Book of Common Prayer
13 Watu hawa wote mashuhuri wakaendelea kuishi kwa imani hadi walipofariki. Hawakuwa wamepata mambo ambayo Mungu aliwaahidi watu wake. Lakini walikuwa na furaha kuona tu kwamba ahadi hizi zilikuwa zinakuja kwa mbali siku zijazo. Waliukubali ukweli kwamba wao walikuwa kama wageni na wasafiri hapa duniani. 14 Watu wanapolikubali jambo la namna hiyo, wanaonesha kuwa wanaingojea nchi itakayokuwa yao wenyewe. 15 Kama wangekuwa wanaifikiria nchi walikotoka, wangekuwa wamerejea. 16 Lakini walikuwa wanaingoja nchi iliyo bora zaidi, nchi ya mbinguni. Hivyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao. Naye amewaandalia mji.
17-18 Mungu aliijaribu imani ya Ibrahimu. Mungu alimtaka amtoe Isaka kama sadaka. Ibrahimu akatii kwa sababu alikuwa na imani. Tayari alikuwa na ahadi kutoka kwa Mungu. Na Mungu tayari alikuwa amekwishamwambia, “Ni kupitia kwa Isaka kwamba vizazi vyako watakuja.”(A) Lakini Ibrahimu alikuwa tayari kumtoa mwana wake wa pekee. Alifanya hivi kwa sababu alikuwa na imani. 19 Aliamini kwamba Mungu angeweza kuwafufua watu kutoka kifoni. Na hakika, Mungu alipomzuia Ibrahimu katika kumuua Isaka, ilikuwa ni kama vile alimpata tena kutoka kifoni.
20 Isaka akayabariki maisha ya mbeleni ya Yakobo na Esau. Alifanya hivyo kwa sababu alikuwa na imani. 21 Na Yakobo, pia kwa vile alikuwa na imani, alimbariki kila mmoja wa wana wa Yusufu. Alifanya haya wakati alipokuwa akifa, akaiegemea fimbo yake akimwabudu Mungu.
22 Na Yusufu alipokuwa karibu amefariki, alizungumza kuhusu watu wa Israeli kuondoka Misri. Na aliwaambia yale waliyotakiwa kuufanyia mwili wake. Alifanya haya kwa sababu alikuwa na imani.
Yesu Mchungaji Mwema
7 Hivyo Yesu akasema tena, “Hakika ninawaambia, Mimi ni mlango wa kondoo. 8 Wote walionitangulia walikuwa wezi na wanyang'anyi. Kondoo hawakuwasikiliza hao. 9 Mimi ni mlango. Yeyote anayeingia kupitia kwangu ataokoka. Ataweza kuingia na kutoka nje. Atapata kila anachohitaji. 10 Mwizi anakuja kuiba, kuua, na kuangamiza. Lakini mimi nilikuja kuwaletea uzima, na muwe nao kwa ukamilifu.
11 Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huyatoa maisha yake kwa ajili ya kondoo. 12 Mtumishi anayelipwa ili kuwachunga kondoo yuko tofauti na mchungaji. Mtumishi wa mshahara, kondoo siyo mali yake. Hivyo anapomwona mbwa mwitu anakuja, hukimbia na kuwaacha kondoo peke yao. Mbwa mwitu huwashambulia na kuwatawanya kondoo. 13 Mtu huyu huwakimbia kondoo kwa sababu yeye ni mfanyakazi wa mshahara tu. Hawajali kabisa kondoo.
14-15 Mimi ni mchungaji ninayewajali kondoo. Nawafahamu kondoo wangu kama ambavyo Baba ananijua mimi. Na kondoo wananijua kama nami ninavyomjua Baba. Nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo hawa. 16 Nina kondoo wengine ambao hawamo kwenye kundi hili hapa. Hao nao napaswa kuwaongoza. Kwani wataisikia sauti yangu. Baadaye kutakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja.[a] 17 Baba ananipenda kwa sababu nautoa uhai wangu. Nautoa uhai wangu ili niweze kuuchukua tena.
© 2017 Bible League International