Book of Common Prayer
9 Mmoja wa malaika saba akaja kwangu. Huyu alikuwa mmoja wa malaika saba waliokuwa na bakuli saba zilizojaa mapigo saba ya mwisho. Malaika akasema, “Njoo huku. Nitakuonesha bibi arusi, mke wa Mwanakondoo.” 10 Malaika akanichukua kwa Roho Mtakatifu mpaka kwenye mlima mkubwa na mrefu. Akanionyesha mji mtakatifu wa Yerusalemu. Mji ulikuwa ukiteremka kutoka mbinguni kwa Mungu.
11 Mji ulikuwa unang'aa kwa utukufu wa Mungu. Ulikuwa unang'aa kwa uangavu kama yaspi, kito cha thamani sana. Ulionekana kwa uwazi kama kioo. 12 Mji ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye malango kumi na mbili. Kulikuwa malaika kumi na mbili kwenye milango. Kwenye kila mlango kuliandikwa jina la kabila moja la Israeli. 13 Yalikuwepo malango matatu upande wa mashariki, malango matatu kaskazini, malango matatu kusini, na malango matatu magharibi. 14 Kuta za mji zilijengwa kwenye mawe kumi na mbili ya msingi. Kwenye mawe kulikuwa kumeandikwa majina ya mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo.
15 Malaika aliyezungumza na mimi alikuwa na fimbo ya kupimia iliyotengenezwa kwa dhahabu. Alikuwa na fimbo hii ili kuupima mji, malango na ukuta wake. 16 Mji ulijengwa kimraba. Urefu wake ulikuwa sawa na upana wake. Malaika aliupima mji kwa fimbo. Mji ulikuwa na urefu wa kilomita 2,400,[a] upana wake ulikuwa kilomita 2,400, na kimo chake kwenda juu kilikuwa kilomita 2,400. 17 Malaika akaupima ukuta pia. Kimo cha ukuta kilikuwa ni mita 60[b] kwenda juu. (Malaika alikuwa anatumia vipimo ambavyo watu hutumia.) 18 Ukuta ulijengwa kwa yaspi. Mji ulijengwa kwa dhahabu safi, iliyo safi kama kioo.
19 Mawe ya msingi wa ukuta wa mji yalikuwa na kila aina ya vito vya thamani ndani yake. Jiwe la kwanza la msingi lilikuwa yaspi, la pili lilikuwa yakuti samawi, la tatu lilikuwa kalkedoni, la nne lilikuwa zumaridi, 20 la tano lilikuwa sardoniki, la sita lilikuwa akiki, la saba lilikuwa krisolitho, la nane lilikuwa zabarajadi, la tisa lilikuwa yakuti ya manjano, la kumi lilikuwa krisopraso, la kumi na moja lilikuwa hiakintho na la kumi na mbili lilikuwa amethisto. 21 Malango kumi na mbili yalikuwa lulu kumi na mbili. Kila lango lilitengenezwa kwa lulu moja. Mitaa ya mji ilitengenezwa kwa dhahabu safi, inayong'aa kama kioo.
Malaika Atangaza Kuzaliwa kwa Yesu
26-27 Mwezi wa sita wa ujauzito wa Elizabeti, Mungu alimtuma malaika Gabrieli kwa msichana mmoja bikira aliyeishi Nazareti, mji wa Galilaya. Msichana huyo alikuwa amechumbiwa na Yusufu mzaliwa katika ukoo wa Daudi. Jina la bikira huyo lilikuwa Mariamu. 28 Malaika alimwendea na kusema “Salamu! Bwana yu pamoja nawe; Kwa kuwa neema yake iko juu yako.”
29 Lakini, Mariamu alichanganyikiwa kutokana na yale aliyosema malaika. Akajiuliza, “Salamu hii ina maana gani?”
30 Malaika akamwambia, “Usiogope Mariamu, kwa kuwa neema ya Mungu iko juu yako. 31 Sikiliza! Utapata mimba na kuzaa mtoto mwanamume, nawe utamwita jina lake Yesu. 32 Mtoto huyo atakuwa Mkuu na watu watamwita Mwana wa Mungu Aliye Mkuu Sana na Bwana Mungu atamfanya kuwa mfalme kama Daudi baba yake. 33 Naye ataitawala nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”
34 Mariamu akamwambia malaika, “Jambo hili litatokeaje? Kwa maana mimi bado ni bikira.”
35 Malaika akamwambia Mariamu, “Roho Mtakatifu atakujia, na nguvu zake Mungu Mkuu zitakufunika. Na hivyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu na ataitwa Mwana wa Mungu. 36 Pia sikiliza hili: Jamaa yako Elizabeti ni mjamzito. Ijapokuwa ni mzee sana, atazaa mtoto wa kiume. Kila mtu alidhani hataweza kuzaa, lakini sasa huu ni mwezi wa sita wa ujauzito wake. 37 Mungu anaweza kufanya jambo lolote!”
38 Mariamu akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, basi jambo hili litokee kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka.
© 2017 Bible League International