Book of Common Prayer
4 Kila atendaye dhambi huivunja sheria ya Mungu. Ndiyo, kutenda dhambi ni sawa na kuishi kinyume na sheria ya Mungu. 5 Mwajua ya kuwa Kristo alikuja kuziondoa dhambi za watu. Haimo dhambi ndani ya Kristo. 6 Hivyo kila anayeishi katika Kristo haendelei kutenda dhambi. Kama wakiendelea kutenda dhambi, kwa hakika hawajamwelewa Kristo na hawajamjua kamwe.
7 Watoto wapendwa, msimruhusu mtu yeyote kuwadanganya. Kristo daima alitenda yaliyo haki. Hivyo kuwa mwema kama Kristo, ni lazima utende yaliyo haki. 8 Mwovu amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kila anayeendelea kutenda dhambi ni mali ya Mwovu. Mwana wa Mungu alikuja kwa ajili ya hili: Kuziharibu kazi za Mwovu.
9 Wale ambao ni watoto wa Mungu hawaendelei kutenda dhambi, kwa sababu wanayo maisha mapya waliyopewa na Mungu.[a] Hawaendelei kutenda dhambi, kwa sababu wamefanyika watoto wa Mungu. 10 Hivyo tunaweza kuwatambua walio watoto wa Mungu na walio watoto wa Mwovu. Hawa ndiyo wasio watoto wa Mungu: Wale wanaotenda mambo yasiyo haki na wale wasiowapenda ndugu zao wa kike na wa kiume katika familia ya Mungu.
Yesu Mchungaji Mwema
7 Hivyo Yesu akasema tena, “Hakika ninawaambia, Mimi ni mlango wa kondoo. 8 Wote walionitangulia walikuwa wezi na wanyang'anyi. Kondoo hawakuwasikiliza hao. 9 Mimi ni mlango. Yeyote anayeingia kupitia kwangu ataokoka. Ataweza kuingia na kutoka nje. Atapata kila anachohitaji. 10 Mwizi anakuja kuiba, kuua, na kuangamiza. Lakini mimi nilikuja kuwaletea uzima, na muwe nao kwa ukamilifu.
11 Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huyatoa maisha yake kwa ajili ya kondoo. 12 Mtumishi anayelipwa ili kuwachunga kondoo yuko tofauti na mchungaji. Mtumishi wa mshahara, kondoo siyo mali yake. Hivyo anapomwona mbwa mwitu anakuja, hukimbia na kuwaacha kondoo peke yao. Mbwa mwitu huwashambulia na kuwatawanya kondoo. 13 Mtu huyu huwakimbia kondoo kwa sababu yeye ni mfanyakazi wa mshahara tu. Hawajali kabisa kondoo.
14-15 Mimi ni mchungaji ninayewajali kondoo. Nawafahamu kondoo wangu kama ambavyo Baba ananijua mimi. Na kondoo wananijua kama nami ninavyomjua Baba. Nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo hawa. 16 Nina kondoo wengine ambao hawamo kwenye kundi hili hapa. Hao nao napaswa kuwaongoza. Kwani wataisikia sauti yangu. Baadaye kutakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja.[a]
© 2017 Bible League International