Book of Common Prayer
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Sardi
3 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi:
Huu ni ujumbe kutoka kwake Yeye mwenye roho saba na nyota saba.
Ninayajua matendo yako. Watu husema kuwa u hai, lakini hakika umekufa. 2 Amka! Jitie nguvu kabla ya nguvu kidogo uliyonayo haijakuishia kabisa. Unachofanya hakistahili kwa Mungu wangu. 3 Hivyo usisahau kile ulichopokea na kusikia. Ukitii. Geuza moyo na maisha yako! Amka, la sivyo nitakuja kwako na kukushtukiza kama mwizi. Hautajua wakati nitakapokuja.
4 Lakini una watu wachache katika kundi lako hapo Sardi waliojiweka safi. Watatembea pamoja nami. Watavaa nguo nyeupe, kwa kuwa wanastahili. 5 Kila atakayeshinda atavikwa nguo nyeupe kama wao. Sitayafuta majina yao katika kitabu cha uzima. Nitawakiri mbele za Baba yangu na malaika zake ya kuwa wao ni wangu. 6 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000
(Mt 14:13-21; Mk 6:30-44; Lk 9:10-17)
6 Baadaye, Yesu akavuka Ziwa Galilaya (ambalo pia linaitwa Ziwa Tiberia). 2 Umati mkubwa wa watu ukamfuata kwa sababu waliona ishara za miujiza alizofanya kwa kuponya wagonjwa. 3 Yesu akapanda mlimani na kukaa pale pamoja na wafuasi wake. 4 Siku hizo sherehe ya Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.
5 Yesu akainua macho yake na kuuona umati wa watu ukija kwake. Akamwambia Filipo, “Tunaweza kununua wapi mikate ya kuwatosha watu hawa wote?” 6 Alimwuliza Filipo swali hili ili kumjaribu. Yesu alikwishajua kile alichopanga kufanya.
7 Filipo akajibu, “Wote tunapaswa kufanya kazi kwa mwezi mmoja ili kununua mikate ya kutosha na kumpa kila mmoja aliyepo angalau kipande kidogo.”
8 Mfuasi mwingine aliyekuwepo alikuwa Andrea, ndugu yake Simoni Petro. Andrea akasema, 9 “Yupo hapa kijana mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wadogo wawili. Lakini hiyo haitoshi kwa umati huu wa watu.”
10 Yesu akasema, “Mwambieni kila mtu akae chini.” Sehemu hiyo ilikuwa yenye nyasi nyingi, na wanaume wapatao 5,000 walikaa hapo. 11 Yesu akaichukua ile mikate akamshukuru Mungu kwa ajili ya hiyo. Kisha akawapa watu waliokuwa wakisubiri kula. Alifanya vivyo hivyo kwa samaki. Akawapa watu kadiri walivyohitaji.
12 Wote hao wakawa na chakula cha kutosha. Walipomaliza kula, Yesu akawaambia wafuasi wake, “Kusanyeni vipande vya samaki vilivyobaki na mikate ambayo haikuliwa. Msipoteze chochote.” 13 Hivyo wakakusanya vipande vilivyobaki wakajaza vikapu 12 vikubwa vya mikate ya ngano iliyowabakia wale waliokula. Watu walikuwa wameanza kula wakiwa na vipande vitano tu vya mikate ya ngano.
14 Watu waliiona ishara hii aliyoifanya Yesu na kusema, “Huyu atakuwa ndiye yule Nabii[a] anayekuja ulimwenguni!”
© 2017 Bible League International