Add parallel Print Page Options

Watu 144,000 wa Israeli

Baada ya hili kutokea, niliwaona malaika wanne wamesimama kwenye pembe nne za dunia wakiwa wamezishikilia pepo nne za dunia. Walikuwa wanazuia upepo kupuliza katika nchi au katika bahari au kwenye mti wowote. Kisha nikaona malaika mwingine akija akitokea upande wa mashariki. Malaika huyu alikuwa na muhuri wa Mungu aliye hai. Malaika akawaita kwa sauti kuu malaika wale wanne. Malaika hawa wanne walikuwa malaika ambao Mungu amewapa mamlaka ya kuidhuru dunia na bahari. Malaika akawaambia, “Msiidhuru nchi au bahari au miti kabla hatujawawekea alama kwenye vipaji vya nyuso zao wale wanaomtumikia Mungu wetu.”

Kisha nikasikia idadi ya watu wenye alama ya Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao. Walikuwa watu 144,000. Walitoka katika kila kabila la Israeli:

Kutoka katika kabila la Yuda walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Rubeni walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Gadi walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Asheri walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Naftali walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Manasse walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Simeoni walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Lawi walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Isakari walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Zabuloni walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Yusufu walikuwa elfu kumi na mbili

Kutoka katika kabila la Benjamini walikuwa elfu kumi na mbili.

Umati Mkubwa

Kisha nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu. Walikuwa wengi hakuna mtu angeweza kuwahesabu wote. Walikuwa wametoka katika kila taifa, kabila, rangi za watu na lugha za dunia. Walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo. Wote walikuwa wamevaa majoho meupe na wameshika matawi ya mitende mikononi mwao. 10 Walipaza sauti kwa nguvu, wakasema “Ushindi ni wa Mungu wetu, anayeketi kwenye kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo.”

11 Wazee na wenye uhai wanne walikuwa pale. Malaika wote walikuwa wamesimama kuwazunguka na kukizunguka kiti cha enzi. Malaika wakainamisha nyuso zao, wakasujudu mpaka chini mbele ya kiti cha enzi, wakamwabudu Mungu. 12 Walisema, “Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, nguvu na uweza ni vyake Mungu wetu milele na milele. Amina!”

13 Kisha mmoja wa wazee akaniuliza, “Watu hawa waliovaa kanzu nyeupe ni akina nani? Wametoka wapi?”

14 Nikajibu, “Wewe unajua ni akina nani, bwana.”

Mzee akasema, “Hawa ni wale waliokuja kutokana na mateso makuu. Wamefua kanzu zao[a] kwa kutumia damu ya Mwanakondoo, wako safi na ni weupe. 15 Hivyo sasa watu hawa wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Wanamwabudu Mungu mchana na usiku hekaluni mwake. Naye aketiye kwenye kiti cha enzi atawalinda. 16 Hawatasikia njaa tena. Hawatasikia kiu tena. Jua halitawadhuru. Hakuna joto litakalowachoma. 17 Mwanakondoo mbele ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao. Atawaongoza kwenda kwenye chemichemi za maji ya uzima. Na Mungu atafuta kila chozi kutoka kwenye macho yao.”

Footnotes

  1. 7:14 Wamefua kanzu zao Inamaanisha kwamba walimwamini Yesu na wamesafishwa dhambi zao kwa sadaka ya yake ya damu. Tazama Ufu 5:9; Ebr 9:14; 10:14-22; Mat 22:16; 1 Yoh 1:7.