Yohana 14-17
Neno: Bibilia Takatifu
Yesu Ndiye Njia Ya Kufika Kwa Mungu
14 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia. 2 Katika nyumba ya baba yangu mna nafasi nyingi. Kama sivyo, nisingeliwaambia kwamba nakwenda kuwaandalia makao. 3 Na nikishawaandalia, nitarudi kuwachukua mkae pamoja nami; ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo. 4 Ninyi mnajua njia ya kufikia ninakokwenda.” 5 Tomaso akamwuliza, “Bwana, hatujui unakokwenda; tutaijuaje njia?” 6 Yesu akawaam bia, “Mimi ndiye Njia na Kweli na Uzima; mtu hawezi kufika kwa Baba bila kupitia kwangu. 7 Kama mngekuwa mnajua mimi ni nani, mngemfahamu na Baba yangu. Tangu sasa mnamfahamu Baba yangu na mmemwona.”
8 Filipo akamwambia Yesu, “Bwana, tuonyeshe Baba yako nasi tutaridhika.” 9 Yesu akamjibu, “Filipo, imekuwaje hunifahamu baada ya mimi kuwa pamoja nanyi muda wote huu? Mtu ye yote ambaye ameniona mimi, amemwona Baba. Sasa inakuwaje unasema, ‘Tuonyeshe Baba’? 10 Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba yangu, na Baba yangu yuko ndani yangu? Mambo ninayowaambia siyasemi kwa mamlaka yangu mwenyewe, bali yanatoka kwa Baba yangu ambaye anaishi ndani yangu, na ndiye anayetenda haya yote. 11 Niaminini ninapowaambia ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu na Baba yangu yu ndani yangu. La sivyo, niaminini kwa sababu ya haya mambo ninayotenda. 12 Ninawaambia hakika, mtu ye yote akiniamini ataweza kufanya miujiza kama hii na hata zaidi, kwa kuwa mimi ninakwenda kwa Baba yangu. 13 Kitu cho chote mtakachoomba kwa jina langu, nitawafanyia, ili Baba yangu apate kutukuzwa kwa yale ambayo mimi Mwanae nitawafanyia. 14 Mkiniomba cho chote kwa jina langu nitawafanyia.”
Ahadi Ya Kupewa Roho Mtakatifu
15 “Kama mnanipenda mtatimiza amri zangu. 16 Nami nitam womba Baba, naye atawapeni Msaidizi mwingine akae nanyi siku zote. 17 Huyo ndiye Roho wa Kweli ambaye watu wasioamini hawawezi kumpokea. Watu kama hao hawamwoni wala hawamfahamu. Ninyi mnamfahamu kwa kuwa anakaa ndani yenu na ataendelea kuwa nanyi. 18 Sitawaacha kama yatima. Nitarudi kwenu. 19 Baada ya muda mfupi watu wa ulimwengu hawataniona tena, ila ninyi mta niona; na kwa kuwa mimi ni hai, ninyi pia mtakuwa hai. 20 Wakati huo utakapofika mtajua ya kuwa mimi niko ndani ya Baba yangu na ninyi mko ndani yangu. 21 Mtu anayezishika amri zangu na kuziti miza ndiye anayenipenda. Na mtu anayenipenda, Baba yangu atam penda; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.” 22 Yuda, siyo Iskariote, akamwuliza, “Bwana, itakuwaje ujidhihirishe kwetu tu na si kwa ulimwengu mzima?” 23 Yesu akamjibu, “Mtu akinipenda atashika mafundisho yangu na Baba yangu atampenda, nasi tutafanya makao yetu kwake. 24 Mtu asiyenipenda hayashiki mafundisho yangu na mafundisho niliyowapeni si yangu bali yametoka kwa Baba yangu aliyenituma.
25 “Nimewaambia mambo haya wakati nikiwa bado nipo nanyi. 26 Lakini yule Msaidizi, yaani Roho Mtakatifu, ambaye Baba yangu atamtuma kwenu kwa jina langu, atawafundisha mambo yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27 Ninawaachia amani. Nawapeni amani yangu; amani hii ulimwengu hauwezi kuwapa. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope. 28 Kumbukeni nilivyowaambia, ‘Ninakwenda, na nitarudi.’ Kama kweli mngalinipenda mngefurahi, kwa kuwa nakwenda kwa Baba; na Baba yangu ni mkuu kuliko mimi. 29 Na sasa nimewaambia mambo haya kabla hayajatokea ili yataka potokea mpate kuamini. 30 Sitasema tena mengi nanyi kwa sababu mtawala wa dunia hii anakuja. Yeye hana uwezo juu yangu. 31 Lakini ninatii amri ya Baba ili ulimwengu upate kujua kwamba nampenda Baba. Simameni tuondoke hapa.’ ’
Mzabibu Wa Kweli
15 ‘Mimi ni mzabibu wa kweli na Baba yangu ndiye mkulima. 2 Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata; na kila tawi lizaalo, yeye hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi. 3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya mafundisho nili yowapa. 4 Kaeni ndani yangu nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda pasipo kuwa sehemu ya mzabibu, vivyo hivyo, ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kufanya lo lote. 5 Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; anayekaa ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa matunda mengi sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya lo lote. 6 Mtu asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea. 7 Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lo lote mtakalo nanyi mtatendewa. 8 Mnapozaa matunda kwa wingi Baba yangu anatukuzwa, na hivyo mnadhihirisha kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.
9 “Kama Baba alivyonipenda mimi, hivyo ndivyo mimi nilivy owapenda ninyi; dumuni katika pendo langu. 10 Mkizishika amri zangu mtakaa ndani ya pendo langu kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.
11 “Nimewaambia haya kusudi furaha yangu iwe ndani yenu, nanyi mpate kuwa na furaha iliyokamilika.
12 “Amri yangu ni hii: pendaneni kama nilivyowapenda. 13 Hakuna mtu mwenye upendo unaozidi ule wa mtu anayejitoa afe kwa ajili ya rafiki zake. 14 Ninyi ni rafiki zangu ikiwa mtafa nya ninayowaagiza. 15 Siwaiti ninyi watumishi tena kwa sababu mtumishi haelewi shughuli za bwana wake; bali nimewaita rafiki, kwa maana mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu nimewa fahamisha. 16 Hamkunichagua, bali mimi nimewachagua ninyi na nimewatuma mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kudumu, ili lo lote mtakalomwomba Baba katika jina langu, awatimizie. 17 Hii ndio amri yangu: pendaneni.
18 “Kama ulimwengu ukiwachukia, fahamuni kwamba ulinichukia mimi kabla haujawachukia ninyi. 19 Kama mngekuwa watu wa ulim wengu huu, ulimwengu ungeliwapenda. Ulimwengu unawachukia kwa sababu ninyi si wa ulimwengu huu na mimi nimewachagua kutoka katika ulimwengu.
20 “Kumbukeni lile neno nililowaambia, ‘Hakuna mtumishi aliye mkuu kuliko bwana wake.’ Kama wamenitesa mimi na ninyi pia watawatesa; kama wamelishika neno langu na neno lenu watalishika pia. 21 Lakini yote haya watawatendea kwa ajili yangu kwa sababu hawamfahamu Baba yangu ambaye amenituma. 22 Kama sikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia. Lakini sasa hawana udhuru kwa dhambi zao. 23 Mtu ye yote anayenichukia mimi anamchukia na Baba yangu. 24 Kama nilikuwa sikuwafanyia miujiza ambayo haijapata kufanywa na mtu mwingine ye yote, wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini wameona miujiza hii na bado wakatuchukia mimi na Baba yangu. 25 “Hali hii imetokea kama ilivyoandikwa katika Sheria kwamba, ‘Walinichukia pasipo sababu.’ 26 Lakini atakapokuja yule Msaidizi nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, yaani yule Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi. 27 Na ninyi pia ni mashahidi wangu kwa maana tangu mwanzo mmekuwa pamoja nami.”
16 “Nimewaambia mambo haya yote ili msije mkapoteza imani yenu. 2 Watawatenga na kuwatoa katika ushirika wa masinagogi. Na si hivyo tu, bali utafika wakati ambapo mtu ye yote atakayewaua atadhani kuwa anamtumikia Mungu. 3 Watu watawatendea haya kwa sababu hawamfahamu Baba wala hawanifahamu mimi. 4 Lakini nimew aambia mambo haya kusudi muda huo utakapofika mkumbuke kuwa nili kuwa nimewaambia. Sikuwaambia mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi.
Kazi Ya Roho Mtakatifu
5 “Lakini sasa ninakwenda kwake yeye aliyenituma, wala hakuna mmoja wenu anayeniuliza, ‘Unakwenda wapi?’ 6 Kwa kuwa nimewaambia mambo haya, mioyo yenu imejawa na huzuni. 7 Lakini nawaambia kweli kwamba kuondoka kwangu ni kwa faida yenu kwa maana nisipoondoka, yule Msaidizi hatakuja kwenu. Lakini nikienda nitamtuma aje kwenu. 8 Naye akija atauthibitishia ulim wengu kuhusu dhambi, haki na hukumu. 9 Kuhusu dhambi kwa sababu hawaniamini; 10 kuhusu haki kwa sababu ninakwenda kwa Baba na hamtaniona tena; 11 na kuhusu hukumu kwa sababu mtawala wa ulim wengu huu amekwisha kuhukumiwa.
12 “Nina mambo mengi zaidi ya kuwaambia lakini hamwezi kuy apokea sasa. 13 Akija yule Roho wa kweli atawaongoza muijue kweli yote. Yeye hatanena kwa uwezo wake mwenyewe bali atanena yote atakayosikia. Atawafundisha kuhusu mambo yote yajayo. 14 Atanitukuza mimi, kwa maana atayachukua yaliyo yangu na kuwaambia ninyi. 15 Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu, ndio maana nimesema kuwa atachukua yaliyo yangu na kuwaambia ninyi.
Huzuni Na Furaha
16 “Baada ya muda mfupi hamtaniona tena; na kisha muda mfupi baadaye mtaniona.” 17 Baadhi ya wanafunzi wakaulizana, “Ana maana gani asemapo, ‘Baada ya muda mfupi hamtaniona tena na muda mfupi baadaye mtaniona’? Na ana maana gani asemapo, ‘Kwa sababu ninakwenda kwa baba’?” 18 Wakaendelea kuulizana, “Ana maana gani asemapo, ‘muda mfupi?’ Hatuelewi ana maana gani!”
19 Yesu alitambua walilotaka kumwuliza kwa hiyo akawaambia, “Mnaulizana nina maana gani nisemapo, ‘Baada ya muda mfupi ham taniona tena na baada ya muda mfupi mtaniona?’ 20 Ninawaambia yaliyo hakika kwamba mtalia na kuomboleza lakini ulimwengu utafu rahi. Mtahuzunika lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. 21 Mwanamke akaribiapo kuzaa huwa na huzuni kwa sababu saa yake ya uchungu imefika. Lakini mtoto azaliwapo mama anasahau mateso hayo kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtoto duniani. 22 Na ninyi sasa mna huzuni lakini nitawaona tena na mtafurahi, wala hakuna atakayewaondolea furaha yenu. 23 Wakati huo hamtaniomba kitu cho chote. Ninawaambia kweli kwamba Baba yangu atawapa lo lote mta kaloomba kwa jina langu. 24 Mpaka sasa hamjaomba lo lote kwa jina langu. Ombeni nanyi mtapewa ili furaha yenu ipate kukamil ika.
Ushindi
25 “Nimewaambia mambo haya kwa mafumbo. Lakini wakati unakuja ambapo sitazungumza nanyi tena kwa mafumbo bali nita waeleza wazi wazi kuhusu Baba yangu. 26 Wakati huo mtaomba kwa jina langu. Wala sisemi kwamba nitamwomba Baba kwa niaba yenu; 27 kwa maana Baba mwenyewe anawapenda kwa sababu mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Baba. 28 Nilitoka kwa Baba na nimekuja ulimwenguni, tena sasa naondoka ulimwenguni na ninak wenda kwa Baba.” 29 Wanafunzi wake wakasema, “Sasa unazungumza wazi wazi wala si kwa mafumbo. 30 Sasa tumejua kwamba wewe una jua mambo yote wala hakuna haja ya mtu kukuuliza maswali. Kwa hiyo tunaamini kwamba ulitoka kwa Mungu.” 31 Yesu akawajibu, “Sasa mnaamini? 32 Saa inakuja, tena imeshawadia, ambapo mtata wanyika, kila mtu aende nyumbani kwake na kuniacha peke yangu; lakini mimi siko peke yangu kwa sababu Baba yuko pamoja nami. 33 Nimewaambia mambo haya ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”
Yesu Anawaombea Wanafunzi Wake
17 Yesu alipomaliza kusema maneno haya, alitazama mbinguni akasema, “Baba, wakati umefika. Dhihirisha utukufu wangu ili nami nikutukuze wewe, 2 kwa kuwa umenipa mamlaka juu ya watu wote, niwape uzima wa milele wale ambao umewakabidhi kwangu. 3 Na huu ndio uzima wa milele: wakufahamu wewe ambaye pekee ni Mungu wa kweli, nakumfah amu Yesu Kristo ambaye umemtuma. 4 Baba nime kutukuza hapa duniani kwa kutimiza kazi uliyonipa niifanye. 5 Na sasa Baba nipe mbele yako ule utukufu niliokuwa nao pamoja na wewe hata kabla dunia haijaumbwa. 6 Nimewafahamisha jina lako wale ambao umenipa kutoka katika ulimwengu. Wao wametii neno lako. 7 Sasa wamefahamu ya kuwa vyote ulivyonipa vinatoka kwako ; 8 kwa kuwa nimewapa ujumbe ulionipa, nao wameupokea. Wamefahamu hakika ya kuwa nimetoka kwako na wameamini kwamba ulinituma. 9 Siwaombei watu wote wa ulimwengu bali nawaombea hawa ulionipa kwa sababu wao ni wako. 10 Wote ulionipa ni wako, na walio wako ni wangu; nao wanadhihirisha utukufu wangu. 11 Mimi naondoka ulimwenguni ninakuja kwako. Lakini wao wako ulimwenguni. Baba Mtakatifu, walinde kwa jina lako ambalo umenipa ili wawe na umoja kama sisi tulivyo mmoja. 12 Nilipokuwa pamoja nao niliwalinda wakawa salama kwa uwezo wa jina ulilonipa. Nimewalinda na hakuna hata mmoja aliyepotea, isipokuwa yule aliyeamua kupotea, ili Maandiko yapate kutimia. 13 Lakini sasa nakuja kwako na ninasema haya wakati nikiwa ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu kikamil ifu. 14 Nimewapa neno lako na ulimwengu umewachukia kwa kuwa wao, kama mimi, si wa ulimwengu huu. 15 Siombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde na yule mwovu shetani. 16 Kama mimi nisivyo mwenyeji wa ulimwengu huu, wao pia sio wa ulimwengu. 17 Watakase kwa neno lako; kwa maana neno lako ndilo kweli. 18 Kama ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nawatuma wao ulim wenguni. 19 Kwa ajili yao nimejitoa wakfu kwako ili na wao wapate kuwa watakatifu kwa kufahamu kweli yako.
Yesu Anawaombea Watakaoamini Baadaye
20 “Siwaombei hawa peke yao; bali nawaombea pia wale wote watakaoniamini kwa sababu ya ushuhuda wa hawa. 21 Ninawaombea wote wawe kitu kimoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi ni ndani yako; ili na wao wawe ndani yetu na ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ulinituma. 22 Nimewapa utukufu ule ule ulionipa ili wawe kitu kimoja kama sisi tulivyo - 23 mimi nikiwa ndani yao na wewe ndani yangu; ili wakamilike katika umoja na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma na kwamba unawapenda kama unavyonipenda mimi. 24 Baba, shauku yangu ni kwamba, hawa watu ulionipa wawepo mahali nilipo ili waweze kuona utukufu wangu; utukufu ambao umenipa kwa kuwa ulinipenda hata kabla ulimwengu haujaumbwa. 25 Baba Mtakatifu, ijapokuwa ulimwengu haukufahamu wewe, mimi ninakufahamu, na hawa wanajua ya kuwa umenituma. 26 Nimekutambulisha wewe kwao, na nitaendelea kulitambulisha jina lako kwao ili upendo ulio nao kwangu uwe upendo wao pia; nami niwe ndani yao.”
Copyright © 1989 by Biblica