Book of Common Prayer
Watoto na Wazazi Wao
6 Watoto, watiini wazazi wenu katika namna ambayo Bwana anataka, kwa sababu hili ni jambo sahihi kutenda. 2 Amri husema, “Waheshimu baba yako na mama yako.”(A) Hii ndiyo amri ya kwanza iliyo na ahadi pamoja nayo. 3 Na hii ndiyo ahadi: “Ndipo utakapofanikiwa, na utakuwa na maisha marefu duniani.”(B)
4 Wababa, msiwakasirishe watoto wenu, lakini waleeni kwa mafunzo na mausia mliyopokea kutoka kwa Bwana.
Watumwa na Bwana
5 Watumwa, watiini bwana zenu hapa duniani kwa hofu na heshima. Na fanyeni hivi kwa moyo ulio wa kweli, kama mnavyomtii Kristo. 6 Mfanye hivi siyo tu kwa kuwafurahisha bwana zenu wakati wanapowaona, bali wakati wote. Kwa vile ninyi hakika ni watumwa wa Kristo, mfanye kwa mioyo yenu yale Mungu anayotaka. 7 Fanyeni kazi zenu, na mfurahie kuzifanya. Fanyeni kana kwamba mnamtumikia Bwana, siyo tu bwana wa duniani. 8 Kumbukeni kwamba Bwana atampa kila mmoja zawadi kwa kufanya vema. Kila mmoja, mtumwa au aliye huru, atapata zawadi kwa mambo mema aliyotenda.
9 Mabwana, kwa jinsi hiyo hiyo, muwe wema kwa watumwa wenu. Msiseme mambo ya kuwatisha. Mnajua kuwa yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, na humchukulia kila mmoja sawa.
Yesu Atuliza Dhoruba
(Mt 8:23-27; Lk 8:22-25)
35 Siku ile ilipofika jioni aliwaambia, “Hebu tuvuke kwenda ng'ambo ya pili ya ziwa.” 36 Kwa hiyo wakaliacha lile kundi. Wakamchukua pamoja nao alipokuwa amerudi katika mtumbwi. Wakati ule ule palikuwepo na mitumbwi mingi mingine ziwani. 37 Dhoruba kubwa ikatokea na mawimbi yalikuwa yanakuja katika pembe zote za mtumbwi. Mtumbwi nao ulikaribia kujaa maji kabisa 38 lakini Yesu alikuwa amelala nyuma ya mtumbwi akiegemea mto. Wakamwaamsha na kumwambia, “Mwalimu je wewe hujali kwamba tunazama?”
39 Kisha akainuka, akaukemea upepo, na akaliamuru ziwa, “Nyamaza Kimya! Tulia!” Upepo ule ukatulia na ziwa nalo likatulia kabisa.
40 Kisha akawaambia, “Kwa nini mnaogopa? Je! Bado hamna imani yoyote?”
41 Lakini walikuwa na woga sana, na wakasemezana wao kwa wao, “Ni nani basi huyu ambaye hata upepo na ziwa vinamtii?”
© 2017 Bible League International