Add parallel Print Page Options

Yesu Awafariji Wafuasi Wake

14 Yesu akasema, “Msisumbuke. Mwaminini Mungu, na mniamini na mimi. Kuna vyumba vya kutosha katika nyumba ya Baba yangu. Nisingewaambia hivi ikiwa isingelikuwa kweli. Ninaenda huko kuandaa mahali kwa ajili yenu. Nitakapomaliza kuandaa, nitarudi. Kisha nitawachukua ili muwe pamoja nami mahali niliko. Mnaijua njia iendayo kule ninakokwenda.”

Thomaso akasema, “Bwana, hatujui unakokwenda, sasa tutaijuaje njia?”

Yesu akajibu, “Mimi ndiye njia, kweli, na uzima. Njia pekee ya kwenda kwa Baba ni kupitia kwangu. Kwa kuwa sasa ninyi nyote mmenijua, mtamjua Baba yangu pia. Kwa kweli, sasa mnamjua Baba na mmekwisha kumwona.”

Filipo akamwambia, “Bwana, utuonyeshe Baba. Hilo tu ndilo tunalohitaji.”

Yesu akajibu, “Nimekuwa pamoja nanyi kwa kipindi kirefu. Hivyo wewe, Filipo unapaswa kunijua. Yeyote aliyeniona mimi amemwona Baba pia. Hivyo kwa nini unasema, ‘Utuonyeshe Baba’? 10 Hamwamini kuwa mimi nimo ndani ya Baba na Baba naye yumo ndani yangu? Mambo niliyowaambia hayatoki kwangu. Baba anakaa ndani yangu, naye anafanya kazi yake mwenyewe. 11 Mniamini ninaposema kwamba nimo ndani ya Baba na Baba yumo ndani yangu. Vinginevyo muamini kwa sababu ya miujiza niliyoifanya.

12 Hakika nawaambia, yeyote anayeniamini atafanya mambo kama yale niliyoyafanya. Naye atafanya mambo makubwa zaidi ya yale niliyofanya, kwa sababu mimi naenda kwa Baba. 13 Na kama mtaomba jambo lo lote kwa jina langu, nitawafanyia. Kisha utukufu wa Baba utadhihirishwa kupitia kwa Mwana wake. 14 Ikiwa mtaniomba chochote kwa jina langu, mimi nitakifanya.

Ahadi ya Roho Mtakatifu

15 Ikiwa mnanipenda, mtafanya ninayowaagiza. 16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi[a] mwingine atakayekuwa nanyi siku zote. 17 Huyo Msaidizi ni Roho wa Kweli ambaye watu wa ulimwengu hawawezi kumpokea, kwa sababu hawamwoni wala hawamjui. Lakini ninyi mnamjua kwa kuwa anakaa pamoja nanyi, na atakuwa ndani yenu.

18 Mimi sitawaacha peke yenu kama watu wasiokuwa na wazazi. Bali nitakuja tena kwenu. 19 Katika kipindi kifupi watu wa ulimwengu hawataniona tena. Lakini ninyi mtaniona. Mtaishi kwa sababu mimi ninaishi. 20 Katika siku hiyo mtaelewa kuwa mimi nimo ndani ya Baba. Kadhalika mtajua pia kuwa ninyi mmo ndani yangu nami nimo ndani yenu. 21 Wale wanaonipenda kweli ni wale ambao si tu kwamba wanazijua amri zangu bali pia wanazitii. Baba yangu atawapenda watu wa jinsi hiyo, nami pia nitawapenda. Nami nitajitambulisha kwao.”

22 Kisha Yuda (siyo Yuda Iskariote) akasema, “Bwana, utawezaje kujitambulisha kwetu, lakini si kwa ulimwengu?”

23 Yesu akajibu, “Wale wote wanipendao watayafuata mafundisho yangu. Naye Baba yangu atawapenda. Kisha Baba yangu na mimi tutakuja kwao na kukaa pamoja nao. 24 Lakini yeyote asiyenipenda hafuati mafundisho yangu. Mafundisho haya mnayosikia kwa hakika siyo yangu. Ni kutoka kwa Baba yangu aliyenituma.

25 Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi. 26 Lakini yule Msaidizi atawafundisha kila kitu na kuwafanya mkumbuke kila nilichowaambia. Huyu Msaidizi ni Roho Mtakatifu[b] ambaye Baba atamtuma kwa jina langu.

27 Nawaachia amani. Ninawapa amani yangu mwenyewe. Ninawapa amani kwa namna tofauti kabisa na jinsi ulimwengu unavyofanya. Hivyo msihangaike. Msiogope. 28 Mlinisikia nikiwaambia, ‘Naondoka, lakini nitakuja tena kwenu.’ Mngenipenda, mngefurahi kuwa naenda kwa Baba, kwa sababu Baba ni mkuu kuliko mimi. 29 Nawaambia haya hivi sasa, kabla hayajatokea. Kisha yatakapotokea, mtaamini.

30 Sitaendelea kuongea nanyi kwa muda mrefu zaidi. Mtawala wa ulimwengu[c] huu anakuja. Hata hivyo hana nguvu juu yangu. 31 Lakini ni lazima ulimwengu utambue kuwa ninampenda Baba. Hivyo ninafanya yale Baba aliyoniambia.

Njooni sasa, twendeni.”

Footnotes

  1. 14:16 Msaidizi Au “Mfariji”, Roho Mtakatifu (tazama Roho Mtakatifu katika Orodha ya Maneno). Pia katika 14:26; 15:26; 16:7,8.
  2. 14:26 Roho Mtakatifu Pia anaitwa Roho wa Mungu, Roho wa Kristo, na Mfariji. Katika muungano na Mungu na Kristo, hufanya kazi za Mungu miongoni mwa watu ulimwenguni.
  3. 14:30 Mtawala wa ulimwengu Huu ni Shetani. Tazama Shetani katika Orodha ya Maneno.