Wao pia walionekana waking'aa na wenye utukufu. Walikuwa wanazungumza na Yesu kuhusu kifo chake kitakachotokea Yerusalemu. 32 Petro na wenzake walikuwa wanasinzia. Lakini waliamka na kuuona utukufu wa Yesu. Waliwaona pia watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye. 33 Musa na Eliya walipokuwa wanaondoka, Petro akasema, “Mkuu, ni vizuri tuko hapa. Tutajenga vibanda vitatu hapa, kimoja kwa ajili ya kukutukuza wewe, kingine kwa ajili kumtukuza Musa na kingine wa ajili ya kumtukuza Eliya.” Petro hakujua alichokuwa anasema.
34 Petro alipokuwa akisema mambo haya, wingu likaja, likawafunika wote. Petro, Yohana na Yakobo waliogopa walipofunikwa na wingu. 35 Sauti ikatoka katika wingu na kusema, “Huyu ni Mwanangu. Ndiye niliyemchagua. Mtiini yeye.”
36 Sauti hiyo ilipomalizika, Yesu peke yake ndiye alikuwa pale. Petro, Yohana na Yakobo hawakusema chochote. Na kwa muda mrefu baada ya hilo, hawakumwambia mtu yeyote yale waliyoyaona.
© 2017 Bible League International