Kuhusu Kuutawala Ulimi

Ndugu zangu, wengi wenu msiwe walimu, kwa maana mnafahamu kwamba sisi tufundishao tutahukumiwa vikali zaidi. Sisi sote hufanya makosa mengi. Ikiwa kuna mtu asiyekosea kwa usemi wake, huyo ni mkamilifu, naye anaweza kuutawala mwili wake wote.

Tunapowawekea farasi lijamu vinywani mwao ili watutii, tunatawala miili yao yote. Kadhalika meli, ingawa ni kubwa sana na huendeshwa na upepo mkali, lakini huongozwa na usukani mdogo sana, ikaenda ko kote anakotaka nahodha. Ulimi nao ni kiungo kidogo sana lakini hujivunia mambo makuu. Fikirini jinsi moto mdogo unavyoweza kuteketeza msitu mkubwa! Ulimi pia ni kama moto. Ulimi ni ulimwengu wa uovu kati ya viungo vyetu. Humchafua mtu nafsi nzima na kuwasha moto maisha yake yote, nao ulimi huwashwa moto wa kuzimu. Wanyama wa kila aina, ndege, nyoka na viumbe vya baharini wanafugwa na wamekwisha kufugwa na binadamu. Lakini hakuna mtu awezaye kuufuga ulimi. Ni uovu unaohangaika huku na kule, uliojaa sumu inayoua.

Kwa kutumia ulimi tunamsifu Bwana na Baba yetu na kwa ulimi huo huo tunawalaani watu ambao wameumbwa kwa mfano wa Mungu. 10 Katika kinywa hicho hicho hutoka sifa na laana. Ndugu zangu, haipaswi kuwa hivyo. 11 Je, chemchemi yaweza kutoa kutoka katika tundu moja maji matamu na maji machungu? 12 Je, ndugu zangu, mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu waweza kuzaa tini? Pia haiwezekani chemchemi ya chumvi kutoa maji matamu.

Aina Mbili Za Hekima

13 Ni nani miongoni mwenu aliye na hekima na ufahamu? Basi aonyeshe hayo kwa maisha yake mazuri na kwa matendo yake anayot enda kwa unyenyekevu utokanao na hekima. 14 Lakini ikiwa mna wivu wenye chuki na kufikiria mno maslahi yenu binafsi, msiji sifie hayo wala kuikataa kweli. 15 Hekima ya namna hiyo haishuki kutoka mbinguni bali ni ya kidunia; si hekima ya kiroho bali ni ya shetani. 16 Kwa maana penye wivu na ubinafsi, ndipo penye machafuko na kila tendo ovu.

17 Lakini hekima itokayo mbinguni kwanza ni safi, kisha ni yenye kupenda amani, yenye kufikiria wengine, yenye unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, na ya kweli. 18 Wapenda-amani wapandao katika amani huvuna mavuno ya haki.