Book of Common Prayer
Kutoka Mauti hadi Uzima
2 Zamani mlikuwa wafu kiroho kwa sababu ya dhambi na mambo mliyotenda kinyume na Mungu. 2 Ndiyo, zamani maisha yenu yalijaa dhambi hizo. Mliishi kwa namna ya ulimwengu; mkimfuata mkuu wa nguvu za uovu[a] zilizo katika anga, roho hiyo hiyo inatenda kazi sasa ndani ya watu wasiomtii Mungu. 3 Tuliishi hivyo zamani, tukijaribu kuzifurahisha tamaa zetu za mwili. Tulitenda mambo ambayo miili na akili zetu zilitaka. Kama ilivyo kwa kila mtu ulimwenguni, tulistahili kuteseka kutokana na hasira ya Mungu kwa sababu ya jinsi tulivyokuwa.
4 Lakini Mungu ni mwingi wa rehema na anatupenda sana. 5 Tulikuwa wafu kiroho kwa sababu ya matendo maovu tuliyotenda kinyume naye. Lakini yeye alitupa maisha mapya pamoja na Kristo. (Mmeokolewa na neema ya Mungu.) 6 Ndiyo, ni kwa sababu sisi ni sehemu ya Kristo Yesu, ndiyo maana Mungu alitufufua pamoja naye kutoka kwa wafu na akatuketisha pamoja naye mbinguni. 7 Mungu alifanya hivi ili wema wake kwetu sisi tulio wa Kristo Yesu uweze kuonesha nyakati zote zijazo utajiri wa ajabu wa neema yake.
8 Nina maana ya kuwa mmeokolewa kwa neema kwa sababu mliweka imani yenu kwake.[b] Hamkujiokoa ninyi wenyewe; bali ni zawadi kutoka kwa Mungu. 9 Msijisifu kwa kuwa hamkuokolewa kutokana na matendo yenu. 10 Mungu ndiye aliyetufanya hivi tulivyo. Ametuumba wapya katika Kristo Yesu ili tutende mambo mema katika maisha yetu. Mambo aliyokwisha kutupangia.
Yesu Awaponya Watu Wengi
(Mt 8:14-17; Lk 4:38-41)
29 Wakaondoka kutoka katika sinagogi na mara hiyo hiyo wakaenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. 30 Mara Yesu alipoingia ndani ya nyumba watu wakamweleza kuwa mama mkwe wake Simoni alikuwa mgonjwa sana na alikuwa amepumzika kitandani kwa sababu alikuwa na homa. 31 Yesu akasogea karibu na kitanda, akamshika mkono na kumsaidia kusimama juu. Ile homa ikamwacha, na yeye akaanza kuwahudumia.
32 Ilipofika jioni, baada ya jua kuzama waliwaleta kwake watu wote waliokuwa wagonjwa na waliokaliwa na mashetani. 33 Mji mzima ulikusanyika mlangoni pale. 34 Naye akawaponya watu waliokuwa na magonjwa ya kila aina, na kufukuza mashetani wengi. Lakini yeye hakuyaruhusu mashetani kusema, kwa sababu yalimjua.[a]
Yesu Aenda Katika Miji Mingine
(Lk 4:42-44)
35 Asubuhi na mapema, ilipokuwa giza na bado hakujapambazuka, Yesu aliamka na kutoka kwenye nyumba ile na kwenda mahali ili awe peke yake na kuomba. 36 Lakini Simoni na wale wote waliokuwa pamoja naye waliondoka kwenda kumtafuta Yesu 37 na walipompata, wakamwambia, “kila mmoja anakutafuta.”
38 Lakini Yesu akawaambia, “Lazima twende kwenye miji mingine iliyo karibu na hapa, ili niweze kuhubiri huko pia, kwa sababu hilo ndilo nililokuja kulifanya.” 39 Hivyo Yesu alienda katika wilaya yote iliyoko mashariki mwa ziwa la Galilaya akihubiri Habari Njema katika masinagogi na kuwafungua watu kutoka katika nguvu za mashetani.
Yesu Amponya Mgonjwa
(Mt 8:1-4; Lk 5:12-16)
40 Ikatokea mtu mmoja mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwendea Yesu na kupiga magoti hadi chini akimwomba msaada. Mtu huyo mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi akamwambia Yesu, “Kama utataka, wewe una uwezo wa kuniponya nikawa safi.”
41 Aliposikia maneno hayo Yesu akakasirika.[b] Lakini akamhurumia. Akautoa mkono wake na kumgusa mtu yule mwenye ugonjwa mbaya sana wa ngozi, na kumwambia, “Ninataka kukuponya. Upone!” 42 Mara moja ugonjwa ule mbaya sana wa ngozi ulimwacha, naye akawa safi.
43 Baada ya hayo Yesu akampa maonyo yenye nguvu na kumruhusu aende zake mara moja. 44 Akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea. Lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze,[c] Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru[d] watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona kwa kuwa safi tena. Ukayafanye haya ili yawe uthibitisho kwa kila mmoja ya kwamba umeponywa.” 45 Lakini mtu yule aliondoka hapo na kwenda zake, na huko alianza kuzungumza kwa uhuru kamili na kusambaza habari hizo. Matokeo yake ni kwamba Yesu asingeweza tena kuingia katika mji kwa wazi wazi. Ikamlazimu kukaa mahali ambapo hakuna watu. Hata hivyo watu walikuja toka miji yote na kumwendea huko.
© 2017 Bible League International