Wimbo Wa Musa Na Mwana-Kondoo

15 Ndipo nikaona ishara nyingine mbinguni, ishara kubwa na ya ajabu: malaika saba wenye maafa saba ya mwisho, kwa maana, maafa hayo yanakamilisha ghadhabu ya Mungu.

Na nikaona kitu kama bahari ya kioo imechanganyika na moto. Na kando ya hiyo bahari, walikuwa wamesimama wale watu waliom shinda yule mnyama na sanamu yake pamoja na namba ya jina lake. Walikuwa wameshika vinubi walivyopewa na Mungu. Nao waliimba wimbo wa Musa, mtumishi wa Mungu na wimbo wa Mwana-Kondoo wakisema, ‘ ‘Matendo yako Bwana Mungu Mwenyezi, ni makuu na ya ajabu! Njia zako wewe Mfalme wa Mataifa ni za haki na za kweli! Ni nani asiyekucha wewe Bwana na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako ni mtakatifu. Mataifa yote yatakuja na kukuabudu kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha dhihirishwa.”

Baada ya hapo nikatazama, nikaona mbinguni Hekalu, yaani hema ya ushuhuda, imefunguliwa. Basi wale malaika saba wenye maafa saba wakatoka humo Hekaluni wakiwa wamevaa nguo za kitani safi zing’aazo na vifuani mwao walivaa mikanda ya dhahabu. Kisha mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai, akawapa wale mal aika saba mabakuli saba ya dhahabu yalizojaa ghadhabu ya Mungu aishiye milele na milele. Na Hekalu ilijaa moshi uliotokana na utukufu na uweza wake, wala hakuna mtu aliyeweza kuingia Hekaluni mpaka yale maafa saba ya wale malaika saba yakamilike.