Book of Common Prayer
10 Na sasa ninawaamuru wale walio katika ndoa. Si amri kutoka kwangu, lakini ndivyo Bwana aliamuru. Mke hapaswi kuondoka kwa mume wake. 11 Lakini ikiwa mke anaondoka, anapaswa kukaa bila kuolewa au arudi kwa mume wake. Na mume hapaswi kumtaliki mke wake.
12 Ushauri nilionao kwa wengine unatoka kwangu. Bwana hajatupa mafundisho mengine kuhusu hili. Ukiwa na mke asiyeamini, usimtaliki ikiwa yuko radhi kuendelea kuishi pamoja nawe. 13 Na kama una mume asiyeamini, usimtaliki ikiwa yuko radhi kuendelea kuishi pamoja nawe. 14 Mume asiyeamini ametengwa kwa ajili ya Bwana kupitia mke wake anayeamini. Na mke asiyeamini ametengwa kwa ajili ya Bwana kupitia mume wake anayeamini. Ikiwa hii si sahihi basi watoto wenu wasingefaa kwa ajili ya kumwabudu Mungu. Lakini sasa wametengwa kwa ajili yake.
15 Lakini mume au mke asiyemwamini akiamua kuondoka katika ndoa. Hili linapotokea, ndugu aliye katika Kristo anakuwa huru. Mungu aliwachagua ili muwe na maisha ya amani. 16 Inawezekana ninyi wake mtawaokoa waume zenu; nanyi waume mtawaokoa wake zenu kwani bado hamjui kitakachotokea baadaye.
Ishini Kama Mlivyokuwa Mungu Alivyowaita
17 Kila mmoja wenu anapaswa kuendelea kuishi katika namna ambayo Bwana Mungu amewapa, kuishi kama mlivyoishi Mungu alipowaita. Ninawaambia watu katika makanisa yote kufuata kanuni hii. 18 Mwanaume asibadili tohara yake ikiwa alikuwa ametahiriwa alipoitwa. Ikiwa hakuwa ametahiriwa alipoitwa, asitahiriwe. 19 Kutahiriwa au kutotahiriwa si muhimu. Kilicho muhimu ni kutii amri za Mungu. 20 Kila mmoja wenu awe katika hali aliyokuwa nayo Mungu alipomwita. 21 Usijisikie vibaya ikiwa ulipochaguliwa na Mungu ulikuwa mtumwa. Lakini ikiwa unaweza kujikomboa, basi fanya hivyo. 22 Kama ulikuwa mtumwa Bwana alipokuita, uko huru sasa katika Bwana. Wewe ni wa Bwana. Vivyo hivyo, kama ulikuwa huru ulipoitwa, wewe ni mtumwa wa Kristo sasa. 23 Mungu alilipa gharama kubwa kwa ajili yako, hivyo usiwe mtumwa kwa mtu yeyote tena. 24 Ndugu zangu, katika maisha yenu mapya pamoja na Mungu, kila mmoja wenu anapaswa kuendelea kuwa katika hali ya tohara kama alivyokuwa Mungu alipowaita.
Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Wachafu
(Mt 8:28-34; Lk 8:26-39)
5 Wakafika ng'ambo ya ziwa, katika nchi walimoishi Wagerasi.[a] 2 Yesu alipotoka katika mashua ile ghafla, mtu mmoja aliyekuwa na roho chafu alitoka makaburini kuja kumlaki. 3 Mtu huyu aliishi makaburini, na hakuna mtu yeyote aliyeweza kumfunga hata kwa mnyororo, 4 Watu walijaribu kila mara kumfunga kwa minyororo na vyuma kwenye miguu na mikono. Hata hivyo, aliweza kuivunja minyororo ile na pingu zile za vyuma wala hakuna aliyekuwa na nguvu za kutosha kumdhibiti. 5 Kila mara usiku na mchana akiwa makaburini na kwenye milima alipiga kelele na kujikata kwa mawe.
6 Alipomwona Yesu kutoka mbali, alimkimbilia, na kusujudu mbele yake. 7 Kisha akalia kwa sauti kubwa na kusema, “Unataka nini kwangu, Yesu Mwana wa Mungu Aliye Mkuu zaidi? Nakuomba uape mbele za Mungu kwamba hutanitesa.” 8 Yule pepo alisema haya kwa sababu Yesu alikuwa anamwambia, “Mtoke huyo mtu, ewe pepo mchafu!”
9 Ndipo Yesu akamwuliza yule mtu, “Jina lako nani?”
Naye akamjibu, “Jina langu ni Jeshi,[b] kwa sababu tuko wengi.” 10 Yule pepo akamwomba Yesu tena na tena asiwaamuru kutoka katika eneo lile.
11 Kulikuwepo kundi kubwa la nguruwe likila katika kilima. 12 Wale pepo wakamwomba Yesu awatume waende katika lile kundi la nguruwe na kuliingia, 13 Naye akawaruhusu. Kwa hiyo pepo wachafu walimtoka mtu yule na kuwaingia nguruwe.[c] Kundi lile lilikuwa na idadi karibu ya elfu mbili, lilikimbia kuelekea kwenye kingo zenye mtelemko mkali na kutumbukia ziwani, ambamo walizama.
14 Wale waliowachunga walikimbia. Wakatoa taarifa mjini na katika maeneo jirani ya mashambani. Watu wakaja kuona ni kitu gani kilichotokea. 15 Watu hao wakamwendea Yesu. Nao wakamwona yule aliyekuwa na mashetani ameketi mahali pale, amevaa nguo na akiwa mwenye akili zake nzuri; huyu ni yule aliyekuwa amepagawa na jeshi la mashetani. Wakaogopa. 16 Wale waliokuwa wameona hili waliwasimulia kile kilichomtokea mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani na kuhusu nguruwe wale. 17 Nao wakamwomba Yesu aondoke katika eneo lile.
18 Wakati Yesu akipanda katika mtumbwi, mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani alimwomba Yesu afuatane naye. 19 Lakini Yesu hakumruhusu aende naye, isipokuwa alimwambia, “Nenda kwa watu wa kwenu, na uwaambie yote ambayo Bwana amekufanyia, na uwaambie jinsi alivyokuwa na huruma kwako.”
20 Hivyo mtu yule aliondoka, na akaanza kuwaeleza watu katika Dekapoli[d] mambo mengi ambayo Yesu amemtendea, na watu wote walistaajabu.
© 2017 Bible League International