Yuda
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
1 Salamu kutoka kwa Yuda, mtumwa wa Yesu Kristo na ndugu yake Yakobo. Kwa wale waliochaguliwa na kupendwa na Mungu Baba na kulindwa ndani ya Yesu Kristo.
2 Rehema, amani na upendo viwe pamoja nanyi zaidi na zaidi.
Mungu Atawaadhibu Watendao Mabaya
3 Rafiki wapendwa, nilitaka sana kuwaandikia kuhusu wokovu tunaoshiriki pamoja. Lakini nimejisikia kuwa ni muhimu niwaandikie kuhusu kitu kingine: Ninataka kuwatia moyo kuipigania kwa nguvu imani ambayo Mungu aliwapa watakatifu wake. Mungu alitoa imani hii mara moja na ni nzuri wakati wote. 4 Baadhi ya watu wamejiingiza kwa siri kwenye kundi lenu. Watu hawa wamekwisha kuhukumiwa kuwa wakosaji kwa sababu ya matendo yao. Zamani zilizopita manabii waliandika kuhusu watu hao. Wako kinyume na Mungu. Wameigeuza neema ya Mungu kujihalalishia kutenda chochote wanachotaka. Wanakataa kumtii Mkuu aliye peke yake, Bwana wetu Yesu Kristo.
5 Ninataka kuwasaidia mkumbuke baadhi ya vitu mnavyovifahamu tayari: Kumbukeni kwamba Bwana[a] aliwaokoa watu wake kwa kuwatoa katika nchi ya Misri. Lakini baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini. 6 Na kumbukeni malaika waliopoteza mamlaka yao ya kutawala. Waliacha mahali pao pa kuishi. Hivyo Bwana amewaweka gizani, wamefungwa kwa minyororo ya milele, mpaka watakapohukumiwa siku iliyo kuu. 7 Pia kumbukeni miji ya Sodoma na Gomora na miji mingine iliyoizunguka. Kama wale malaika, watu wa miji ile walikuwa na hatia ya dhambi ya uzinzi, hata wakataka kuzini na malaika. Na waliadhibiwa kwa moto wa milele. Miji hii ni mfano kwa waovu watakaoteseka kwa adhabu ya moto wa milele.
8 Ni sawasawa na watu hawa waliojiingiza kwenye kundi lenu. Wanaongozwa na ndoto, wanajichafua wenyewe kwa dhambi. Wanapuuza mamlaka ya Bwana na kusema mambo mabaya kinyume na walio watukufu.[b] 9 Hata malaika mkuu Mikaeli hakufanya hivi. Mikaeli alibishana na Ibilisi kuhusu nani angeuchukua mwili wa Musa. Lakini Mikaeli hakutamka hukumu kwa Ibilisi kwa mashitaka yake ya uongo. Badala yake, Mikaeli alisema, “Bwana mwenyewe akuadhibu!”
10 Lakini watu hawa hukashifu mambo wasiyoyaelewa. Wanaelewa baadhi ya mambo, isipokuwa wanayaelewa mambo haya si kwa kufikiri bali kwa kuhisi, kama wanyama wasiofikiri. Na haya ni mambo yanayowaangamiza. 11 Itakuwa vibaya kwao kwa kuwa wameifuata njia ambayo Kaini[c] aliitumia. Kwa kutafuta fedha, wamejiingiza katika kosa lile lile la Balaamu.[d] Wamepigana kinyume na Mungu kama alivyofanya Kora.[e] Na wataangamizwa vile vile kama Kora.
12 Watu hawa ni kama madoa machafu miongoni mwenu, wanawatia aibu mnapokutanika pamoja kuonesha upendo miongoni mwenu na kula chakula kwa pamoja kama kanisa. Pasipo kuwa na aibu wanakula pamoja nanyi. Wanajijali wao wenyewe tu. Wao ni kama mawingu yasiyo na mvua yanayosukumwa na upepo kila upande. Wako kama miti isiyo na matunda wakati wa mavuno ambayo hung'olewa kutoka ardhini. Hivyo wamekufa mara mbili. 13 Kama mapovu machafu juu ya mawimbi ya bahari, kila mtu anaweza kuona mambo ya aibu wanayoyafanya. Ni kama nyota zinazotangatanga angani. Nao wameandaliwa mahali penye giza kuu milele.
14 Henoko, mtu wa kizazi cha saba kutoka Adamu, alisema hivi kuhusu watu hawa: “Tazama! Bwana anakuja pamoja na maelfu ya malaika watakatifu. 15 Kumhukumu kila mmoja. Atawaadhibu wale wote walio kinyume naye kutokana na maovu waliyotenda kwa sababu ya kutokumheshimu. Ndiyo, Bwana atawaadhibu watenda dhambi wote hawa wasiomheshimu. Atawaadhibu kwa sababu ya mambo maovu waliyosema kinyume naye.”
16 Watu hawa daima hulalamika na kutafuta ubaya kwa wengine. Daima hutenda mambo maovu wanayotaka kufanya. Hujisifu wenyewe. Huwatendea vyema baadhi ya watu kuliko wengine ili wapate vitu wanavyovitaka.
Tahadhari na Mambo ya Kufanya
17 Rafiki wapendwa, kumbukeni mambo ambayo mitume wa Bwana Yesu Kristo walisema kuwa yatatokea. 18 Walisema, “Katika nyakati za mwisho kutakuwa watu wanaomcheka Mungu na kufanya yale wanayotaka kufanya tu, mambo ambayo ni kinyume na Mungu.” 19 Hawa ni watu wanaowagawa katika makundi. Si wa rohoni kwa sababu hawana Roho Mtakatifu.
20 Lakini ninyi, rafiki wapendwa, itumieni imani yenu takatifu zaidi kusaidiana ninyi kwa ninyi ili muwe imara zaidi katika imani. Ombeni kwa msaada wa Roho Mtakatifu. 21 Jiwekeni salama katika upendo wa Mungu, kadri mnavyomsubiri Bwana Yesu Kristo kuionesha rehema yake kwenu kwa kuwapa uzima wa milele.
22 Waonesheni rehema walio na mashaka. 23 Waokoeni wale wanaoishi katika hatari ya moto wa jehanamu. Muwatendee wengine kwa rehema, lakini muwe waangalifu kuwa maisha yao maovu yasichafue mwenendo wenu mwema.[f]
Msifuni Mungu
24 Mungu ana nguvu na anaweza kuwafanya msianguke. Anaweza kuwaingiza katika uwepo wa utukufu wake bila makosa yoyote ndani yenu na akawapa furaha kuu. 25 Ni Mungu peke yake, aliye Mwokozi wetu. Kwake uwepo utukufu, ukuu, nguvu na mamlaka kupitia Yesu Kristo kwa wakati uliopita, uliopo na milele. Amina.
Footnotes
- 1:5 Bwana Baadhi ya matoleo ya kale ya Kiyunani ya waraka huu wa Yuda yameandika “Yesu”. Baadhi ya matoleo ya hivi karibuni yana “Mungu”.
- 1:8 watukufu Hapa inamaanisha viumbe wa mbinguni, malaika.
- 1:11 Kaini Tazama Mwa 4:1-16.
- 1:11 Balaamu Tazama Hes 25:1-4; 31:16.
- 1:11 Kora Tazama Hes 16:1-40.
- 1:23 maisha yao … mwema Kwa maana ya kawaida, “kuchukia hata nguo ya ndani inayochafuliwa na mwili”.

Ufunuo 1-2

Yohana Aeleza Kuhusu Kitabu Hiki
1 Huu ni ufunuo[a] kutoka kwa Yesu Kristo, ambao Mungu alimpa ili awaoneshe watumishi wake yale ambayo ni lazima yatokee muda mfupi ujao. Yesu Kristo alimtuma malaika wake ili amwonyeshe Yohana, mtumishi wake, 2 ambaye amesema kila kitu alichokiona. Ni ukweli alioambiwa na Yesu Kristo; ni ujumbe kutoka kwa Mungu. 3 Ana heri anayesoma maneno ya ujumbe huu kutoka kwa Mungu kwa kupaza sauti na wale wanaousikia ujumbe huu na kuyatendea kazi yaliyoandikwa ndani yake. Wakati uliosalia ni mfupi.
Yohana Ayaandikia Makanisa
4 Kutoka kwa Yohana,
Kwenda kwa makanisa saba yaliyo katika Asia:
Neema na amani ziwe kwenu kutoka kwake aliyepo, aliyekuwepo daima na anayekuja; na kutoka katika roho saba zilizoko mbele ya kiti chake cha enzi; 5 na kutoka kwa Yesu Kristo aliye shahidi mwaminifu. Aliye wa kwanza miongoni mwa watakaofufuliwa kutoka kwa wafu na ndiye mtawala wa wafalme wote wa dunia.
Yesu ndiye anayetupenda na ametuweka huru na dhambi zetu kwa sadaka ya damu yake. 6 Ametufanya sisi kuwa ufalme wake na makuhani wanaomtumikia Mungu, Baba yake. Utukufu na nguvu viwe kwa Yesu milele na milele! Amina.
7 Tazama, Yesu anakuja pamoja na mawingu! Kila mtu atamwona, hata wale waliomchoma.[b] Watu wote wa dunia watamwombolezea.[c] Ndiyo, hili litatokea! Amina.
8 Bwana Mungu asema, “Mimi ni Alfa na Omega.[d] Mimi ndiye niliyepo, aliyekuwepo na anayekuja. Mimi ni Mwenye Uwezo Wote.” 9 Mimi ni Yohana, mwamini mwenzenu. Tuko pamoja katika Yesu na tunashirikiana mambo haya: mateso, ufalme na uvumilivu wenye subira. Nilikuwa katika kisiwa cha Patmo[e] kwa sababu nimekuwa mwaminifu kwa ujumbe wa Mungu na kwa ajili ya kweli ya Yesu. 10 Siku ya Bwana, Roho Mtakatifu alinitawala. Nilisikia sauti kuu nyuma yangu iliyosikika kama tarumbeta. 11 Ilisema, “Yaandike kwenye kitabu yale unayoyaona na uyatume kwa makanisa saba ya Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.”
12 Niligeuka nyuma nimwone aliyekuwa anazungumza nami. Nilipogeuka, niliona vinara saba vya taa vya dhahabu. 13 Nikamwona mmoja katikati ya vinara aliyeonekana kama Mwana wa Mtu. Alikuwa amevaa vazi refu, na mshipi wa dhahabu uliofungwa kuzunguka kifua chake. 14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe kama theluji. Macho yake yalikuwa kama miali ya moto. 15 Miguu yake ilikuwa kama shaba ing'aayo inapochomwa katika tanuru. Sauti yake ilikuwa kama kelele za mafuriko ya maji. 16 Alikuwa ameshikilia nyota saba katika mkono wake wa kulia. Upanga wenye makali kuwili ulitoka kinywani mwake. Uso wake ulikuwa jua linalong'aa sana mchana.
17 Nilipomwona nilianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Aliweka mkono wake wa kulia juu yangu na kusema, “Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa Mwisho. 18 Mimi ndiye ninayeishi. Nilikufa, lakini tazama, niko hai milele na milele! Na ninashikilia funguo za mauti na Kuzimu. 19 Hivyo andika unachokiona. Yaandike mambo yanayotokea sasa na mambo yatakayotokea baadaye. 20 Hii ni maana iliyofichwa ya nyota na vinara saba vya taa vya dhahabu ulivyoviona: Vinara saba ni makanisa saba. Nyota saba ni malaika wa makanisa saba.”
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Efeso
2 “Andika hivi kwa malaika[f] wa kanisa lililoko Efeso:
Huu ni ujumbe kutoka kwake yeye anayeshikilia nyota saba katika mkono wake wa kulia na kutembea katikati ya vinara vya taa saba vya dhahabu.
2 Ninayajua matendo yako, unavyofanya kazi kwa bidii na usivyokata tamaa. Ninajua kwamba huwakubali watu waovu. Umewajaribu wote wanaojiita mitume lakini si mitume. Umegundua kuwa ni waongo. 3 Huachi kujaribu. Umestahimili taabu kwa ajili ya jina langu na hujakata tamaa.
4 Lakini nina neno hili nawe umeuacha upendo uliokuwa nao hapo mwanzo. 5 Hivyo kumbuka ulipokuwa kabla ya kuanguka. Ugeuze moyo wako na utende yale uliyoyatenda mwanzoni. Usipobadilika, nitakuja kwako na kutoa kinara chako cha taa mahali pake. 6 Lakini unafanya vizuri kuyachukia matendo ya Wanikolai.[g] Mimi pia nayachukia mambo wanayotenda.
7 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Wale watakaoshinda, nitawapa haki ya kula matunda kutoka kwenye mti wa uzima, ulio katika Bustani ya Mungu.
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Smirna
8 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna:
“Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa na akawa hai tena.
9 Ninayajua matatizo yako, na ninajua kwamba wewe ni maskini, lakini hakika wewe ni tajiri! Ninayajua matusi unayoteseka kutoka kwa watu wanaojiita Wateule wa Mungu.[h] Lakini si Wayahudi halisi. Watu hao ni wa kundi[i] la Shetani. 10 Usiogope mambo yatakayokupata hivi karibuni. Ninakwambia, Ibilisi atawafunga gerezani baadhi yenu ili kuipima imani yenu. Mtateseka kwa siku kumi, lakini iweni waaminifu, hata ikiwa mtatakiwa kufa. Mkiendelea kuwa waaminifu, nitawapa thawabu[j] ya uzima wa milele.
11 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Wale watakaoshinda hawatadhuriwa na mauti ya pili.
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Pergamo
12 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo:
Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye na upanga wenye makali kuwili unaotoka katika kinywa chake.
13 Ninapafahamu mahali unapoishi. Unaishi mahali kilipo kiti cha enzi cha Shetani, lakini wewe ni mwaminifu kwangu. Hukukataa kueleza kuhusu imani yako kwangu hata wakati wa Antipa. Antipa alikuwa shahidi wangu mwaminifu[k] aliyeuawa katika mji wako, mji ambao shetani anaishi.
14 Lakini nina vitu vichache kinyume nawe. Una watu huko wanaofuata mafundisho ya Balaamu. Balaamu alimfundisha Balaki namna ya kuwafanya watu wa Israeli kutenda dhambi. Walitenda dhambi kwa kula vyakula vilivyotolewa kwa ajili ya sanamu na kwa kufanya uzinzi. 15 Ndivyo ilivyo hata kwa kundi lako. Una watu wanaofuata mafundisho ya Wanikolai. 16 Hivyo igeuzeni mioyo yenu! Msipobadilika, nitakuja kwenu haraka na kupigana kinyume na watu hawa kwa kutumia upanga unaotoka katika kinywa changu.
17 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa!
Kila atakayeshinda nitampa mana iliyofichwa. Pia nitampa kila mshindi jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya juu yake. Na hakuna atakayejua jina hili isipokuwa yule atakayepata jiwe hili.
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Thiatira
18 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira:
Huu ni ujumbe kutoka kwa Mwana wa Mungu, aliye na macho yanayong'aa kama moto na miguu kama shaba inayong'aa.
19 Ninayajua matendo yako. Ninajua kuhusu upendo wako, imani yako, huduma yako na uvumilivu wako. Ninajua kwamba unafanya zaidi sasa kuliko ulivyofanya kwanza. 20 Lakini ninalo hili kinyume nawe: Umemruhusu yule mwanamke Yezebeli afanye anachotaka. Anasema kwamba yeye ni nabii,[l] lakini anawapotosha watu wangu kwa mafundisho yake. Yezebeli huwaongoza watu wangu kutenda dhambi ya uzinzi na kula vyakula vilivyotolewa kwa sanamu. 21 Nimempa muda ili aubadili moyo wake na kuiacha dhambi yake, lakini hataki kubadilika.
22 Hivyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso. Na wale wote wanaozini naye watateseka sana. Nitafanya hivi sasa ikiwa hawataacha mambo anayofanya. 23 Pia, nitawaua wafuasi wake. Ndipo makanisa yote wataona kuwa mimi ndiye ninayefahamu kile ambacho watu wanadhani na kufikiri. Na nitamlipa kila mmoja wenu kutokana na kile alichotenda.
24 Lakini ninyi wengine mlioko Thiatira ambao hamjafuata mafundisho yake. Hamjajifunza mambo yanayoitwa ‘Siri za ndani za Shetani.’ Hivi ndivyo ninawaambia: Sitawatwika mzigo wowote. 25 Shikeni katika kweli mliyo nayo tu mpaka nitakapo kuja.
26 Nitawapa nguvu juu ya mataifa wale wote watakaoshinda na wakaendelea kutenda yale ninayotaka mpaka mwisho. 27 Watayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma. Watayavunja vipande vipande kama vyombo vya udongo wa mfinyanzi.[m] 28 Watakuwa na nguvu ile ile niliyoipokea kutoka kwa Baba yangu, na nitawapa nyota ya asubuhi. 29 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.
Footnotes
- 1:1 ufunuo Utangulizi (kujulisha) wa ukweli uliofichwa.
- 1:7 waliomchoma Yesu alipouawa, alichomwa mkuki ubavuni. Tazama Yh 19:34.
- 1:7 watamwombolezea Ama, “watajipiga vifuani mwao”. Usemi huu unatumika kuonesha huzuni na majonzi kwa yaliyomtokea pia hii ni ishara ya kuomboleza. Neno la Kiyunani lina maana ya kitendo zaidi ya kilio kwa sauti.
- 1:8 Alfa na Omega Herufi ya kwanza na ya mwishi katika mfumo wa herufi wa Kiyunani, hapa inamaanisha “wa Kwanza na wa Mwisho”.
- 1:9 Patmo Kisiwa kidogo katika bahari ya Aegeani. Kisiwa hiki kiko karibu na pwani ya nchi ya Uturuki kama inavyojulikana siku za leo.
- 2:1 malaika Ama mwakilishi wa kanisa. Pia katika mstari wa 8,12 na 18 na pia katika barua zinazofuata Sura 3:1,7 na 14.
- 2:6 Wanikolai Kikundi cha kidini kilichofuata mafundisho ya uongo. Pia katika mstari wa 15.
- 2:9 Wateule wa Mungu Kwa maana ya kawaida, “Wayahudi”. Pia katika 3:9.
- 2:9 kundi Kwa maana ya kawaida, “sinagogi”. Pia katika 3:9.
- 2:10 thawabu Kwa maana ya kawaida, “taji”, ni shada la majani au matawi ya miti lililowekwa juu ya vichwa vya washindi wa riadha ili kuwaheshimu. Ni alama inayoonyesha ushindi na zawadi.
- 2:13 shahidi wangu mwaminifu Mtu anayehubiri ujumbe wa Mungu kwa uaminifu, hata nyakati za hatari.
- 2:20 nabii Yezebeli alikuwa nabii mwongo. Alidai kuwa anazungumza kwa niaba ya Mungu, lakini hakuisema kweli ya Mungu.
- 2:26-27 Mistari hii inafanana na Zab 2:8-9 (tafsiri ya Kiyunani).

© 2017 Bible League International