Book of Common Prayer
Maonyo juu ya Walimu wa uongo
4 Roho anasema wazi wazi kwamba katika siku za mwisho wengine watajitenga na imani. Watazitii roho zinazodanganya, na kufuata mafundisho ya mashetani. 2 Mafundisho hayo yanafundishwa na watu wanaodanganya na kuwafanyia hila wengine. Watu hawa waovu hawapambanui kati ya mema na maovu. Ni kana kwamba dhamiri zao zimeharibiwa kwa chuma cha moto. 3 Wanasema ni vibaya kuoa. Na wanasema kwamba kuna baadhi ya vyakula ambavyo watu lazima wasile. Lakini Mungu aliumba vyakula hivi, na wale wanaoamini na kuelewa ukweli wanaweza kuvila kwa shukrani. 4 Kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, hakuna chakula kitakachokataliwa kama kikikubaliwa kwa shukrani. 5 Kila kitu alichokiumba kiliumbwa kitakatifu kwa namna alivyosema na kwa maombi.
Uwe Mtumishi Mwema wa Kristo Yesu
6 Waambie haya kaka na dada huko. Hii itakuonesha wewe kuwa ni mtumishi mwema wa Kristo Yesu. Utaonyesha kwamba umefundishwa maneno ya imani na mafundisho mazuri uliyoyafuata. 7 Usitumie muda wowote katika masimulizi ya kipuuzi ambayo hayakubaliani na ukweli wa Mungu. Badala yake jizoeshe mwenyewe kuishi maisha ya kumheshimu na kumpendeza Mungu. 8 Kufanya mazoezi ya mwili wako kuna manufaa kidogo kwako. Lakini kujaribu kumpendeza Mungu kwa njia zote kunakufaa zaidi. Kunakuletea baraka katika maisha haya na maisha ya baadaye pia. 9 Huu ni usemi wa kweli ambao unaweza kukukubaliwa bila kuuliza swali: 10 Tunayo matumaini kwa Mungu aliye hai, Mwokozi wa watu wote. Ambaye hasa, ni Mwokozi wa wale wote wanaomuamini. Na hii ndiyo sababu tunafanya kazi na kupambana.
11 Amuru na kufundisha mambo haya. 12 Wewe ni kijana, lakini usiruhusu yeyote kukufanya wewe kama si mtu muhimu. Uwe mfano kuonesha waamini namna wanavyoweza kuishi. Waoneshe kwa namna unavyosema, unavyoishi, unavyopenda, unavyo amini, na namna ya maisha yako safi.
13 Endelea kusoma Maandiko kwa watu, watie moyo, na uwafundishe. Fanya hivyo mpaka nitakapo kuja. 14 Kumbuka kutumia kipawa ulichonacho, ambacho ulipewa kupitia unabii wakati kundi la wazee lilipo kuweka mikono juu yako. 15 Endelea kufanya haya, na jitoe maisha yako kutenda hayo. Kisha kila mtu anaweza kuona namna ilivyo vema unavyotenda. 16 Uwe mwangalifu katika maisha na mafundisho yako. Endelea kuishi na kufundisha kwa usahihi. Kisha, utajiokoa mwenyewe na wale wanaosikiliza mafundisho yako.
Yesu Atakufa Yerusalemu
(Mt 23:37-39)
31 Wakati huo huo baadhi ya Mafarisayo wakaja kwa Yesu, na wakamwambia, “Ondoka hapa, nenda ukajifiche. Kwa sababu Herode anataka kukuua!”
32 Lakini Yesu akawaambia, “Nendeni, mkamwambie yule mbweha,[a] ‘Leo na kesho ninatoa pepo wachafu na kuponya watu, na kesho kazi itakwisha.’ 33 Baada ya hilo, ni lazima niende, kwa sababu manabii wote wanapaswa kufia Yerusalemu.
34 Yerusalemu! Yerusalemu! Uwauaye manabii. Unawapiga kwa mawe watu waliotumwa na Mungu kwako. Mara ngapi nimetaka kuwasaidia watu wako! Nilitaka kuwakusanya kama kuku anavyovikusanya vifaranga vyake chini ya mbawa zake. Lakini hukuniruhusu. 35 Mungu atakuacha ukiwa. Ninawaambia, hamtaniona tena mpaka wakati ule mtakaposema, ‘Karibu! Mungu ambariki yeye ajaye katika jina la Bwana.’”(A)
© 2017 Bible League International