Yesu Ndiye Njia Ya Kufika Kwa Mungu

14 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia. Katika nyumba ya baba yangu mna nafasi nyingi. Kama sivyo, nisingeliwaambia kwamba nakwenda kuwaandalia makao. Na nikishawaandalia, nitarudi kuwachukua mkae pamoja nami; ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo. Ninyi mnajua njia ya kufikia ninakokwenda.” Tomaso akamwuliza, “Bwana, hatujui unakokwenda; tutaijuaje njia?” Yesu akawaam bia, “Mimi ndiye Njia na Kweli na Uzima; mtu hawezi kufika kwa Baba bila kupitia kwangu. Kama mngekuwa mnajua mimi ni nani, mngemfahamu na Baba yangu. Tangu sasa mnamfahamu Baba yangu na mmemwona.”

Filipo akamwambia Yesu, “Bwana, tuonyeshe Baba yako nasi tutaridhika.” Yesu akamjibu, “Filipo, imekuwaje hunifahamu baada ya mimi kuwa pamoja nanyi muda wote huu? Mtu ye yote ambaye ameniona mimi, amemwona Baba. Sasa inakuwaje unasema, ‘Tuonyeshe Baba’? 10 Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba yangu, na Baba yangu yuko ndani yangu? Mambo ninayowaambia siyasemi kwa mamlaka yangu mwenyewe, bali yanatoka kwa Baba yangu ambaye anaishi ndani yangu, na ndiye anayetenda haya yote. 11 Niaminini ninapowaambia ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu na Baba yangu yu ndani yangu. La sivyo, niaminini kwa sababu ya haya mambo ninayotenda. 12 Ninawaambia hakika, mtu ye yote akiniamini ataweza kufanya miujiza kama hii na hata zaidi, kwa kuwa mimi ninakwenda kwa Baba yangu. 13 Kitu cho chote mtakachoomba kwa jina langu, nitawafanyia, ili Baba yangu apate kutukuzwa kwa yale ambayo mimi Mwanae nitawafanyia. 14 Mkiniomba cho chote kwa jina langu nitawafanyia.”

Ahadi Ya Kupewa Roho Mtakatifu

15 “Kama mnanipenda mtatimiza amri zangu. 16 Nami nitam womba Baba, naye atawapeni Msaidizi mwingine akae nanyi siku zote. 17 Huyo ndiye Roho wa Kweli ambaye watu wasioamini hawawezi kumpokea. Watu kama hao hawamwoni wala hawamfahamu. Ninyi mnamfahamu kwa kuwa anakaa ndani yenu na ataendelea kuwa nanyi. 18 Sitawaacha kama yatima. Nitarudi kwenu. 19 Baada ya muda mfupi watu wa ulimwengu hawataniona tena, ila ninyi mta niona; na kwa kuwa mimi ni hai, ninyi pia mtakuwa hai. 20 Wakati huo utakapofika mtajua ya kuwa mimi niko ndani ya Baba yangu na ninyi mko ndani yangu. 21 Mtu anayezishika amri zangu na kuziti miza ndiye anayenipenda. Na mtu anayenipenda, Baba yangu atam penda; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.” 22 Yuda, siyo Iskariote, akamwuliza, “Bwana, itakuwaje ujidhihirishe kwetu tu na si kwa ulimwengu mzima?” 23 Yesu akamjibu, “Mtu akinipenda atashika mafundisho yangu na Baba yangu atampenda, nasi tutafanya makao yetu kwake. 24 Mtu asiyenipenda hayashiki mafundisho yangu na mafundisho niliyowapeni si yangu bali yametoka kwa Baba yangu aliyenituma.

25 “Nimewaambia mambo haya wakati nikiwa bado nipo nanyi. 26 Lakini yule Msaidizi, yaani Roho Mtakatifu, ambaye Baba yangu atamtuma kwenu kwa jina langu, atawafundisha mambo yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27 Ninawaachia amani. Nawapeni amani yangu; amani hii ulimwengu hauwezi kuwapa. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope. 28 Kumbukeni nilivyowaambia, ‘Ninakwenda, na nitarudi.’ Kama kweli mngalinipenda mngefurahi, kwa kuwa nakwenda kwa Baba; na Baba yangu ni mkuu kuliko mimi. 29 Na sasa nimewaambia mambo haya kabla hayajatokea ili yataka potokea mpate kuamini. 30 Sitasema tena mengi nanyi kwa sababu mtawala wa dunia hii anakuja. Yeye hana uwezo juu yangu. 31 Lakini ninatii amri ya Baba ili ulimwengu upate kujua kwamba nampenda Baba. Simameni tuondoke hapa.’ ’