Book of Common Prayer
Watu Wengi Wataacha Kumpenda Mungu
3 Kumbuka hili: Katika siku za mwisho nyakati ngumu zitakuja. 2 Watu watajipenda wenyewe na kupenda fedha. Watakuwa na majivuno na wenye jeuri. Watawatukana wengine kwa matusi. Hawatawatii wazazi wao. Watakuwa wasio na shukrani. Watapinga kila kinachompendeza Mungu. 3 Hawatakuwa na upendo kwa wengine na hawatakubali kuwasamehe wengine. Watawasingizia wengine na hawataweza kujizuia. Watakuwa wakatili na watayachukia yaliyo mema. 4 Watu watawasaliti rafiki zao. Watafanya mambo ya kipuuzi bila kufikiri na watajisifu wenyewe. Badala ya kumpenda Mungu watapenda starehe. 5 Watajifanya kuwa wanamheshimu Mungu, lakini watazikana nguvu za uzima ambazo ndizo zinazotuwezesha kwa hakika kumpa utukufu na kumpendeza. Ukae mbali na watu wa jinsi hiyo.
6 Nasema hivi kwa sababu baadhi yao wanaziendea nyumba na kuwateka wanawake dhaifu, waliolemewa na dhambi na kuvutwa na kila aina ya tamaa. 7 Wanawake hawa nyakati zote wanataka kujifunza, lakini hawawezi kamwe kuufikia ufahamu wote wa kweli. 8 Kama ambavyo Yane na Yambre[a] walivyompinga Musa, ndivyo hata watu hawa wanavyoipinga kweli. Ni watu ambao akili zao zimeharibika, nao wameshindwa kuifuata imani. 9 Lakini hawataendelea mbele zaidi, kwa sababu upumbavu wao utadhihirika wazi wazi kwa watu wote, kama ujinga wa Yane na Yambre ulivyojulikana.
Maelekezo ya Mwisho
10 Ninyi hata hivyo mmeyazingatia na kuyashika mafundisho yangu, mwenendo wangu na kusudi langu katika maisha, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu na ustahimilivu wangu, 11 mateso yangu na taabu zangu. Mnayajua mambo yaliyonitokea kule Antiokia, Ikonia, na Listra, mateso ya kutisha niliyoyastahimili! Lakini Bwana akaniokoa kutoka katika hayo yote. 12 Kwa hakika wote wanaoishi maisha yenye kumtukuza Mungu kama wafuasi wa Kristo Yesu watasumbuliwa. 13 Lakini watu waovu na wanaodanganya wengine wataendelea kuwa wabaya zaidi. Watawadaganya wengine na wao pia watajidanganya wenyewe.
14 Lakini imekupasa wewe kuendelea kuyashika mambo yale uliyojifunza na kuyathibitisha moyoni mwako kuwa ni ya kweli. Wewe unawajua na unawaamini wale waliokufundisha. 15 Na unajua kwamba umeyajua Maandiko Matakatifu tangu ukiwa mtoto. Maandiko hayo yana uwezo wa kukupa hekima. Hekima hiyo itakuongoza hadi kwenye wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. 16 Maandiko yote tumepewa na Mungu. Na maandiko yote yanafaa kwa mafundisho kwa kusudi la kuwaonesha watu makosa yao na kuwafundisha njia sahihi ya kuishi 17 ili mtu anayemtumikia Mungu aweze kuandaliwa na kukamilishwa kwa ajili ya kufanya kila kazi njema.
Yesu Aiosha Miguu ya Wafuasi wake
13 Sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi ilikaribia. Yesu alijua kwamba wakati wake wa kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ulikuwa umefika. Daima Yesu aliwapenda watu wa ulimwengu huu waliokuwa wake. Huu ulikuwa wakati alipowaonesha upendo wake mkuu.
2 Yesu na wafuasi wake walikuwa wakila chakula cha jioni. Ibilisi alikuwa tayari amekwisha kumshawishi Yuda Iskariote kumsaliti Yesu kwa maadui zake. (Yuda alikuwa Mwana wa Simoni.) 3 Baba alikuwa amempa Yesu uwezo juu ya kila kitu. Naye Yesu alilifahamu hili. Alijua pia kuwa yeye alitoka kwa Mungu. Tena alijua kuwa alikuwa anarudi kwa Mungu. 4 Kwa hiyo walipokuwa wakila,[a] Yesu alisimama na kulivua vazi lake. Akachukua taulo na kuifunga kiunoni mwake. 5 Kisha akamimina maji katika bakuli na kuanza kuwaosha miguu[b] wafuasi wake. Kisha akaifuta miguu yao kwa taulo aliolifunga kiunoni mwake.
6 Akamfikia Simoni Petro, naye Simoni Petro akamwambia, “Bwana, huwezi kuiosha miguu yangu.”
7 Yesu akamjibu, “Huyaelewi ninayofanya hivi sasa. Lakini utayaelewa baadaye.”
8 Petro akasema, “Hapana! Huwezi kamwe kuniosha miguu yangu kamwe.”
Yesu akamjibu, “Kama sitakuosha miguu yako, basi hutakuwa miongoni mwa watu wangu.”
9 Simoni Petro akasema, “Bwana, utakapomaliza miguu, unioshe mikono na kichwa pia!”
10 Yesu akamwambia, “Baada ya mtu kuoga, mwili wake wote huwa safi. Anahitaji tu kunawa miguu. Nanyi mko safi, lakini sio nyote.” 11 Yesu alimjua yule atakayemsaliti mbele ya adui zake. Ndiyo maana alisema, “Sio wote mlio safi.”
12 Yesu alipomaliza kuwaosha miguu wafuasi, alivaa nguo zake na kurudi pale mezani. Akawauliza, “Je, mmelielewa nililowafanyia? 13 Mnaniita mimi ‘Mwalimu’. Tena mnaniita mimi ‘Bwana’. Hayo ni sahihi, kwa sababu hivyo ndivyo nilivyo. 14 Mimi ni Bwana na Mwalimu wenu. Lakini niliwaosha miguu yenu kama mtumishi. Hivyo nanyi mnapaswa kuoshana miguu yenu. 15 Nilifanya hivyo kama mfano. Hivyo nanyi mnapaswa kuhudumiana ninyi kwa ninyi kama nilivyowahudumia. 16 Mniamini mimi, watumishi huwa sio wakubwa kuzidi bwana zao. Wale waliotumwa kufanya jambo fulani sio wakubwa kumzidi yule aliyewatuma. 17 Sasa, mkielewa maana ya yale niliyotenda, Mungu atawabariki mkiyatendea kazi.
18 Nami sizungumzii habari zenu nyote. Nawafahamu watu wale niliowachagua. Lakini Maandiko yanapaswa kutimia kama yanavyosema: ‘Mtu aliyekula chakula pamoja nami amenigeuka.’[c] 19 Ninawaambia hili sasa kabla halijatokea. Hivyo litakapotokea, mtaweza kuamini kuwa MIMI NDIYE.[d] 20 Hakika nawaambieni, yeyote anayempokea mtu yule niliyemtuma ananipokea mimi pia. Na yeyote anayenipokea mimi humpokea pia yeye aliyenituma.”
© 2017 Bible League International