Add parallel Print Page Options

Uzima Katika Roho

Hivyo mtu yeyote aliye wa Kristo Yesu hana hukumu ya kifo. Hiyo ni kwa sababu kwa njia ya Kristo Yesu sheria ya Roho inayoleta uzima imewaweka ninyi[a] huru kutoka katika sheria inayoleta dhambi na kifo. Ndiyo, sheria haikuwa na nguvu ya kutusaidia kwa sababu ya udhaifu wetu wa kibinadamu. Lakini Mungu akafanya kile ambacho sheria haikuweza kufanya: Alimtuma Mwanaye duniani akiwa na mwili ule ule tunaoutumia kutenda dhambi. Mungu alimtuma ili awe njia ya kuiacha dhambi. Alitumia maisha ya mwanadamu ili kuipa dhambi hukumu ya kifo. Mungu alifanya hivi ili tuweze kuishi kama sheria inavyotaka. Sasa tunaweza kuishi hivyo kwa kumfuata Roho na si kwa jinsi ya udhaifu wa kibinadamu.

Watu wanaoishi kwa kufuata udhaifu wa kibinadamu[b] huyafikiri yale wanayoyataka tu. Lakini wale wanaoishi kwa kumfuata Roho huyafikiri yale Roho anayotaka wafanye. Ikiwa fikra zenu zinaongozwa na udhaifu wa kibinadamu, kuna kifo cha kiroho. Lakini ikiwa fikra zenu zinaongozwa na Roho, kuna uhai na amani. Je, hili ni kweli? Kwa sababu kila mtu ambaye fikra zake zinaongozwa na udhaifu wa kibinadamu yuko kinyume na Mungu maana hukataa kuitii sheria ya Mungu. Na kwa hakika hawawezi kutii. Wale wanaotawaliwa na udhaifu wa kibinadamu hawawezi kumpendeza Mungu.

Lakini ninyi hamtawaliwi na udhaifu wenu wa kibinadamu, bali mnatawaliwa na Roho, ikiwa Roho huyo wa Mungu anakaa ndani yenu. Na mtu yeyote asiye na Roho wa Kristo, huyo si wa Kristo. 10 Miili yenu inaelekea kifo kwa sababu ya dhambi. Lakini ikiwa Kristo anaishi ndani yenu, basi Roho anawapa uzima kwa sababu ya uaminifu wa wema wa Mungu.[c] 11 Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. Na ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu, ataifanya hai tena miili yenu inayokufa. Ndiyo, Mungu ndiye aliyemfufua Kristo kutoka kwa wafu, naye atawafufua ninyi na kuwapa uzima kupitia Roho wake anayeishi ndani yenu.

12 Hivyo, kaka na dada zangu, ni lazima tusitawaliwe na udhaifu wa kibinadamu kwa kufuata tamaa zake. 13 Ikiwa mtayatumia maisha yenu kufanya yale ambayo udhaifu wenu wa kibinadamu unataka, mtakufa kiroho. Lakini ikiwa mtaupokea msaada wa Roho na mkaacha kutenda mambo mabaya mnayotenda na miili yenu, mtakuwa na uzima wa kweli.

14 Watoto wa kweli wa Mungu ni wale wanaokubali kuongozwa na Roho wa Mungu. 15 Roho tuliyempokea si roho anayetufanya kuwa watumwa tena na kutusababisha tuwe na hofu. Roho tuliye naye hutufanya tuwe watoto waliochaguliwa na Mungu. Na kwa Roho huyo twalia “Aba,[d] yaani Baba.” 16 Na Roho mwenyewe huzungumza na roho zetu na kutuhakikishia kuwa sisi ni watoto wa Mungu. 17 Nasi kwa kuwa ni watoto wa Mungu, basi sisi ni warithi, warithi wa Mungu na warithi pamoja na Kristo. Mungu atatupa yale yote aliyompa Kristo. Sisi tunaoteseka sasa kama Kristo alivyoteseka tutashiriki katika utukufu wake.

Wakati Wetu wa Utukufu Unakuja

18 Nanayachukulia mateso ya sasa kuwa si kitu ukilinganisha na utukufu mkuu tunaoutarajia. 19 Hata uumbaji una shauku kuu, ukisubiri kwa hamu wakati ambapo atawadhihirisha “watoto halisi wa Mungu”[e] kuwa ni na. 20 Kila alichokiumba Mungu kiliruhusiwa kuwa na mapungufu kana kwamba hakitafikia utimilifu wake. Hilo halikuwa kwa matakwa ya viumbe, lakini Mungu aliruhusu hayo yatokee kwa mtazamo wa tumaini hili: 21 kwamba uumbaji ungewekwa huru mbali na uharibifu, na kwamba kila alichokiumba Mungu kiwe na uhuru na utukufu ule ule ulio wa watoto wa Mungu.

22 Tunajua kuwa kila kitu alichoumba Mungu kimekuwa kikingoja hadi sasa katika kuugua na uchungu kama wa mwanamke aliye tayari kuzaa mtoto. 23 Siyo uumbaji tu, bali sisi pia tumekuwa tukingoja kwa kuugua na uchungu ndani yetu. Tunaye Roho kama sehemu ya kwanza ya ahadi ya Mungu. Kwa hiyo tunamngoja Mungu amalize kutufanya sisi watoto wake yeye mwenyewe. Nina maana kuwa tunasubiri kuwekwa huru kwa miili yetu. 24 Tuliokolewa ili tuwe na tumaini hili. Ikiwa tunaweza kuona kile tunachokisubiri, basi hilo siyo tumaini la kweli. Watu hawatumaini kitu ambacho tayari wanacho. 25 Lakini tunatumaini kitu tusichokuwa nacho, na hivyo tunakisubiri kwa uvumilivu.

26 Roho hutusaidia pia. Sisi ni dhaifu sana, lakini Roho hutusaidia katika udhaifu wetu. Hatujui jinsi ya kuomba kama Mungu anavyotaka, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa Mungu kwa kuungua kusikotamkika. 27 Tayari Mungu anayajua mawazo yetu ya ndani sana. Na anaelewa Roho anataka kusema nini, kwa sababu Roho huomba kwa ajili ya watu wa Mungu katika namna inayokubaliana na mapenzi ya Mungu.

28 Tunajua kwamba katika kila kitu Mungu[f] hufanya kazi ili kuwapa mema wale wanaompenda. Hawa ni watu aliowachagua Mungu, kwa sababu huo ndiyo ulikuwa mpango wake. 29 Mungu aliwajua kabla hajauumba ulimwengu. Na aliamua hao wangekuwa kama Mwanaye. Na Yesu angekuwa mzaliwa wa kwanza wa watoto wake wengi. 30 Mungu aliwakusudia wao wawe kama Mwanaye. Aliwachagua na kuwahesabia haki pamoja na Mungu. Na alipowahesabia haki, akawapa utukufu wake.

Mungu Huonesha Pendo lake Kupitia Yesu

31 Hivyo tuseme nini juu ya hili? Ikiwa Mungu yuko kwa ajili yetu, hakuna anayeweza kuwa kinyume nasi. 32 Naye alimwacha mwanae ateswe kwa ajili yetu. Mungu alimtoa Mwanaye kwa ajili yetu sisi sote. Sasa kwa kuwa tu wa Kristo, hakika Mungu atatupa mambo mengine yote. 33 Nani atakayewashitaki watu waliochaguliwa na Mungu? Hayupo! Mungu ndiye hutuhesabia haki. 34 Ni nani anaweza kuwahukumu watu wa Mungu kuwa wana hatia? Hayupo! Kristo Yesu alikufa kwa ajili yetu na alifufuliwa kutoka kwa wafu. Na sasa ameketi upande wa kulia wa Mungu na anazungumza na Mungu kwa ajili yetu. 35 Je, kuna kitu chochote kinachoweza kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni matatizo au shida au mateso? Ikiwa hatuna chakula au mavazi au tunakabiliwa na hatari au kifo, je mambo hayo yatatutenga sisi kutoka katika upendo wake? 36 Kama Maandiko yanavyosema,

“Kwa ajili yako, tunakabiliana na kifo wakati wote.
    Watu wanadhani hatuna thamani kama kondoo wanaowachinja.”(A)

37 Lakini katika shida zote hizo tuna ushindi kamili kupitia Mungu, aliyetuonyesha upendo wake. 38-39 Ndiyo, nina uhakika kuwa hakuna kitu kinachoweza kututenganisha sisi na upendo wa Mungu, si kifo, maisha, malaika, wala roho zinazotawala. Nina uhakika kuwa hakuna wakati huu, hakuna wakati ujao; hakuna mamlaka, hakuna kilicho juu yetu au chini yetu, hakuna katika ulimwengu wote ulioumbwa, kitakachoweza kututenganisha sisi na upendo wa Mungu ulioonyeshwa kwetu katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Footnotes

  1. 8:2 imewaweka ninyi Nakala zingine za Kiyunani zina “mimi” Vilevile katika sentensi inayofuata.
  2. 8:5 kibinadamu Yaani tamaa za mwili, nafsi na dhambi.
  3. 8:10 kwa sababu … Mungu Ama kwa sababu mmekombolewa (mmewekwa huru) kutoka dhambi na mauti.
  4. 8:15 Aba Ni neno la Kiaramu lililotumiwa na watoto wa Kiyahudi kama jina la kuwaita baba zao.
  5. 8:19 watoto halisi wa Mungu Kwa maana ya kawaida, “wana wa Mungu”, hapa Paulo anasisitiza tofauti kati ya waamini na mfalme wa Kirumi ambaye alikuwa anajidai kuwa ni “mwana wa Mungu”.
  6. 8:28 Mungu Au “Roho”.