Add parallel Print Page Options

Jitoe Mwenyewe kwa Mungu

Mapigano na magombano yanatokea wapi miongoni mwenu? Je, hayatoki kutoka ndani yenu wenyewe, kutoka katika tamaa zenu za starehe ambazo zinafanya vita siku zote ndani ya miili yenu? Mnataka mambo lakini hamyapati, hivyo mnaua na mnakuwa na wivu juu ya watu wengine. Lakini bado hamwezi kuyafikia mnayoyataka, hivyo mnagombana na kupigana. Nanyi ndugu zangu hampokei mambo mnayoyataka kwa sababu hamumwombi Mungu. Na mnapoomba, lakini hampokei cho chote kwa sababu mnaomba kwa dhamiri mbaya, ili muweze kuvitumia mlivyopatiwa kwa anasa zenu.

Watu msio waaminifu, hamjui kwamba kuupenda ulimwengu ni sawa na kumchukia Mungu? Yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hujifanya mwenyewe kuwa adui wa Mungu. Je, kile Maandiko yanachokisema hakina maana yoyote kwenu? Ile roho ambayo Mungu aliifanya ikae ndani yetu wanadamu imejaa tamaa yenye wivu? Lakini Mungu ametuonesha sisi, rehema kuu zaidi. Ndiyo maana Maandiko yanasema:

Mungu huwapinga wenye kiburi,
    lakini huwapa neema wale walio wanyenyekevu.(A)

Kwa hiyo jiwekeni chini ya Mungu. Mpingeni Shetani naye atawakimbia ninyi. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Iosheni mikono yenu ninyi wenye dhambi na kuitakasa mioyo yenu enyi wanafiki! Ombolezeni na kulia! Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa maombolezo, na furaha yenu igeuzwe kuwa huzuni kubwa. 10 Jinyenyekezeni chini ya Bwana, naye atawainua juu.

Wewe Siyo Hakimu

11 Ndugu, msiendelee kukosoana ninyi kwa ninyi. Yeye anayemnenea mabaya ndugu yake au anayemhukumu ndugu yake atakuwa anailaumu Sheria na atakuwa anaihukumu Sheria. Na kama utaihukumu Sheria, hautakuwa unafanya yale yanayosemwa na Sheria, bali utakuwa ni hakimu. 12 Kuna Mtoa Sheria mmoja tu na hakimu, ndiye Mungu aliye na uwezo wa kuokoa na kuangamiza. Hivyo wewe unafikiri ni nani, wewe unayemhukumu jirani yako?

Mwache Mungu Apange Maisha Yako

13 Sikilizeni mnaosema, “Leo au kesho tutasafiri kwenda kwenye mji huu au ule, na tutakaa mwaka mzima pale, tutafanya biashara hapo na kujipatia fedha nyingi.” 14 Hamjui hata yatakayotokea katika maisha yenu kesho yake tu. Kwani ninyi ni mvuke tu ambao huonekana kwa kipindi kifupi tu kisha hutoweka. 15 Badala yake, nyakati zote mngesema, “Kama Bwana anapenda, tutaishi na tutafanya hivi au vile.” 16 Kama ilivyo, ninyi mna kiburi na kujivuna. Majivuno yote ya jinsi hiyo ni uovu! 17 Hivyo sasa, mnaposhindwa kufanya mliyoyajua ni haki, mtakuwa na hatia ya dhambi.

Onyo kwa Matajiri na Wachoyo

Sikilizeni, ninyi matajiri! Ombolezeni na kulia kwa sauti kwa ajili ya dhiki inayowajia. Utajiri wenu umeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu zenu na fedha vimeliwa na kutu! Hiyo kutu itakuwa ni ushuhuda dhidi yenu, na itaila miili yenu kama kwa moto. Mmejilimbikizia mali kwa ajili yenu katika kizazi hiki cha siku za mwisho! Angalieni! Mmeyazuia malipo ya wafanyakazi waliopalilia mashamba yenu. Sasa wananililia! Na kilio cha hao wanaovuna pia kimeyafikia masikio ya Bwana Aliye na Nguvu.

Mmeishi maisha ya anasa duniani na kujifurahisha na kila kitu mlichotaka. Mmeinenepesha miili yenu, kama wanyama walio tayari kwa siku ya kuchinjwa. Mmehukumu na kuua wale watu wasio na hatia, na ambao hawakupingana nanyi.

Uwe Mstahimilivu

Hivyo kina kaka na kina dada, muwe na subira; hadi kuja kwa mara ya pili kwa Bwana. Kumbukeni kuwa mkulima huyasubiria mazao yake yenye thamani yakue ardhini. Huyangoja kwa subira mpaka yapate mvua za masika na za vuli.[a] Hata ninyi pia mnapaswa kungoja kwa subira. Muwe imara mioyoni mwenu, kwa sababu kuja kwa Bwana mara ya pili kumekaribia. Kaka na dada zangu, msiendelee kunung'unikiana ninyi kwa ninyi, ili msije kuhukumiwa kuwa na hatia. Tazameni! Hakimu anasimama mlangoni akiwa tayari kuingia ndani.

10 Kina kaka na kina dada, fuateni mfano wa manabii waliosema kwa jina la Bwana. Wao walipata mateso mengi mabaya lakini walivumilia. 11 Na tunatoa heshima kubwa sana kwa wale wote waliostahimili mateso. Mmesikia juu ya uvumilivu wa Ayubu,[b] na mnayajua ya kuwa baada ya yote hayo Bwana alimsaidia. Hii basi inaonesha ya kuwa Bwana ni mwenye wingi wa rehema na huruma.

Uwe Makini na Unayosema

12 Juu ya mambo yote kaka zangu na dada zangu, usitumie kiapo unapotoa ahadi, Usiape kwa mbingu wala kwa dunia, ama kwa kitu kingine chochote. “Ndiyo” yenu na iwe “Ndiyo halisi”, na “Hapana” yenu na iwe “Hapana halisi”, ili msije mkaingia katika hukumu ya Mungu.

Nguvu ya Maombi

13 Je, miongoni mwenu kuna aliye na shida? Anapaswa kuomba. Je, yupo yeyote mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa. 14 Je, kuna yeyote kwenu aliye mgonjwa? Anapaswa kuwaita wazee wa kanisa kumwombea na kumpaka mafuta katika jina la Bwana. 15 Maombi yanayofanywa kwa imani yatamfanya mgonjwa apone, na Bwana atampa uzima. Kama atakuwa ametenda dhambi, Bwana atamsamehe.

16 Hivyo muungame dhambi ninyi kwa ninyi, na kuombeana ninyi kwa ninyi ili muweze kuponywa. Maombi yanayofanywa na mtu mwenye haki yana nguvu sana na yana matokeo makubwa sana. 17 Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi tulivyo. Aliomba kwamba mvua isinyeshe, na haikunyesha katika ardhi kwa miaka mitatu na nusu. 18 Kisha akaomba tena inyeshe, na anga ikatoa mvua, na ardhi ikatoa mazao.

Kuwasaidia Watu Wanapotenda Dhambi

19 Kaka na dada zangu Ndugu zangu, kama mmoja wenu atapotoka katika kweli, na mwingine akamrejeza, 20 yule aliyemrejeza atambue kuwa yule anayemrejeza mtenda dhambi kutoka katika njia yake mbaya ataiokoa roho ya huyo mtu kutoka katika kifo cha milele na atasababisha dhambi nyingi zisamehewe.

Footnotes

  1. 5:7 mvua za masika na za vuli “Mvua za masika” zilinyesha mwanzoni na “mvua za vuli” zilinyesha mwishoni.
  2. 5:11 uvumilivu wa Ayubu Tazama Kitabu cha Ayubu katika Agano la Kale.

Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu.[a] Mimi ni mtume kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu atupaye tumaini.

Ninakuandikia wewe, Timotheo. Wewe ni kama mwanangu halisi kwa sababu ya imani yetu.

Neema, rehema na amani kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu ziwe pamoja nawe.

Maonyo kuhusu Mafundisho ya Uongo

Nilipokwenda Makedonia, nilikuomba ubaki Efeso. Baadhi ya watu huko wanafundisha mambo yasiyo ya kweli, nami ninataka uwaonye waache. Uwaambie wasitumie muda wao kusimulia simulizi zisizo na maana za mambo ya kale na kutengeneza orodha ndefu ya mababu. Mambo hayo husababisha mabishano tu na hayaisaidii katika kuikamilisha kazi ya Mungu tuliyopewa, ambayo ni lazima tuikamilishe kwa imani. Kusudi langu la kukueleza ufanye jambo hili ni kutaka kukuza upendo; aina ya upendo unaooneshwa na wale ambao mawazo yao ni safi; watu ambao hufanya yale wanayojua kuwa ni sahihi na ambao imani yao kwa Mungu ni ya kweli. Lakini wengine wamekosa jambo hili la msingi katika mafundisho yao na wamepoteza mwelekeo. Sasa wanazungumza juu ya mambo yasiyo na msaada kwa mtu yeyote. Wanataka kuwa walimu wa sheria,[b] lakini hawafahamu mambo wanayosema, wanasema kwa ujasiri wote juu ya mambo wasiyoyaelewa wenyewe.

Tunajua kwamba sheria ni nzuri ikiwa mtu anaitumia kwa usahihi. Pia tunajua kwamba sheria haikutengenezwa kwa ajili ya wale wanaotenda haki. Imetengenezwa kwa ajili ya wale wanayoipinga na kukataa kuifuata. Sheria ipo kwa ajili ya wenye dhambi wanaompinga Mungu na mambo yote yanayompendeza. Ipo kwa ajili ya wale wasio na hamu ya mambo ya kiroho na kwa ajili ya wale wanaowaua baba au mama zao au mtu yeyote yule. 10 Ipo kwa ajili ya watu wanaotenda dhambi ya uasherati, kwa wanaume wanaolala na wanaume wenzao au wavulana, kwa wote wanaoteka watu na kuwauza kama watumwa, kwa wote wanaodanganya au wale wasiosema ukweli wakiwa katika kiapo, na kwa ajili ya wale walio kinyume na mafundisho ya kweli ya Mungu. 11 Mafundisho hayo ni sehemu ya Habari Njema ambayo Mungu wetu wa utukufu alinipa kuhubiri na ndani yake tunauona utukufu wake.

Shukrani kwa Rehema za Mungu

12 Ninamshukuru Kristo Yesu Bwana wetu kwa sababu aliniamini na kunipa kazi hii ya kumtumikia. Yeye hunitia nguvu ya kufanya kazi hii. 13 Hapo zamani nilimtukana Kristo. Nikiwa mtu mwenye majivuno na mkorofi, niliwatesa watu wake. Lakini Mungu alinihurumia kwa sababu sikujua nilichokuwa nafanya. Nilifanya hayo kabla sijaamini. 14 Lakini Bwana wetu alinipa kiwango kikubwa cha neema yake. Na pamoja na neema hiyo imani na upendo ulio katika Kristo Yesu vilifuata.

15 Huu ndiyo usemi wa kweli unaopaswa kukubaliwa pasipo kuuliza maswali; kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, nami ni mbaya zaidi ya wote. 16 Lakini nilipata rehema kwa sababu ili Kristo Yesu aweze kunitumia, mimi mtenda dhambi kuliko wote, ili kuonesha uvumilivu wake usio na kikomo. Alitaka niwe mfano kwa wale ambao wangemwamini na kupata uzima wa milele. 17 Heshima na utukufu kwa mfalme anayetawala milele. Hawezi kuharibiwa wala kuonekana. Heshima na utukufu apewe Mungu wa pekee milele na milele, Amina.

18 Timotheo wewe ni mwanangu mwenyewe kwa sababu ya ushirika wetu wa imani ya kweli. Ninayokuambia kuyatenda yanakubaliana na unabii[c] ambao ulisemwa juu yako hapo zamani. Nataka uukumbuke unabii huo na kupigana vita vizuri vya imani. 19 Endelea kumwamini Mungu na kutenda yale unayojua kuwa ni sahihi. Watu wengine hawajatenda haya, na imani yao sasa imeharibiwa. 20 Himenayo na Iskanda ni mfano wa watu hao. Nimewakabidhi kwa Shetani ili wafundishwe kutosema kinyume cha Mungu.

Mungu Anataka Tumwombee Kila Mtu

Kwanza kabisa, ninakuagiza uwaombee watu wote. Uwaombee kwa Mungu ili awabariki na kuwapa mahitaji yao. Kisha umshukuru Yeye. Unapaswa kuwaombea watawala na wote wenye mamlaka. Uwaombee viongozi hawa ili tuweze kuishi maisha yenye utulivu na amani, maisha yaliyojaa utukufu kwa Mungu na yanayostahili heshima. Hili ni jambo jema na linampendeza Mungu Mwokozi wetu.

Mungu anataka kila mtu aokolewe na aielewe kweli kikamilifu. Kuna Mungu mmoja tu, na kuna mwanadamu mmoja tu anayeweza kuwaleta pamoja wanadamu wote na Mungu wao. Huyo mtu ni Kristo Yesu kama mwanadamu. Alijitoa mwenyewe kulipa deni ili kila mtu awe huru. Huu ni ujumbe ambao Mungu alitupa wakati unofaa. Nami nilichaguliwa kama mtume kuwaambia watu ujumbe huo. Ninasema kweli. Sidanganyi. Nilichaguliwa kuwafundisha wasio Wayahudi na nimefanya kazi hii kwa imani na ukweli.

Maagizo Maalumu kwa Wanawake na Wanaume

Nataka wanaume walio kila mahali waombe. Ni lazima wawe watu wanaoishi kwa kumpendeza Mungu na wanaonyoosha mikono yao wanapoomba na wawe watu wasio na hasira na wanaopenda mabishano.

Na ninawataka wanawake wajipambe kwa namna inayofaa. Mavazi yao yawe yanayofaa na yanayostahili. Hawapaswi kuvutia watu kwa kutengeneza nywele zao kwa mitindo ya ajabu ama kwa kuvaa dhahabu, vito au lulu au nguo za gharama. 10 Lakini wajipambe na kuvutia kwa matendo mema wanayofanya. Hayo ndiyo yanayofaa zaidi kwa wanawake wanaosema kuwa wamejitoa kwa ajili ya Mungu.

11 Mwanamke anapaswa kujifunza akisikiliza kwa utulivu huku akiwa radhi kutii kwa moyo wake wote. 12 Simruhusu mwanamke kumfundisha mwanaume au kumwelekeza jambo la kufanya. Bali lazima asikilize kwa utulivu, 13 kwa sababu Adamu aliumbwa kwanza na Hawa akaumbwa baadaye. 14 Na Adamu hakudanganywa.[d] Bali mwanamke ndiye aliyedanganywa naye akatenda dhambi. 15 Lakini wanawake wataokolewa kwa jukumu lao la kuzaa watoto.[e] Wakiendelea kuishi katika imani, upendo, utakatifu na tabia njema.

Footnotes

  1. 1:1 Kristo Yesu Au “Mfalme Yesu”. Neno “Kristo” ni tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi”, ambao ni wadhifa wa kifalme. Tazama Mk 15:32: Lk 23:2. Tazama pia Kristo na Masihi katika Orodha ya Maneno.
  2. 1:7 sheria “Sheria” pengine ni “sheria ya Mungu” ambayo Mungu alimpa Musa kwa ajili ya watu wake. Tazama Sheria katika Orodha ya Maneno. Pia katika mstari wa 8.
  3. 1:18 unabii “Unabii” ina maana mambo ambayo manabii waliyasema juu ya maisha ya Timotheo kabla ya yote kutokea.
  4. 2:14 Adamu hakudanganywa “Adamu siye aliyedanganywa” Shetani alimdanganya Hawa, naye Hawa alisababisha Adamu kutenda dhambi. Tazama Mwa 3:1-13.
  5. 2:15 kuzaa watoto Kwa maana ya kawaida, “Ataokolewa katika kazi yake ya kuzaa watoto.” Kuzaa watoto, inaweza kutumika hapa kama kielelezo cha maana ya “kuzaa sifa njema”, zinazofafanuliwa katika mstari unaofuata.