Muhuri Wa Saba

Mwana-Kondoo alipofungua muhuri wa saba, mbinguni palikuwa kimya kwa muda upatao nusu saa hivi. Kisha nikawaona wale mal aika saba wanaosimama mbele za Mungu, nao wakapewa tarumbeta saba.

Malaika mwingine aliyekuwa na chetezo cha dhahabu, alikuja akasimama mbele ya madhabahu. Akapewa ubani mwingi auchanganye pamoja na sala za watu wote wa Mungu, kwenye madhabahu ya dhahabu iliyo mbele ya kile kiti cha enzi. Ule moshi wa ubani ukapanda juu mbele za Mungu, pamoja na maombi ya watu wa Mungu , kutoka mkononi mwa huyo malaika. Halafu yule malaika akachukua kile chetezo akakijaza moto kutoka kwenye ile madhabahu akautupa juu ya nchi. Pakatokea radi, ngurumo, umeme na tetemeko la nchi.

Tarumbeta Za Kwanza Nne

Kisha wale malaika saba waliokuwa na tarumbeta saba waka jiandaa kuzipiga. Malaika wa kwanza akapiga tarumbeta yake, pakatokea mvua ya mawe na moto uliochanganyika na damu, ikanyesha kwa nguvu juu ya nchi; na theluthi moja ya nchi ikateketea, na theluthi moja ya miti ikateketea na majani yote mabichi yakateke tea.

Malaika wa pili akapiga tarumbeta yake na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto kikatupwa baharini. Theluthi moja ya bahari ikageuka kuwa damu, theluthi moja ya viumbe hai waishio bahar ini wakafa na theluthi moja ya meli zikaharibiwa.

10 Malaika wa tatu akapiga tarumbeta yake, na nyota kubwa iliyokuwa ikiwaka kama taa ilianguka kutoka angani, ikaangukia theluthi moja ya mito na chemchemi za maji. 11 Nyota hiyo inaitwa “Uchungu”. Theluthi moja ya maji yakawa machungu, na watu wengi walikufa kutokana na maji hayo kwa maana yalikuwa machungu.

12 Kisha malaika wa nne akapiga tarumbeta, na theluthi moja ya jua, theluthi moja ya mwezi na theluthi moja ya nyota, zika pigwa. Kwa hiyo theluthi moja ya mwanga wao ukawa giza. Theluthi moja ya mchana ilikuwa haina mwanga na pia theluthi moja ya usiku.

13 Halafu tena nikatazama, nikasikia tai mmoja akipiga kelele kwa sauti kuu wakati akiruka katikati ya mbingu, “Ole wao! Ole wao! Ole wao watu waishio duniani wakati itakaposikika milio ya tarumbeta ambazo karibuni zitapigwa na malaika watatu waliobakia.”