Matendo 6-13
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Watu Saba Wachaguliwa kwa Kazi Maalumu
6 Watu wengi zaidi walipokuwa wafuasi wa Yesu. Wafuasi waliokuwa wakizungumza Kiyunani walianza kuwalalamikia wafuasi wenzao waliokuwa wanazungumza Kiebrania au Kiaramu. Walisema kuwa wajane wao walikuwa hawapewi mgao wao kutokana na kile wafuasi walikuwa wanapewa kila siku. 2 Mitume kumi na mbili wakaita kundi lote la wafuasi pamoja.
Mitume wakawaambia, “Haitakuwa sahihi sisi kuacha kazi yetu ya kuwafundisha watu neno la Mungu ili tuwe wasimamizi wa ugawaji wa chakula kwa watu. 3 Hivyo, kaka zetu na dada zetu, chagueni wanaume saba miongoni mwenu wenye ushuhuda mzuri, watu waliojaa hekima na Roho. Nasi tutawaweka kuwa wasimamizi wa kazi hii muhimu. 4 Na hivyo itatuwezesha sisi kutumia muda wetu wote katika kuomba na kufundisha neno la Mungu.”
5 Kundi lote la waamini likakubaliana na wazo hili. Hivyo wakawachagua wanaume saba: Stefano (aliyejaa imani na Roho Mtakatifu), Filipo,[a] Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena, na Nikolasi (mtu wa Antiokia aliyeongoka na kufuata dini ya Kiyahudi). 6 Kisha, wakawaweka watu hawa mbele ya mitume, nao mitume waliwaombea na kuweka mikono juu yao.
7 Neno la Mungu lilikuwa linawafikia watu wengi zaidi. Kundi la wafuasi katika Yerusalemu likawa kubwa sana. Hata idadi kubwa ya makuhani wa Kiyahudi waliamini na kutii.
Baadhi ya Wayahudi Wampinga Stefano
8 Mungu alimpa Stefano nguvu ya kutenda maajabu makuu na miujiza katikati ya watu. 9 Lakini baadhi ya Wayahudi pale waliotoka katika sinagogi la Watu Huru,[b] kama lilivyoitwa. Kundi hili lilijumuisha Wayahudi kutoka Kirene, Iskanderia, Kilikia na Asia. Walianza kubishana na Stefano. 10 Lakini Roho Mtakatifu alimwezesha kuzungumza kwa hekima. Maneno yake yalikuwa na nguvu hata Wayahudi hawa hawakuweza kubishana naye.
11 Hivyo wakawaambia baadhi ya watu waseme, “Tumemsikia Stefano akimtukana Musa na Mungu!” 12 Jambo hili liliwakasirisha sana watu, wazee wa Kiyahudi na walimu wa sheria. Wakamkamata Stefano na kumpeleka mbele ya Baraza Kuu.
13 Wayahudi wakawaleta baadhi ya watu kwenye mkutano ili kusema uongo kuhusu Stefano. Watu hawa walisema, “Daima mtu huyu husema maneno kinyume na mahali hapa patakatifu na kinyume na Sheria ya Musa. 14 Tulimsikia akisema kwamba Yesu kutoka Nazareti atapaharibu mahali hapa na kubadilisha yale ambayo Musa aliyotuambia kufanya.” 15 Kila mtu aliyekuwa kwenye mkutano wa baraza alikuwa akimshangaa Stefano kwani uso wake ulionekana kama uso wa malaika.
Hotuba ya Stefano
7 Kuhani mkuu akamwambia Stefano, “Mambo haya ndivyo yalivyo?” 2 Stefano akajibu, “Ndugu zangu na baba zangu Wayahudi, nisikilizeni! Mungu wetu mkuu na mwenye utukufu alimtokea Ibrahimu, baba yetu, alipokuwa Mesopotamia. Kabla hajahamia Harani. 3 Mungu alimwambia, ‘Ondoka katika nchi yako na watu wako, kisha uende katika nchi nitakayokuonesha.’(A)
4 Hivyo Ibrahimu akaondoka katika nchi ya Ukaldayo[c] na kwenda kuishi Harani. Baada ya baba yake kufa, Mungu akamleta katika nchi hii, mahali mnapoishi sasa. 5 Lakini Mungu hakumpa Ibrahimu sehemu yoyote ya ardhi hii, hata eneo dogo lenye ukubwa wa unyayo wake. Lakini Mungu aliahidi kuwa atampa Ibrahimu nchi hii yeye na watoto wake hapo baadaye. Hii ilikuwa kabla Ibrahimu hajapata watoto.
6 Mungu alimwambia: ‘Wazao wako wataishi katika nchi nyingine. Watakuwa wageni. Watu wa huku watawafanya kuwa watumwa na kuwatendea vibaya kwa miaka mia nne. 7 Lakini nitaliadhibu taifa lililowafanya watumwa.’(B) Pia, Mungu alisema, ‘Baada ya mambo hayo kutokea, watu wako watatoka katika nchi hiyo. Kisha wataniabudu mahali hapa.’(C)
8 Mungu aliweka agano na Ibrahimu; alama ya agano hili ilikuwa tohara. Na Ibrahimu alipopata mwana, alimtahiri siku ya nane baada ya kuzaliwa. Jina la mwanaye lilikuwa Isaka. Pia, Isaka alimtahiri mwanaye Yakobo. Na Yakobo alifanya vivyo hivyo kwa wanaye, ambao ndiyo baba wakuu kumi na mbili wa watu wetu.
9 Baba zetu hawa walimwonea wivu Yusufu ndugu yao na wakamwuza ili awe mtumwa Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye, 10 akamwokoa kutoka katika matatizo yake yote. Wakati huo Farao alikuwa mfalme wa Misri. Alimpenda na akamheshimu Yusufu kwa sababu ya hekima ambayo Mungu alimpa. Farao alimfanya Yusufu kuwa gavana wa Misri na msimamizi wa watu wote na kila kitu katika kasri lake. 11 Lakini nchi yote ya Misri na Kanaani zikakosa mvua na mazao ya chakula hayakuweza kuota. Watu waliteseka sana na watu wetu hawakuweza kupata chakula chochote.
12 Lakini Yakobo aliposikia kulikuwa chakula Misri aliwatuma mababa zetu huko. Hii ilikuwa safari yao ya kwanza kwenda Misri. 13 Kisha walikwenda safari ya pili. Safari hii Yusufu akawaeleza ndugu zake yeye ni nani. Ndipo Farao akatambua kuhusu familia ya Yusufu. 14 Kisha Yusufu aliwatuma kaka zake wamwambie Yakobo, baba yake, ahamie Misri. Aliwaalika pia ndugu zake wote, jumla yao wote walikuwa watu sabini na tano. 15 Hivyo Yakobo alitelemka kwenda Misri. Yeye na baba zetu waliishi huko mpaka walipokufa. 16 Baadaye, miili yao ilihamishiwa Shekemu, ambako iliwekwa katika kaburi ambalo Ibrahimu alilinunua kwa fedha kutoka kwa wana wa Hamori.
17 Watu wetu walipokuwa Misri idadi yao iliongezeka. Watu wetu walikuwa wengi mno huko. Ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa Ibrahimu ilikuwa karibu kutimia. 18 Ndipo mfalme mwingine akaanza kutawala Misri, ambaye hakujua lolote kuhusu Yusufu. 19 Mfalme huyu aliwahadaa watu wetu. Akawatendea vibaya sana, akawalazimisha wawaache watoto wao nje ili wafe.
20 Huu ni wakati ambapo Musa alizaliwa. Alikuwa mtoto mzuri sana, na kwa miezi mitatu wazazi wake walimtunza nyumbani. 21 Walipolazimishwa kumtoa nje, Binti wa Farao alimchukua. Alimkuza kama mwanaye wa kumzaa. 22 Musa alielimishwa kwa elimu bora ya Kimisri. Wamisri walimfundisha kila kitu walichojua. Alikuwa mwenye nguvu katika yote aliyosema na kutenda.
23 Musa alipokuwa na umri wa miaka kama arobaini, aliamua kuwatembelea watu wake mwenyewe, watu wa Israeli. 24 Aliona mmoja wao ananyanyaswa na Mmisri, hivyo akamtetea; Musa akampiga na kumwua Mmisri ili kulipiza kwa kumwumiza Mwisraeli. 25 Musa alidhani kwamba watu wake wangeelewa kuwa Mungu alikuwa anamtumia kuwaokoa. Lakini hawakuelewa.
26 Siku iliyofuata, Musa akawaona wawili wa watu wake wakipigana. Alijaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Ninyi ni ndugu! Kwa nini mnataka kuumizana?’ 27 Aliyekuwa akimwumiza mwenzake akamsukuma Musa na akamwambia, ‘Nani amekufanya wewe uwe mtawala na mwamuzi wetu? 28 Unataka kuniua kama ulivyomwua yule Mmisri jana?’(D) 29 Musa alipomsikia akisema hili, alikimbia Misri. Alikwenda kuishi Midiani kama mgeni. Katika kipindi alichoishi huko, alipata wana wawili.
30 Miaka arobaini baadaye, Musa alipokuwa jangwani karibu na Mlima Sinai, malaika alimtokea katika mwali wa moto uliokuwa unawaka katika kichaka. 31 Musa alipoliona hili, alishangaa. Alisogea ili kuangalia kwa karibu. Akasikia sauti; ilikuwa sauti ya Bwana. 32 Bwana alisema, ‘Mimi ni Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zako. Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.’(E) Musa akaanza kutetemeka kwa woga. Aliogopa kukitazama kichaka.
33 Kisha Bwana akamwambia, ‘Vua viatu vyako, kwa sababu mahali uliposimama ni ardhi takatifu. 34 Nimewaona watu wangu wanavyoteseka sana Misri. Nimesikia watu wangu wakilia na nimeshuka ili kuwaokoa. Njoo sasa, Musa, ninakutuma urudi Misri.’(F)
35 Huyu ni Musa ndiye aliyekataliwa na watu wake. Walisema, ‘Nani amekufanya uwe mtawala na mwamuzi wetu?’(G) Lakini ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mtawala na mwokozi. Mungu alimtuma pamoja na msaada wa malaika,[d] ambaye Musa alimwona katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto. 36 Hivyo Musa aliwaongoza watu kutoka Misri. Alitenda maajabu na ishara za miujiza Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani kwa miaka arobaini.
37 Huyu ni Musa yule yule aliyewaambia maneno haya watu wa Israeli: ‘Mungu atakupa nabii. Nabii huyo atakuja kutoka miongoni mwa watu wako mwenyewe. Atakuwa kama mimi.’(H) 38 Musa huyo huyo alikuwa pamoja na kusanyiko la watu wa Mungu jangwani. Alikuwa na malaika aliyezungumza naye alipokuwa Mlima Sinai, na alikuwa pamoja na baba zetu. Alipokea maneno yaletayo uzima kutoka kwa Mungu, na Musa akatupa sisi Maneno hayo.
39 Lakini baba zetu hawakutaka kumtii Musa. Walimkataa, wakataka kurudi Misri. 40 Walimwambia Haruni, ‘Musa alituongoza kutoka katika nchi ya Misri. Lakini hatujui kilichompata. Hivyo tengeneza miungu ili iwe mbele yetu ituongoze.’(I) 41 Hivyo watu wakatengeneza kinyago kinachofanana na ndama. Kisha wakakitolea sadaka za kuteketezwa. Walifurahia kile walichotengeneza kwa mikono yao wenyewe. 42 Lakini Mungu akawaacha, nao wakaendelea kuabudu nyota na sayari.[e] Kitabu cha manabii[f] kinasema hivi:
‘Watu wa Israeli, hamkunipa dhabihu
jangwani kwa miaka arobaini.
43 Mlibeba hema kwa ajili ya kumwabudia Moleki,
na sanamu ya nyota ya mungu wenu Refani.
Hizi zilikuwa sanamu mlizotengeneza ili mziabudu.
Hivyo nitawahamishia mbali, kuvuka Babeli.’(J)
44 Baba zetu walikuwa na Hema Takatifu walipokuwa jangwani. Mungu alimwelekeza Musa jinsi ya kutengeneza hema hii. Aliitengeneza kwa kufuata ramani aliyoonyeshwa na Mungu. 45 Baadaye, Yoshua aliwaongoza baba zetu kuteka ardhi ya mataifa mengine. Watu wetu waliingia, na Mungu akawafukuza watu wengine. Watu wetu walipoingia katika ardhi hii mpya, waliibeba hema hii pamoja nao. Watu wetu waliipata hema hii kutoka kwa baba zao, na watu wetu waliitunza mpaka wakati wa Daudi. 46 Mungu alimpenda Daudi.[g] Na Daudi akamwomba Mungu amruhusu ajenge Hekalu kwa ajili ya watu wa Israeli[h] 47 Lakini Sulemani ndiye aliyemjengea Mungu Hekalu.
48 Lakini Mungu Aliye Juu sana hahitaji yumba zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu ili aishi ndani yake. Nabii aliandika hivi:
49 ‘Bwana asema, Mbingu ni kiti changu cha enzi,
na dunia ni sehemu ya kuweka miguu yangu.
Hivyo mnadhani mnaweza kunijengea nyumba?
Je, ninahitaji mahali pa kupumzika?
50 Kumbukeni, niliumba vitu vyote hivi?’”(K)
51 Kisha Stefano akasema, “Enyi viongozi wa Kiyahudi mlio wakaidi! Mnakataa kumpa Mungu mioyo yenu na mnakataa hata kumsikiliza. Daima mko kinyume na Roho Mtakatifu. Baba zenu walikuwa vivyo hivyo, nanyi mko kama wao! 52 Walimtesa kila nabii aliyewahi kuishi. Waliwaua hata wale ambao zamani zilizopita walisema kwamba Mwenye Haki ilikuwa aje. Na sasa mmekuwa kinyume na Mwenye Haki na mmemwua. 53 Ninyi ndiyo mliipokea Sheria ya Mungu,[i] aliyoitoa kupitia malaika zake. Lakini hamtaki kuitii!”
Stefano Auawa
54 Waliokuwa kwenye mkutano wa baraza waliposikia maneno haya, walikasirika sana na wakamsagia meno Stefano kwa hasira. 55 Lakini Stefano, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alitazama juu mbinguni, na kuuona utukufu wa Mungu. Alimwona Yesu amesimama upande wa kulia wa Mungu. 56 Stefano akasema, “Tazama! Naona mbingu zimefunguka. Na ninamwona Mwana wa Adamu amesimama upande wa kulia wa Mungu.”
57 Kila mmoja pale akaanza kupiga kelele, wakaziba masikio yao kwa mikono yao. Wote kwa pamoja wakamvamia Stefano. 58 Wakamtoa nje ya mji na kuanza kumpiga kwa mawe. Mashahidi walioshuhudia uongo kinyume cha Stefano waliacha makoti yao kwa kijana aliyeitwa Sauli. 59 Walipokuwa wanampiga kwa mawe, Stefano aliomba, akisema, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” 60 Alianguka kwa magoti yake na kupaza sauti, akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii!” Haya yalikuwa maneno yake ya mwisho kabla ya kufa.
8 1-3 Sauli aliridhia kuwa kuuawa kwa Stefano lilikuwa jambo jema. Baadhi ya wacha Mungu walimzika Stefano, wakaomboleza na kumlilia kwa sauti kuu.
Matatizo Kwa waamini
Kuanzia siku hiyo Wayahudi walianza kulitesa sana kanisa na waamini katika mji wa Yerusalemu. Sauli pia alijaribu kuliharibu kanisa. Aliingia katika nyumba za waamini, akawaburuta wanaume na wanawake, na kuwafunga gerezani. Waamini wote walikimbia kutoka Yerusalemu, mitume peke yao ndiyo walibaki. Waamini walikwenda mahali tofauti tofauti katika Uyahudi na Samaria. 4 Walitawanyika kila mahali, na kila walikokwenda waliwahubiri watu Habari Njema.
Filipo Ahubiri Katika Samaria
5 Filipo[j] alikwenda katika mji mkuu wa jimbo la Samaria na kuwahubiri watu kuhusu Masihi. 6 Watu wa Samaria walimsikiliza Filipo na kuona miujiza aliyotenda. Wote walisikiliza kwa makini yale aliyosema. 7 Watu wengi miongoni mwao walikuwa na mapepo, lakini Filipo aliyakemea mapepo na yaliwatoka watu. Mapepo yalipiga kelele nyingi yalipokuwa yanawatoka watu. Walikuwepo pia watu wengi waliopooza na walemavu wa miguu pale. Filipo aliwaombea na wote walipona. 8 Kulikuwa furaha kubwa katika mji ule wa Samaria siku ile!
9 Mtu mmoja aliyeitwa Simoni alikuwa anaishi katika mji huo. Kabla Filipo hajaenda huko, Simoni alikuwa akifanya uchawi na kuwashangaza watu wote wa Samaria. Alijigamba na kujiita mtu mkuu. 10 Watu wote, kuanzia mdogo hadi mkubwa, waliamini yale aliyosema Simoni. Walisema, “Mtu huyu ndiye anayeitwa ‘Nguvu Kuu ya Mungu.’” 11 Simoni aliwashangaza watu kwa muda mrefu kwa uchawi wake na watu wote wakawa wafuasi wake. 12 Lakini Filipo alipowahubiri watu Habari Njema kuhusu Ufalme wa Mungu na Nguvu za Yesu Kristo. Wanaume na wanawake waliamini alichosema Filipo na wakabatizwa. 13 Simoni mwenyewe aliamini, na baada ya kubatizwa, alikaa karibu na Filipo. Alipoona miujiza na matendo makuu ya ajabu yaliyofanyika kupitia Filipo, alishangaa.
14 Mitume mjini Yerusalemu, waliposikia kuwa watu wa Samaria wameupokea Ujumbe wa Mungu, waliwatuma Petro na Yohana kwenda kwa watu wa Samaria. 15 Petro na Yohana walipofika, waliomba ili Roho Mtakatifu awashukie waamini wa Samaria. 16 Watu hawa walikuwa wamebatizwa katika jina la Bwana Yesu, lakini Roho Mtakatifu alikuwa bado hajamshukia hata mmoja wao. Na hii ndiyo sababu Petro na Yohana waliomba. 17 Mitume hawa wawili walipoweka mikono yao juu ya watu, Roho Mtakatifu aliwashukia.
18 Simoni aliyekuwa mchawi alipoona Roho Mtakatifu anatolewa kwa watu kwa kuweka mikono juu yao. Aliwapa pesa mitume. 19 Akasema, “Nipeni na mimi nguvu hii ili nitakapoweka mikono yangu juu ya mtu yeyote, atampata Roho Mtakatifu.”
20 Petro akamwambia Simoni, “Wewe pamoja na pesa zako mwangamie kwa sababu unadhani unaweza kununua karama kutoka kwa Mungu kwa pesa. 21 Huwezi kushirikiana nasi katika kazi hii. Moyo wako si safi mbele za Mungu. 22 Badili moyo wako! Achana na mawazo haya maovu na umwombe Bwana. Yumkini atakusamehe! 23 Kwa kuwa ninaona umejaa wivu mwingi nawe ni mfungwa wa uovu.”
24 Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Bwana, ili haya uliyosema yasinipate.”
25 Ndipo wale mitume wawili waliwaambia watu waliyoona Yesu akitenda. Wakawaambia ujumbe wa Bwana. Kisha wakarudi Yerusalemu. Wakiwa njiani kurudi, walipitia katika miji mingi ya Wasamaria na kuwahubiri watu Habari Njema.
Filipo Amfundisha Mtu Kutoka Ethiopia
26 Malaika wa Bwana alimwambia Filipo, “Jiandae na uende kusini katika barabara ya jangwani inayoteremka kutoka Yerusalemu kwenda Gaza.”
27 Filipo alijiandaa na kwenda. Akiwa njiani alimwona mwanaume kutoka Ethiopia. Alikuwa towashi na ofisa muhimu wa Kandake, malkia wa Ethiopia. Alikuwa na mweka hazina mkuu wa malkia. Mtu huyu alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu. 28 Na alikuwa anarudi Ethiopia. Alikuwa ameketi katika gari lake la kukokotwa na farasi akiwa anasoma kitabu cha nabii Isaya.
29 Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye gari hilo na uwe karibu yake.” 30 Hivyo Filipo akaenda karibu na gari, akamsikia mtu yule akisoma kutoka katika kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamwuliza, “Unaelewa unachosoma?”
31 Yule mtu akajibu, “Nitaelewaje? Ninahitaji mtu wa kunifafanulia.” Ndipo akamwomba Filipo apande garini na aketi pamoja naye. 32 Sehemu ya Maandiko aliyokuwa anasoma ilikuwa hii:
“Alikuwa kama kondoo
anayepelekwa kwa mchinjaji.
Alikuwa kama mwana kondoo asivyopiga kelele
anapokatwa manyoya yake.
Hakusema kitu.
33 Alidhalilishwa,
na kunyimwa haki zake zote.
Maisha yake duniani yamekoma.
Hivyo hakutakuwa simulizi yoyote kuhusu wazaliwa wake.”(L)
34 Afisa[k] akamwambia Filipo, “Tafadhali niambie, nabii anazungumza kuhusu nani? Anazungumza kuhusu yeye mwenyewe au mtu mwingine?” 35 Filipo akaanza kuzungumza. Alianzia na Andiko hili na kumwambia mtu yule Habari Njema kuhusu Yesu.
36 Walipokuwa wanasafiri waliyakuta maji mahali fulani. Afisa akasema, “Tazama! Hapa kuna maji! Nini kinanizuia nisibatizwe?” 37 [l] 38 Ndipo Afisa akaamuru gari lake lisimame. Wote wawili, Filipo na Afisa, wakatelemka wakaingia kwenye maji na Filipo akambatiza towashi. 39 Walipotoka kwenye maji, Roho wa Bwana akamchukua Filipo; afisa hakumwona Filipo tena. Afisa aliendelea na safari yake kurudi nyumbani, akiwa mwenye furaha sana. 40 Lakini Filipo alionekana katika mji ulioitwa Azoto. Alikuwa akienda kwenye mji wa Kaisaria. Aliwahubiri watu Habari Njema katika miji yote wakati anasafiri kutoka Azoto kwenda Kaisaria.
Sauli Awa Mfuasi wa Yesu
9 Huko Yerusalemu Sauli aliendelea kuwatisha wafuasi wa Bwana, na hata kuwaambia kuwa angewaua. Alikwenda kwa kuhani mkuu, 2 na kumwomba aandike barua kwenda kwenye masinagogi yaliyokuwa katika mji wa Dameski. Sauli alitaka kuhani mkuu ampe mamlaka ya kuwatafuta watu katika mji wa Dameski waliokuwa wafuasi wa Njia ya Bwana.[m] Ikiwa angewapata waamini huko, wanaume au wanawake, angewakamata na kuwaleta Yerusalemu.
3 Hivyo Sauli alikwenda Dameski. Alipoukaribia mji, ghafla mwanga mkali kutoka mbinguni ukaangaza kumzunguka. 4 Akadondoka chini na akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli! Kwa nini unanitesa?”
5 Sauli akasema, “Wewe ni nani, Bwana?”
Sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu, unayemtesa. 6 Simama sasa na uingie mjini. Mtu mmoja huko atakueleza unachopaswa kufanya.”
7 Wanaume waliokuwa wanasafiri pamoja na Sauli walisimama pale kimya. Waliisikia sauti, lakini hawakumwona yeyote. 8 Sauli alisimama kutoka chini na kufumbua macho yake, lakini hakuweza kuona. Hivyo wale aliokuwa nao wakamshika mkono na kumwongoza kuingia Dameski. 9 Kwa siku tatu Sauli hakuweza kuona; hakula wala kunywa.
10 Alikuwepo mfuasi wa Yesu katika mji wa Dameski aliyeitwa Anania. Katika maono Bwana alimwita, “Anania!”
Anania alijibu, “Niko hapa, Bwana.”
11 Bwana akamwambia, “Amka na uende katika mtaa unaoitwa Mtaa Ulionyooka. Tafuta nyumba ya Yuda[n] na uliza kuhusu mtu anayeitwa Sauli anayetoka katika mji wa Tarso. Yuko katika nyumba hiyo sasa, anaomba. 12 Ameoneshwa katika maono kuwa mtu anayeitwa Anania anamwendea na kuweka mikono juu yake ili aweze kuona tena.”
13 Lakini Anania akajibu, “Bwana, watu wengi wameniambia kuhusu mtu huyu. Wameniambia kuhusu mambo mengi mabaya aliyowatendea watu wako watakatifu katika mji wa Yerusalemu. 14 Na sasa amekuja hapa Dameski. Viongozi wa makuhani wamempa mamlaka ya kuwakamata watu wote wanaokuamini wewe.”[o]
15 Lakini Bwana Yesu akamwambia Anania, “Nenda, nimemchagua Sauli kwa kazi maalumu. Ninataka ayahubiri mataifa mengine, watawala na watu wa Israeli kuhusu mimi. 16 Nitamwonyesha yote ambayo lazima atateseka kwa ajili yangu.”
17 Hivyo Anania aliondoka na kwenda nyumbani kwa Yuda. Akaweka mikono yake juu ya Sauli na kusema, “Sauli, ndugu yangu, Bwana Yesu amenituma. Ndiye uliyemwona barabarani wakati ukija hapa. Amenituma ili uweze kuona tena, pia ujazwe Roho Mtakatifu.” 18 Ghafla, vitu kama magamba ya samaki vikaanguka kutoka kwenye macho ya Sauli. Akaanza kuona tena! Kisha akasimama na kwenda kubatizwa. 19 Baada ya kula chakula, akaanza kujisikia kuwa na nguvu tena.
Sauli Aanza Kuhubiri Juu ya Yesu Kristo
Sauli alikaa pamoja na wafuasi wa Yesu katika mji wa Dameski kwa siku chache. 20 Baadaye alianza kwenda katika masinagogi na kuwahubiri watu kuhusu Yesu. Aliwaambia watu, “Yesu ni Mwana wa Mungu!”
21 Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa. Wakaulizana, “Je, huyu si yule aliyekuwa anajaribu kuwaangamiza watu wanaomwamini Yesu[p] katika mji wa Yerusalemu? Na hakuja hapa ili awakamate wafuasi wa Yesu na kuwarudisha kwa viongozi wa makuhani?”
22 Lakini Sauli aliendelea kuwa nguvu katika kuthibitisha kwamba Yesu ndiye Masihi. Uthibitisho wake ulikuwa na nguvu kiasi kwamba Wayahudi walioishi Dameski hawakuweza kubishana naye.
Sauli Awatoroka Wayahudi
23 Baada ya siku nyingi kupita, baadhi ya Wayahudi waliweka mpango wa kumwua Sauli. 24 Waliyalinda malango ya mji usiku na mchana. Walitaka kumwua Sauli, lakini aliambiwa kuhusu mpango wao. 25 Usiku mmoja baadhi ya wafuasi ambao Sauli aliwafundisha walimsaidia kuondoka mjini. Walimweka katika kikapu, wakamtoa kwa kumshusha kupitia kwenye tundu lililokuwa kwenye ukuta wa mji.
Sauli Katika Mji wa Yerusalemu
26 Kisha Sauli alikwenda Yerusalemu. Akajaribu kujiunga na kundi la wafuasi, lakini wote walimwogopa. Hawakuamini kuwa naye amekuwa mfuasi wa Yesu. 27 Lakini Barnaba alimkubali Sauli, akamchukua na kumpeleka kwa mitume. Akawaeleza namna ambavyo Sauli alimwona Bwana akiwa njiani na namna ambavyo Bwana aliongea naye. Kisha akawaambia namna ambavyo Sauli amehubiri kwa ujasiri kuhusu Yesu katika mji wa Dameski.
28 Sauli alikaa na wafuasi na kwenda kila mahali katika mji wa Yerusalemu akihubiri kwa ujasiri kwa ajili ya Bwana. 29 Kila mara alibishana na Wayahudi waliokuwa waliozungumza Kiyunani,[q] ambao walianza kutengeneza mpango wa kumwua. 30 Waamini walipoujua mpango huu, walimchukua Sauli mpaka Kaisaria, na kutoka huko walimsafirisha mpaka katika mji wa Tarso.
31 Kanisa katika Uyahudi yote, Galilaya na Samaria likawa na wakati wa amani. Na kwa msaada wa Roho Mtakatifu, vikundi hivi vya waamini vikawa na nguvu katika imani na kuonesha utii kwa ajili ya Bwana kwa namna walivyoishi. Hivyo kanisa kila mahali liliongezeka kwa idadi.
Petro akiwa Lida na Yafa
32 Petro alikuwa akisafiri katika sehemu zote za Uyahudi, Galilaya na Samaria, na akasimama kuwatembelea waamini[r] walioishi Lida. 33 Huko alikutana na mtu aliyeitwa Ainea, ambaye alikuwa amepooza na hakuweza kutoka kitandani kwa miaka nane. 34 Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo amekuponya. Simama na kiweke kitanda chako vizuri!” Ainea alisimama saa ile ile. 35 Watu wote walioishi Lida na tambarare ya Sharoni walimwona, na wakaamua kumfuata Bwana.
36 Katika mji wa Yafa kulikuwa na mfuasi wa Yesu aliyeitwa Tabitha, Jina lake kwa Kiyunani lilikuwa Dorkasi.[s] Daima aliwatendea watu mambo mema na kuwapa pesa wale wenye mahitaji. 37 Petro alipokuwa Lida, Tabitha aliugua na kufa. Waliusafisha mwili wake na kuuweka chumbani ghorofani. 38 Wafuasi waliokuwa Yafa wakasikia kuwa Petro yuko Lida, mji ambao haukuwa mbali na Yafa. Hivyo waliwatuma watu wawili, waliomsihi Petro wakisema, “Tafadhali njoo kwetu haraka!”
39 Petro alijiandaa na kwenda pamoja nao. Alipofika, walimchukua na kumpeleka kwenye chumba ghorofani. Wajane wote walisimama wakamzunguka huku wakilia na wakamwonesha mavazi ambayo Tabitha alitengeneza alipokuwa hai. 40 Petro akawatoa watu wote chumbani. Akapiga magoti na kuomba. Kisha akaugeukia mwili wa Tabitha na kusema, “Tabitha! Simama.” Akafumbua macho yake. Alipomwona Petro akaketi. 41 Petro akamshika mkono na akamsaidia kusimama. Ndipo akawaita waamini na wajane chumbani. Akawaonyesha Tabitha; akiwa hai!
42 Watu kila mahali katika mji wa Yafa wakatambua kuhusu hili, na wengi wakamwamini Bwana. 43 Petro alikaa Yafa siku nyingi nyumbani kwa mtu mmoja aitwaye Simoni, aliyekuwa mtengenezaji wa ngozi.
Petro na Kornelio
10 Kulikuwa mtu aliyeitwa Kornelio katika mji wa Kaisaria. Mtu huyu alikuwa ofisa wa kikosi kilichoitwa “Kikosi cha Kiitalia” katika jeshi la Rumi. 2 Alikuwa mcha Mungu. Yeye na watu wengine wote walioishi katika nyumba yake walikuwa wanamwabudu Mungu wa kweli. Alitoa pesa zake nyingi kuwasaidia maskini miongoni mwa Wayahudi na daima alimwomba Mungu kwa kufuata utaratibu kama ilivyokuwa. 3 Mchana mmoja yapata saa tisa, kwa uwazi na dhahiri Kornelio aliona maono. Alimwona malaika kutoka kwa Mungu akimwendea na akamwambia, “Kornelio!”
4 Akiwa anashangaa na kuogopa, Kornelio akasema, “Unataka nini, bwana?”
Malaika akamwambia, “Mungu amesikia maombi yako na ameona sadaka zako unazowapa maskini. Anakukumbuka kwa yote uliyotenda. 5 Tuma baadhi ya watu sasa waende katika mji wa Yafa wakamlete mtu anayeitwa Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. 6 Anakaa kwa mtu ambaye naye pia anaitwa Simoni, mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko kwenye ufukwe wa bahari.” 7 Malaika aliyeongea na Kornelio akaondoka. Ndipo Kornelio aliita watumishi wake wawili na askari mmoja. Askari alikuwa mcha Mungu, mmoja wa wasaidizi wake wa karibu. 8 Kornelio akawaelekeza kila kitu watu hawa watatu kisha akawatuma kwenda Yafa.
9 Siku iliyofuata wakati wa adhuhuri walipokuwa wanaukaribia mji wa Yafa, Petro alipanda juu ya paa[t] kuomba. 10 Alihisi njaa na akataka chakula. Lakini walipokuwa wanamwandalia chakula ili ale, aliona maono. 11 Aliona mbingu zikifunguka na kitu kama shuka kubwa kikishushwa chini kutoka mbinguni kwa pembe nne. 12 Ndani yake mlikuwa aina zote za wanyama, watambaao na ndege. 13 Kisha sauti ikamwambia, “Petro simama uchinje chochote hapa kisha ule.”
14 Lakini Petro akasema, “Siwezi kufanya hivyo, Bwana! Sijawahi kula kitu chochote kisicho safi au kisicho stahili kutumiwa kwa chakula.”
15 Lakini sauti ikamwambia tena, “Mungu amekwisha vitakasa vitu vyote hivi. Usiseme havistahili kuliwa.” 16 Hili lilimtokea mara tatu. Kisha likachukuliwa mbinguni. 17 Petro alijiuliza maono haya yalikuwa na maana gani.
Watu ambao Kornelio aliwatuma walishaiona nyumba ya Simoni na walikuwa wamesimama mlangoni. 18 Waliuliza, “Je, Simoni Petro yuko hapa?”
19 Petro akiwa bado anafikiri kuhusu maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Sikiliza, kuna watu watatu wanakutafuta. 20 Inuka na ushuke chini. Nenda nao, usisite, kwa sababu nimewatuma.” 21 Hivyo Petro akashuka chini na kuwaambia, “Nafikiri mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja hapa?”
22 Wale watu wakasema, “Malaika mtakatifu amemwambia Kornelio akualike nyumbani mwake. Ni mtu mwema na hutenda kwa haki, na anamwabudu Mungu na Wayahudi wote wanamheshimu. Malaika alimwambia akualike nyumbani kwake ili asikilize yale utakayosema.” 23 Petro akawakaribisha ndani watu wale ili walale usiku huo.
Siku iliyofuata Petro alijiandaa na kuondoka na wale watu watatu. Baadhi ya waamini katika mji wa Yafa walikwenda pamoja naye. 24 Siku iliyofuata walifika katika mji wa Kaisaria. Kornelio alikuwa anawasubiri na alikuwa amewakusanya jamaa na rafiki zake wa karibu nyumbani mwake.
25 Petro alipoingia ndani ya nyumba, Kornelio alimlaki kisha akaanguka miguuni kwa Petro na akamwabudu. 26 Lakini Petro akamwambia asimame. Petro akasema, “Simama! Mimi ni mtu tu kama wewe.” 27 Petro aliendelea kuzungumza na Kornelio. Ndipo Petro akaingia ndani na kuona kundi kubwa la watu wamekusanyika pale.
28 Petro akawaambia watu wale kuwa, “Mnaelewa kuwa ni kinyume na sheria yetu kwa Myahudi kushirikiana au kumtembelea mtu ambaye si Myahudi. Lakini Mungu amenionyesha kuwa nisimchukulie mtu yeyote kuwa yu kinyume na desturi za Kiyahudi. 29 Ndiyo sababu sikubisha watu wenu waliponiambia kuja hapa. Sasa, tafadhali niambieni kwa nini mmeniita hapa.”
30 Kornelio akasema, “Siku nne zilizopita, kama saa tisa mchana nilikuwa ninaomba ndani ya nyumba yangu. Ghafla akawepo mtu mmoja amesimama mbele yangu amevaa mavazi meupe yanayong'aa. 31 Akasema, ‘Kornelio, Mungu amesikia maombi yako na ameona sadaka zako kwa maskini. Anakukumbuka wewe na yote uliyofanya. 32 Hivyo tuma baadhi ya watu kwenye mji wa Yafa na wamwambie Simoni Petro kuja. Anakaa na mtu mwingine anayeitwa Simoni, mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko pembeni mwa bahari.’ 33 Hivyo nikawatuma kwako haraka. Imekuwa vizuri sana umekuja hapa. Sasa sote tupo hapa mbele za Mungu na tuko tayari kusikia kila kitu ambacho Bwana amekwamuru utuambie.”
Petro Ahubiri Katika nyumba ya Kornelio
34 Petro akaanza kwa kusema: “Hakika sasa ninaelewa ni kwa nini Mungu hawachukulii kundi fulani la watu kuwa bora kuliko wengine. 35 Anamkubali yeyote anayemwabudu na anayetenda haki. Haijalishi wanatoka katika taifa lipi. 36 Mungu amezungumza na watu wa Israeli. Aliwaletea Habari Njema kwamba amani imekuja kupitia Yesu Kristo ambaye ndiye Bwana wa watu wote.
37 Mnafahanu kilichotokea katika Uyahudi yote. Kilianzia Galilaya baada ya Yohana kuwaambia watu kuwa inawapasa kubatizwa. 38 Mnajua kuhusu Yesu kutoka Nazareti. Mungu alimfanya Masihi kwa kumpa Roho Mtakatifu na nguvu. Yesu alikwenda kila mahali akiwatendea mema watu. Akawaponya wale waliokuwa wakitawaliwa na yule Mwovu, akionyesha kuwa Mungu alikuwa pamoja naye.
39 Tuliona yote ambayo Yesu alitenda katika Uyahudi na katika mji wa Yerusalemu. Lakini aliuawa. Walimpigilia kwenye msalaba uliotengenezwa kwa mti. 40 Lakini siku ya tatu baada ya kifo chake, Mungu alimfufua na kumfanya aonekane wazi wazi. 41 Hakuonekana kwa Wayahudi wote, lakini alionekana kwetu sisi tu, ambao Mungu tayari alikwisha kutuchagua tuwe mashahidi. Tulikula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu.
42 Yesu alitwambia twende na kuwaeleza watu. Alituagiza tuwaeleza kwamba yeye ndiye ambaye Mungu amemchagua kuwa mwamuzi wa wote walio hai na wote walio kufa. 43 Na ya kwamba kila atakayemwamini Yesu, atasamehewa dhambi zake kupitia nguvu jina Lake. Manabii wote wanakubali kuwa jambo hili ni la kweli.”
Roho Mtakatifu Awashukia Watu Wasio Wayahudi
44 Petro alipokuwa bado anazungumza, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wanamsikiliza. 45 Waamini wa Kiyahudi waliofuatana na Petro walishangaa kwamba Roho Mtakatifu amemiminwa kama zawadi hata kwa watu wasio Wayahudi. 46 Waliwasikia wakiongea lugha mbalimbali na kumsifu Mungu. Ndipo Petro akasema, 47 “Je, mtu yeyote anawezaje kuzuia watu hawa wasibatizwe katika maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea!” 48 Hivyo Petro akawaambia wambatize Kornelio pamoja na jamaa zake na rafiki zake katika jina la Yesu Kristo. Kisha wakamwomba Petro akae nao kwa siku chache.
Petro Arudi Yerusalemu
11 Mitume na waamini katika Uyahudi walisikia kwamba watu wasio Wayahudi wameyapokea mafundisho ya Mungu pia. 2 Lakini Petro alipokuja Yerusalemu, baadhi ya waamini wa Kiyahudi[u] walimkosoa. 3 Walisema, “Uliingia katika nyumba za watu wasio Wayahudi ambao hawajatahiriwa na ukala pamoja nao!”
4 Hivyo Petro akawaelezea namna ilivyotokea. 5 Akasema, “Nilikuwa katika mji wa Yafa. Nilipokuwa nikiomba, niliona maono. Niliona kitu kikishuka chini kutoka mbinguni. Kilionekana kama shuka kubwa ikishushwa chini kwa pembe zake nne. Kikaja chini karibu yangu. 6 Nilipotazama ndani yake, niliona aina zote za wanyama, pamoja na wale wa porini, wanyama wanaotambaa na ndege. 7 Nilisikia sauti ikiniambia. Chinja chochote hapa na ule!”
8 “Lakini nilisema, ‘Siwezi kufanya hivyo Bwana! Sijawahi kula kitu cho chote kisicho safi au kisichostahili kuliwa kama chakula.’
9 Lakini sauti kutoka mbinguni ikajibu tena, ‘Mungu amevitakasa vitu hivi. Usiseme havistahili kuliwa!’
10 Hili lilitokea mara tatu. Ndipo kitu chote kikachukuliwa kurudi mbinguni. 11 Saa hiyo hiyo baada ya hayo wakawepo watu watatu wamesimama nje ya nyumba nilimokuwa ninakaa. Walikuwa wametumwa kutoka Kaisaria kunichukua. 12 Roho Mtakatifu aliniambia niende nao bila kuwa na mashaka. Ndugu hawa hapa sita walikwenda pamoja nami, na tulikwenda katika nyumba ya Kornelio. 13 Alitwambia kuhusu malaika aliyemwona amesimama katika nyumba yake. Malaika alimwambia, ‘Tuma baadhi ya watu waenda Yafa kumchukua Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. 14 Atazungumza na wewe. Ujumbe atakaokwambia utakuokoa wewe na kila mtu anayeishi katika nyumba yako.’
15 Nilipoanza kuzungumza, Roho Mtakatifu alikuja juu yao kama vile alivyokuja juu yetu mwanzo.[v] 16 Ndipo nilikumbuka maneno ya Bwana Yesu, aliyosema: ‘Yohana alibatiza katika maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ 17 Mungu amewapa watu hawa karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo. Hivyo ningewezaje kupinga yale ambayo Mungu alitaka kufanya?”
18 Waamini wa Kiyahudi waliposikia hili, wakaacha kubisha. Wakamsifu Mungu na kusema, “Kwa hiyo Mungu anawaruhusu watu wasio Wayahudi kubadili mioyo yao na kuwa na maisha anayotoa!”
Habari Njema Zafika Antiokia
19 Waamini walitawanyika kwa sababu ya mateso[w] yaliyoanza baada ya Stefano kuuawa. Baadhi ya waamini walikwenda mbali mpaka Foeniki, Kipro na Antiokia. Walihubiri Habari Njema katika maeneo haya, lakini kwa Wayahudi tu. 20 Baadhi ya waamini hawa walikuwa watu kutoka Kipro na Kirene. Watu hawa walipofika Antiokia, walianza kuwahubiri watu wasio Wayahudi.[x] Waliwahubiri Habari Njema kuhusu Bwana Yesu. 21 Nguvu ya Bwana iliambatana na watu hawa, na idadi kubwa ya watu waliamini na kuamua kumfuata Bwana.
22 Kanisa katika mji wa Yerusalemu liliposikia kuhusu hili, lilimtuma Barnaba kwenda Antiokia. 23-24 Barnaba alikuwa mtu mwema, aliyejaa Roho Mtakatifu na imani. Alipokwenda Antiokia na kuona jinsi Mungu alivyowabariki waamini pale, alifurahi sana. Akawatia moyo wote, akasema, “Iweni waaminifu kwa Bwana daima. Mtumikieni Yeye kwa mioyo yenu yote.” Watu wengi zaidi wakawa wafuasi wa Bwana.
25 Kisha Barnaba alikwenda katika mji wa Tarso kumtafuta Sauli. 26 Alipompata, alimpeleka Antiokia. Walikaa pale mwaka mzima. Kila wakati kanisa lilipokusanyika, Barnaba na Sauli walikutana nao na kuwafundisha watu wengi. Ni katika mji wa Antiokia ambako wafuasi wa Bwana Yesu walianza kuitwa “Wafuasi wa Kristo”.[y]
27 Katika wakati huo huo baadhi ya manabii walitoka Yerusalemu na kwenda Antiokia. 28 Mmoja wao, aliyeitwa Agabo, huku akisaidiwa na Roho Mtakatifu, alisimama na kuzungumza. Alisema, “Wakati mbaya sana unakuja katika dunia yote. Hakutakuwa chakula kwa ajili ya watu kula.” (Kipindi hiki cha njaa kilitokea Klaudio alipokuwa mtawala wa Kirumi) 29 Wafuasi wa Bwana wakaamua kwamba kila mmoja wao atatuma kiasi anachoweza kuwasaidia ndugu wote[z] wanaoishi Uyahudi. 30 Walikusanya pesa na kuwapa Barnaba na Sauli, waliozipeleka kwa wazee, katika Uyahudi.
Matatizo Mengi kwa waamini
12 Katika wakati huu huu, Mfalme Herode akaanza kuwatesa baadhi ya waamini waliokuwa sehemu ya kanisa. 2 Aliamuru Yakobo aliyekuwa kaka yake Yohana, auawe kwa upanga. 3 Herode alipoona kuwa Wayahudi wamelifurahia jambo hili, aliamua kumkamata Petro pia. Hii lilitokea katika kipindi cha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. 4 Alimkamata Petro na kumfunga gerezani, ambako alilindwa na kundi la askari kumi na sita.[aa] Herode alipanga kumleta Petro mbele ya watu ili ahukumiwe, lakini alisubiri mpaka baada ya sikukuu ya Pasaka. 5 Hivyo Petro aliwekwa gerezani lakini kanisa lilikuwa likiomba kwa Mungu bila kuacha kwa ajili yake.
Petro Atolewa Nje ya Gereza
6 Wakati wa usiku kabla ya siku ambayo Herode alipanga kumhukumu mbele ya watu, Petro, akiwa amefungwa minyororo miwili, alikuwa amelala katikati ya askari wawili. Na askari waliokuwa nje ya mlango walikuwa wanalinda gereza. 7 Ghafla malaika wa Bwana alikuwa amesimama pale, na chumba kilijaa mwanga. Malaika akamwamsha Petro kwa kumpiga upande, akasema, “Amka haraka!” Minyororo ikaanguka kutoka mikono mwa Petro. 8 Malaika akasema, “Vaa nguo na viatu vyako.” Petro alifanya kama alivyoambiwa. Kisha malaika akasema, “Vaa koti lako na unifuate.”
9 Hivyo malaika akatoka nje na Petro alimfuata. Hakujua kama kweli malaika alikuwa anafanya hili. Alidhani alikuwa anaona maono. 10 Petro na malaika wakavuka lindo la kwanza na lindo la pili. Kisha walifika kwenye lango la chuma lililowatenganisha na mji. Lango likafunguka. Baada ya kuvuka lango na kutembea umbali wa kama mtaa mmoja, malaika akatoweka ghafla.
11 Ndipo Petro akatambua kuwa haikuwa ndoto. Akawaza moyoni akisema, “Sasa ninajua kwamba Bwana hakika alimtuma malaika wake kwangu. Ameniokoa kutoka kwa Herode na kutoka kwenye mabaya yote ambayo Wayahudi walidhani yatanipata.”
12 Petro alipotambua hili, alikwenda nyumbani kwa Mariamu, mama yake Yohana, aliyeitwa Marko. Watu wengi walikuwa wamekusanyika pale wakiomba. 13 Petro alibisha kwenye mlango wa nje. Mtumishi wa kike aliyeitwa Rhoda alikuja ili afungue mlango. 14 Alipoitambua sauti ya Petro, alifurahi sana hata akasahau kufungua mlango. Akakimbilia ndani na kuliambia kundi, “Petro yuko mlangoni!” 15 Waamini wakamwambia, “Wewe una kichaa!” Lakini alipoendelea kusema kwamba ni kweli Petro yuko mlangoni. Waamini walisema, “Lazima atakuwa malaika wa Petro.”
16 Lakini Petro aliendelea kubisha mlangoni. Waamini walipoufungua mlango na kumwona, wakashangaa. 17 Petro akawafanyia ishara kwa mkono wake kuwaambia wanyamaze. Akawaeleza namna Bwana alivyomtoa nje ya gereza. Akasema, “Mwambieni Yakobo na ndugu wengine kilichotokea.” Kisha akawaacha na kwenda sehemu nyingine.
18 Siku iliyofuata askari walichanganyikiwa. Walijiuliza nini kimempata Petro. 19 Herode alimtafuta kila mahali lakini hakumpata. Hivyo aliwahoji walinzi na kuamuru wauawe.
Kifo cha Herode Agripa
Baadaye, Herode alihama kutoka Uyahudi na kwenda katika mji wa Kaisaria na kukaa huko kwa muda. 20 Herode aliwakasirikia sana watu katika miji ya Tiro na Sidoni. Lakini miji hii ilihitaji chakula kutoka katika nchi yake, hivyo baadhi yao walimjia wakitaka amani naye. Waliweza kumshawishi Blasto mtumishi binafsi wa Mfalme ili awasaidie.
21 Herode alichagua siku maalumu ya kukutana nao. Siku hiyo alivaa vazi zuri la kifalme. Aliketi kwenye kiti chake cha enzi na kuwahutubia watu. 22 Watu wakapaza sauti zao na kusema, “Hii ni sauti ya mungu, siyo mwanadamu!” 23 Herode hakumpa Mungu utukufu. Hivyo malaika wa bwana akampiga kwa ugonjwa. Akaliwa na minyoo ndani na kufa.
24 Ujumbe wa Mungu ulikuwa unasambaa, ukiwafikia watu wengi zaidi.
25 Baada ya Barnaba na Sauli kumaliza kazi yao Yerusalemu, walirudi Antiokia, walimchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao.
Barnaba na Sauli Wapewa Kazi Maalum
13 Walikuwepo baadhi ya manabii na walimu katika kanisa la Antiokia. Walikuwa Barnaba, Simeoni (ambaye pia aliitwa Nigeri[ab]), Lukio (kutoka mji wa Kirene), Manaeni (aliyekua pamoja na Mfalme Herode[ac]), na Sauli. 2 Watu hawa wote kwa pamoja walikuwa wanamwabudu Bwana na wamefunga Roho Mtakatifu alipowaambia, “Nitengeeni Barnaba na Sauli ili wanifanyie kazi maalumu. Wao ndio niliowachagua kuifanya kazi hiyo.”
3 Hivyo kanisa lilifunga na kuomba. Wakaweka mikono yao juu ya Barnaba na Sauli, wakaagana nao na kuwaacha waende.
Barnaba na Sauli Wakiwa Kipro
4 Barnaba na Sauli walitumwa na Roho Mtakatifu. Walikwenda katika mji wa Seleukia. Kutoka hapo walitweka tanga na kusafiri mpaka kwenye kisiwa cha Kipro. 5 Barnaba na Sauli walipofika kwenye mji wa Salami, walihubiri ujumbe wa Mungu katika masinagogi ya Kiyahudi. Yohana ambaye pia anaitwa Marko alikuwa pamoja nao ili kuwasaidia.
6 Walisafiri wakitisha kisiwa chote mpaka kwenye mji wa Pafo. Huko walimkuta mwanaume wa Kiyahudi aliyeitwa Bar-Yesu aliyekuwa akifanya uchawi. Alikuwa nabii wa uongo. 7 Alikaa daima karibu na Sergio Paulo, aliyekuwa gavana na mtu makini sana. Sergio Paulo aliwaalika Barnaba na Sauli waende kumtembelea kwa sababu alitaka kusikia ujumbe wa Mungu. 8 Lakini mchawi Elima (Bar-Yesu kama alivyoitwa kwa Kiyunani) alizungumza kinyume nao ili kuwapinga, akijaribu kumzuia gavana asimwamini Yesu. 9 Kisha Sauli (ambaye pia anajulikana kama Paulo), akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alimkazia macho Elima 10 na kusema, “Ewe mwana wa Ibilisi, uliyejaa uongo na aina zote za hila za uovu! Wewe ni adui wa kila kilicho cha kweli. Hautaacha kuzibadili kweli za Bwana kuwa uongo? 11 Sasa Bwana atakugusa na utakuwa asiyeona. Hautaweza kuona kitu chochote kwa muda, hata mwanga wa jua.”
Ndipo kila kitu kikawa giza kwa Elima. Akazunguka kila mahali na akapotea. Alikwenda kila mahali akijaribu kumpata mtu wa kumshika mkono ili amwongoze. 12 Gavana alipoyaona haya, akaamini. Akayashangaa mafundisho kuhusu Bwana.
Paulo na Barnaba Waenda Antiokia ya Pisidia
13 Paulo na watu waliokuwa pamoja naye walitweka tanga na kusafiri kwa merikebu kutoka Pafo mpaka Perge, mji uliokuwa Pamfilia. Hapo Yohana Marko aliwaacha na akarudi Yerusalemu. 14 Waliendelea na safari yao kutoka Perge na kwenda Antiokia, mji karibu na Pisidia.
Siku ya Sabato walikwenda katika sinagogi la Kiyahudi na kuketi chini. 15 Sheria ya Musa na maandishi ya manabii vilisomwa. Kisha viongozi wa sinagogi wakawatumia ujumbe Paulo na Barnaba, wakisema, “Ndugu zetu, ikiwa mna kitu chochote cha kusema kitakachowasaidia watu hapa, tafadhali semeni.”
16 Paulo akasimama, akanyoosha mkono wake ili wamsikilize, akasema, “Watu wa Israeli nanyi nyote msio Wayahudi mnaomwabudu Mungu wa kweli, tafadhali nisikilizeni! 17 Mungu wa Israeli aliwachagua baba zetu. Na watu wetu walipoishi Misri kama wageni, aliwafanya wakuu. Kisha akawatoa katika nchi ile kwa nguvu kuu. 18 Aliwavumilia kwa miaka arobaini walipokuwa jangwani. 19 Mungu aliangamiza mataifa saba katika nchi ya Kanaani na kuwapa nchi yao watu wake. 20 Yote haya yalitokea katika kipindi cha kadiri ya miaka mia nne na hamsini.[ad]
Baada ya hili, Mungu akawapa watu wetu waamuzi kuwaongoza mpaka wakati wa nabii Samweli. 21 Ndipo watu wakaomba kuwa na mfalme. Mungu akawapa Sauli, mwana wa Kishi. Sauli alitoka katika kabila la Benjamini. Alikuwa mfalme kwa miaka arobaini. 22 Baada ya Mungu kumwondoa Sauli katika ufalme, Mungu alimfanya Daudi kuwa Mfalme wao. Hiki ndicho Mungu alisema kuhusu Daudi: ‘Daudi, mwana wa Yese, ni mtu ambaye Mimi mwenyewe nimemchagua. Atafanya kila kitu nitakachotaka afanye.’
23 Kama alivyoahidi, Mungu amemleta mmoja wa wazao wa Daudi katika Israeli ili awe Mwokozi wao, mzao huyo wa Daudi ni Yesu. 24 Kabla Yesu hajaja, Yohana aliwaambia watu wote wa Israeli wanachopaswa kufanya. Waliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa walitaka kubadili maisha yao. 25 Yohana alipokuwa anamaliza kazi yake, alisema, ‘Mnadhani mimi ni nani? Mimi siyo Masihi.[ae] Masihi atakuja baadaye, nami sistahili kuwa mtumwa wake wa kufungua kamba za viatu vyake.’
26 Ndugu zangu, wana katika familia ya Ibrahimu na ninyi watu wengine ambao pia mnamwabudu Mungu wa kweli, sikilizeni! Habari kuhusu wokovu huu imeletwa kwetu. 27 Wayahudi waishio Yerusalemu na viongozi wao hawakutambua kuwa Yesu ni Mwokozi. Maneno ambayo manabii waliandika kuhusu yeye yalikuwa yakisomwa kila siku ya Sabato, lakini hawakuyaelewa. Walimhukumu Yesu. Walipofanya hivi, waliyatimiliza maneno ya manabii. 28 Hawakupata sababu ya msingi kwa nini Yesu afe, lakini walimwomba Pilato amwue.
29 Wayahudi hawa walimtendea Yesu mambo yote mabaya ambayo Maandiko yalisema yangempata Yesu. Kisha walimteremsha Yesu kutoka msalabani na kumweka kaburini. 30 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu! 31 Baada ya hili, kwa siku nyingi, wale waliofuatana na Yesu kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu walimwona. Wao sasa ni mashahidi wake kwa watu wetu.
32 Tunawahubiri Habari Njema kuhusu ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa baba zetu. 33 Sisi ni wazao wao, na Mungu ameitimiza ahadi hii kwa ajili yetu. Mungu aliitimiza ahadi hii kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Tunasoma pia kuhusu hili katika Zaburi 2:
‘Wewe ni Mwanangu.
Leo nimekuwa baba yako.’(M)
34 Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. Yesu hatarudi kaburini na kuwa mavumbi. Hivyo Mungu alisema,
‘Nitawapa ahadi ya kuaminiwa na
takatifu niliyoiahidi kwa Daudi.’(N)
35 Lakini Zaburi nyingine inasema,
‘Hautaruhusu Mtakatifu wako aoze kaburini.’(O)
36 Daudi aliyatenda mapenzi ya Mungu alipokuwa hai. Kisha alikufa na kuzikwa kama baba zake wote. Na mwili wake ulioza kaburini! 37 Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu hakuoza kaburini. 38-39 Ndugu zangu, eleweni yale tunayowaambia. Mnaweza kupata msamaha wa dhambi kupitia huyu Yesu. Sheria ya Musa haikuwatoa kutoka katika dhambi zenu. Lakini mnaweza kuwa huru mbali na hukumu. 40 Hivyo iweni waangalifu! Msiruhusu walichosema manabii kikawatokea ninyi:
41 ‘Sikilizeni enyi watu wenye mashaka!
Mnaweza kushangaa,
lakini sasa nendeni na mfe.
Kwa sababu kipindi cha wakati wenu,
nitafanya kitu ambacho hamtaamini.
Hata kama kitafafanuliwa kwenu!’”(P)
42 Paulo na Barnaba walipokuwa wanaondoka kwenye sinagogi, watu waliwaomba warudi tena Sabato inayofuata ili wawaeleze zaidi kuhusu mambo haya. 43 Baada ya mkutano, watu wengi, Wayahudi na wale waliobadili dini zao na kufuata dini ya Kiyahudi, waliwafuata Paulo na Barnaba; nao waliwatia moyo watu hawa waendelee kuitumaini neema ya Mungu.
44 Siku ya Sabato iliyofuata, karibu watu wote katika mji walikusanyika ili wasikie neno la Bwana. 45 Wayahudi waliokuwepo pale walipowaona watu wote hawa, wakaingiwa na wivu sana. Wakakashifu na kubishia kila kitu alichosema Paulo. 46 Lakini Paulo na Barnaba walihubiri kwa ujasiri. Walisema, “Tulikuwa tuuhubiri ujumbe wa Mungu kwenu ninyi Wayahudi kwanza, lakini mmekataa kusikiliza. Mmeweka wazi kuwa hamstahili kuupata uzima wa milele. Hivyo tutakwenda sasa kwa wale wasio Wayahudi. 47 Hivi ndivyo Bwana alivyotuambia kufanya:
‘Nimewafanya ninyi mwanga kwa ajili ya mataifa mengine,
kuwaonesha watu ulimwenguni kote njia ya wokovu.’”(Q)
48 Wasio Wayahudi waliposikia Paulo akisema hivi, walifurahi sana. Waliuheshimu ujumbe wa Bwana, na wengi wao wakauamini. Hawa ni wale waliochaguliwa kuupata uzima wa milele.
49 Na hivyo ujumbe wa Bwana ulihubiriwa katika nchi yote. 50 Lakini Wayahudi pale walisababisha baadhi ya wanawake muhimu waifuatayo dini na viongozi wa mji kuwakasirikia na kuwachukia Paulo na Barnaba na wakawafukuza mjini. 51 Hivyo Paulo na Barnaba wakakung'uta mavumbi ya miguu yao.[af] Kisha wakaenda katika mji wa Ikonia. 52 Lakini wafuasi wa Bwana katika Antiokia walijaa furaha na walijazwa Roho Mtakatifu.
Footnotes
- 6:5 Filipo Siyo mtume aliyeitwa Filipo.
- 6:9 Watu Huru Wayahudi waliokuwa watumwa au ambao baba zao walikuwa watumwa, lakini wao walikuwa huru.
- 7:4 Ukaldayo Au “Babeli”, nchi iliyo kusini mwa Mesopotamia. Tazama mstari wa 2.
- 7:35 Hapa inamaanisha kuwa Musa aliambatana na nguvu za Mungu na ulinzi wa malaika.
- 7:42 nyota na sayari Ama jeshi lililoko angani. Nyakati za kale watu waliamini kuwa nyota na sayari zilikuwa miungu au malaika.
- 7:42 Kitabu cha manabii Hiki ni kitabu cha manabii wadogo kumi na mbili: Kuanzia Hosea mpaka Malaki.
- 7:46 Mungu alimpenda Daudi Au “alipendelewa na Mungu”.
- 7:46 watu wa Israeli Kwa maana ya kawaida, “nyumba ya Yakobo”. Nakala zingine za Kiyunani zina “Mungu wa Yakobo”.
- 7:53 Sheria ya Mungu Yaani Torati.
- 8:5 Filipo Siyo mtume aliyeitwa Filipo.
- 8:34 Afisa Kwa maana ya kawaida, “towashi”. Pia katika mstari wa 36,38,39.
- 8:37 Nakala zingine za baadaye za Matendo zimeongeza mstari wa 37: Filipo akajibu, “Ikiwa unaamini kwa moyo wako wote unaweza kubatizwa. Ofisa akasema, ‘Ninaamini kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu.’”
- 9:2 Njia ya Bwana Ni maneno yaliyotumika ili kuainisha tabia na mafundisho ya Yesu.
- 9:11 Yuda Huyu si mmoja wa mitume aliyeitwa Yuda.
- 9:14 wanaokuamini wewe Kwa maana ya kawaida, “wanaoliitia jina lako”, ikimaanisha kumwamini Yesu kwa kumwabudu au kumwomba Yeye.
- 9:21 wanaomwamini Yesu Kwa maana ya kawaida, “wanaoliitia jina lake”.
- 9:29 Kiyunani Au “Kigiriki”.
- 9:32 waamini Kwa maana ya kawaida, “watakatifu”, jina kwa ajili ya watu waliomwamini Yesu. Pia katika mstari wa 41.
- 9:36 Dorkasi Maana yake ni mnyama aitwaye paa.
- 10:9 paa Nyakati za Biblia, nyumba zilikuwa na paa zilizosawa kama sakafu, zilizotumika kama vyumba vya ziada au sehemu za kufanyia mazungumzo.
- 11:2 waamini wa Kiyahudi Kwa maana ya kawaida, “watu wa tohara”. Hii inaweza kuwa na maana ya Wayahudi waliodhani kuwa wafuasi wote wa Kristo ni lazima watahiriwe na kutii Sheria ya Musa. Tazama Gal 2:12.
- 11:15 mwanzo Siku ya Pentekoste katika Matendo 2, Roho Mtakatifu alipowashukia wafuasi wa mwanzo wa Yesu na kuwapa nguvu ya kuanza kuuhubiri ulimwengu Habari Njema za wokovu kupitia Yesu.
- 11:19 mateso Au “kipindi cha mateso”. Hiki ni kipindi ambacho viongozi wa Kiyahudi katika mji wa Yerusalemu walikuwa wakiwaadhibu watu wanaomwamini Kristo. Tazama Mdo 8:1-4.
- 11:20 watu wasio Wayahudi Kwa maana ya kawaida, “Wa mataifa” au “Wahelenisti”, au watu waliochangamana na kuathiriwa na utamaduni wa Kiyunani (Kigiriki). Nakala zingine za Kiyunani zina “Wayunani” au “Wagiriki”.
- 11:26 Wafuasi wa Kristo Yaani, Wakristo.
- 11:29 ndugu wote Yaani, Jamaa yote ya Waamini.
- 12:4 kundi la askari kumi na sita Askari hawa walikuwa na zamu ya kulinda ya askari wanne wanne.
- 13:1 Nigeri Ni neno la Kilatini linalomaanisha weusi au nyeusi.
- 13:1 Herode Huyu ni Herode Antipa, mwana wa Herode Mkuu. Huyu ni Herode wa nne. Baada ya Herode Mkuu kufa, ufalme wake uligawanywa kwa wanaye wanne. Tazama Herode katika Orodha ya Maneno.
- 13:20 miaka mia nne na hamsini Yaani miaka 400 ya kuishi Misri, miaka 40 ya kusafiri jangwani na miaka 10 ya kuteka nchi.
- 13:25 Masihi Kwa maana ya kawaida, “Mimi” (yaani, “yeye” au “Yule anayestahili”), Hii inamaanisha yule aliyechaguliwa na kutumwa na Mungu. Linganisha na Yh 1:20. Tazama Masihi katika Orodha ya Maneno.
- 13:51 wakakung'uta … yao Ilionesha kuwa walimaliza kuzungumza na watu hawa.
Matendo 6-10
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Watu Saba Wachaguliwa kwa Kazi Maalumu
6 Watu wengi zaidi walipokuwa wafuasi wa Yesu. Wafuasi waliokuwa wakizungumza Kiyunani walianza kuwalalamikia wafuasi wenzao waliokuwa wanazungumza Kiebrania au Kiaramu. Walisema kuwa wajane wao walikuwa hawapewi mgao wao kutokana na kile wafuasi walikuwa wanapewa kila siku. 2 Mitume kumi na mbili wakaita kundi lote la wafuasi pamoja.
Mitume wakawaambia, “Haitakuwa sahihi sisi kuacha kazi yetu ya kuwafundisha watu neno la Mungu ili tuwe wasimamizi wa ugawaji wa chakula kwa watu. 3 Hivyo, kaka zetu na dada zetu, chagueni wanaume saba miongoni mwenu wenye ushuhuda mzuri, watu waliojaa hekima na Roho. Nasi tutawaweka kuwa wasimamizi wa kazi hii muhimu. 4 Na hivyo itatuwezesha sisi kutumia muda wetu wote katika kuomba na kufundisha neno la Mungu.”
5 Kundi lote la waamini likakubaliana na wazo hili. Hivyo wakawachagua wanaume saba: Stefano (aliyejaa imani na Roho Mtakatifu), Filipo,[a] Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena, na Nikolasi (mtu wa Antiokia aliyeongoka na kufuata dini ya Kiyahudi). 6 Kisha, wakawaweka watu hawa mbele ya mitume, nao mitume waliwaombea na kuweka mikono juu yao.
7 Neno la Mungu lilikuwa linawafikia watu wengi zaidi. Kundi la wafuasi katika Yerusalemu likawa kubwa sana. Hata idadi kubwa ya makuhani wa Kiyahudi waliamini na kutii.
Baadhi ya Wayahudi Wampinga Stefano
8 Mungu alimpa Stefano nguvu ya kutenda maajabu makuu na miujiza katikati ya watu. 9 Lakini baadhi ya Wayahudi pale waliotoka katika sinagogi la Watu Huru,[b] kama lilivyoitwa. Kundi hili lilijumuisha Wayahudi kutoka Kirene, Iskanderia, Kilikia na Asia. Walianza kubishana na Stefano. 10 Lakini Roho Mtakatifu alimwezesha kuzungumza kwa hekima. Maneno yake yalikuwa na nguvu hata Wayahudi hawa hawakuweza kubishana naye.
11 Hivyo wakawaambia baadhi ya watu waseme, “Tumemsikia Stefano akimtukana Musa na Mungu!” 12 Jambo hili liliwakasirisha sana watu, wazee wa Kiyahudi na walimu wa sheria. Wakamkamata Stefano na kumpeleka mbele ya Baraza Kuu.
13 Wayahudi wakawaleta baadhi ya watu kwenye mkutano ili kusema uongo kuhusu Stefano. Watu hawa walisema, “Daima mtu huyu husema maneno kinyume na mahali hapa patakatifu na kinyume na Sheria ya Musa. 14 Tulimsikia akisema kwamba Yesu kutoka Nazareti atapaharibu mahali hapa na kubadilisha yale ambayo Musa aliyotuambia kufanya.” 15 Kila mtu aliyekuwa kwenye mkutano wa baraza alikuwa akimshangaa Stefano kwani uso wake ulionekana kama uso wa malaika.
Hotuba ya Stefano
7 Kuhani mkuu akamwambia Stefano, “Mambo haya ndivyo yalivyo?” 2 Stefano akajibu, “Ndugu zangu na baba zangu Wayahudi, nisikilizeni! Mungu wetu mkuu na mwenye utukufu alimtokea Ibrahimu, baba yetu, alipokuwa Mesopotamia. Kabla hajahamia Harani. 3 Mungu alimwambia, ‘Ondoka katika nchi yako na watu wako, kisha uende katika nchi nitakayokuonesha.’(A)
4 Hivyo Ibrahimu akaondoka katika nchi ya Ukaldayo[c] na kwenda kuishi Harani. Baada ya baba yake kufa, Mungu akamleta katika nchi hii, mahali mnapoishi sasa. 5 Lakini Mungu hakumpa Ibrahimu sehemu yoyote ya ardhi hii, hata eneo dogo lenye ukubwa wa unyayo wake. Lakini Mungu aliahidi kuwa atampa Ibrahimu nchi hii yeye na watoto wake hapo baadaye. Hii ilikuwa kabla Ibrahimu hajapata watoto.
6 Mungu alimwambia: ‘Wazao wako wataishi katika nchi nyingine. Watakuwa wageni. Watu wa huku watawafanya kuwa watumwa na kuwatendea vibaya kwa miaka mia nne. 7 Lakini nitaliadhibu taifa lililowafanya watumwa.’(B) Pia, Mungu alisema, ‘Baada ya mambo hayo kutokea, watu wako watatoka katika nchi hiyo. Kisha wataniabudu mahali hapa.’(C)
8 Mungu aliweka agano na Ibrahimu; alama ya agano hili ilikuwa tohara. Na Ibrahimu alipopata mwana, alimtahiri siku ya nane baada ya kuzaliwa. Jina la mwanaye lilikuwa Isaka. Pia, Isaka alimtahiri mwanaye Yakobo. Na Yakobo alifanya vivyo hivyo kwa wanaye, ambao ndiyo baba wakuu kumi na mbili wa watu wetu.
9 Baba zetu hawa walimwonea wivu Yusufu ndugu yao na wakamwuza ili awe mtumwa Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye, 10 akamwokoa kutoka katika matatizo yake yote. Wakati huo Farao alikuwa mfalme wa Misri. Alimpenda na akamheshimu Yusufu kwa sababu ya hekima ambayo Mungu alimpa. Farao alimfanya Yusufu kuwa gavana wa Misri na msimamizi wa watu wote na kila kitu katika kasri lake. 11 Lakini nchi yote ya Misri na Kanaani zikakosa mvua na mazao ya chakula hayakuweza kuota. Watu waliteseka sana na watu wetu hawakuweza kupata chakula chochote.
12 Lakini Yakobo aliposikia kulikuwa chakula Misri aliwatuma mababa zetu huko. Hii ilikuwa safari yao ya kwanza kwenda Misri. 13 Kisha walikwenda safari ya pili. Safari hii Yusufu akawaeleza ndugu zake yeye ni nani. Ndipo Farao akatambua kuhusu familia ya Yusufu. 14 Kisha Yusufu aliwatuma kaka zake wamwambie Yakobo, baba yake, ahamie Misri. Aliwaalika pia ndugu zake wote, jumla yao wote walikuwa watu sabini na tano. 15 Hivyo Yakobo alitelemka kwenda Misri. Yeye na baba zetu waliishi huko mpaka walipokufa. 16 Baadaye, miili yao ilihamishiwa Shekemu, ambako iliwekwa katika kaburi ambalo Ibrahimu alilinunua kwa fedha kutoka kwa wana wa Hamori.
17 Watu wetu walipokuwa Misri idadi yao iliongezeka. Watu wetu walikuwa wengi mno huko. Ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa Ibrahimu ilikuwa karibu kutimia. 18 Ndipo mfalme mwingine akaanza kutawala Misri, ambaye hakujua lolote kuhusu Yusufu. 19 Mfalme huyu aliwahadaa watu wetu. Akawatendea vibaya sana, akawalazimisha wawaache watoto wao nje ili wafe.
20 Huu ni wakati ambapo Musa alizaliwa. Alikuwa mtoto mzuri sana, na kwa miezi mitatu wazazi wake walimtunza nyumbani. 21 Walipolazimishwa kumtoa nje, Binti wa Farao alimchukua. Alimkuza kama mwanaye wa kumzaa. 22 Musa alielimishwa kwa elimu bora ya Kimisri. Wamisri walimfundisha kila kitu walichojua. Alikuwa mwenye nguvu katika yote aliyosema na kutenda.
23 Musa alipokuwa na umri wa miaka kama arobaini, aliamua kuwatembelea watu wake mwenyewe, watu wa Israeli. 24 Aliona mmoja wao ananyanyaswa na Mmisri, hivyo akamtetea; Musa akampiga na kumwua Mmisri ili kulipiza kwa kumwumiza Mwisraeli. 25 Musa alidhani kwamba watu wake wangeelewa kuwa Mungu alikuwa anamtumia kuwaokoa. Lakini hawakuelewa.
26 Siku iliyofuata, Musa akawaona wawili wa watu wake wakipigana. Alijaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Ninyi ni ndugu! Kwa nini mnataka kuumizana?’ 27 Aliyekuwa akimwumiza mwenzake akamsukuma Musa na akamwambia, ‘Nani amekufanya wewe uwe mtawala na mwamuzi wetu? 28 Unataka kuniua kama ulivyomwua yule Mmisri jana?’(D) 29 Musa alipomsikia akisema hili, alikimbia Misri. Alikwenda kuishi Midiani kama mgeni. Katika kipindi alichoishi huko, alipata wana wawili.
30 Miaka arobaini baadaye, Musa alipokuwa jangwani karibu na Mlima Sinai, malaika alimtokea katika mwali wa moto uliokuwa unawaka katika kichaka. 31 Musa alipoliona hili, alishangaa. Alisogea ili kuangalia kwa karibu. Akasikia sauti; ilikuwa sauti ya Bwana. 32 Bwana alisema, ‘Mimi ni Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zako. Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.’(E) Musa akaanza kutetemeka kwa woga. Aliogopa kukitazama kichaka.
33 Kisha Bwana akamwambia, ‘Vua viatu vyako, kwa sababu mahali uliposimama ni ardhi takatifu. 34 Nimewaona watu wangu wanavyoteseka sana Misri. Nimesikia watu wangu wakilia na nimeshuka ili kuwaokoa. Njoo sasa, Musa, ninakutuma urudi Misri.’(F)
35 Huyu ni Musa ndiye aliyekataliwa na watu wake. Walisema, ‘Nani amekufanya uwe mtawala na mwamuzi wetu?’(G) Lakini ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mtawala na mwokozi. Mungu alimtuma pamoja na msaada wa malaika,[d] ambaye Musa alimwona katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto. 36 Hivyo Musa aliwaongoza watu kutoka Misri. Alitenda maajabu na ishara za miujiza Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani kwa miaka arobaini.
37 Huyu ni Musa yule yule aliyewaambia maneno haya watu wa Israeli: ‘Mungu atakupa nabii. Nabii huyo atakuja kutoka miongoni mwa watu wako mwenyewe. Atakuwa kama mimi.’(H) 38 Musa huyo huyo alikuwa pamoja na kusanyiko la watu wa Mungu jangwani. Alikuwa na malaika aliyezungumza naye alipokuwa Mlima Sinai, na alikuwa pamoja na baba zetu. Alipokea maneno yaletayo uzima kutoka kwa Mungu, na Musa akatupa sisi Maneno hayo.
39 Lakini baba zetu hawakutaka kumtii Musa. Walimkataa, wakataka kurudi Misri. 40 Walimwambia Haruni, ‘Musa alituongoza kutoka katika nchi ya Misri. Lakini hatujui kilichompata. Hivyo tengeneza miungu ili iwe mbele yetu ituongoze.’(I) 41 Hivyo watu wakatengeneza kinyago kinachofanana na ndama. Kisha wakakitolea sadaka za kuteketezwa. Walifurahia kile walichotengeneza kwa mikono yao wenyewe. 42 Lakini Mungu akawaacha, nao wakaendelea kuabudu nyota na sayari.[e] Kitabu cha manabii[f] kinasema hivi:
‘Watu wa Israeli, hamkunipa dhabihu
jangwani kwa miaka arobaini.
43 Mlibeba hema kwa ajili ya kumwabudia Moleki,
na sanamu ya nyota ya mungu wenu Refani.
Hizi zilikuwa sanamu mlizotengeneza ili mziabudu.
Hivyo nitawahamishia mbali, kuvuka Babeli.’(J)
44 Baba zetu walikuwa na Hema Takatifu walipokuwa jangwani. Mungu alimwelekeza Musa jinsi ya kutengeneza hema hii. Aliitengeneza kwa kufuata ramani aliyoonyeshwa na Mungu. 45 Baadaye, Yoshua aliwaongoza baba zetu kuteka ardhi ya mataifa mengine. Watu wetu waliingia, na Mungu akawafukuza watu wengine. Watu wetu walipoingia katika ardhi hii mpya, waliibeba hema hii pamoja nao. Watu wetu waliipata hema hii kutoka kwa baba zao, na watu wetu waliitunza mpaka wakati wa Daudi. 46 Mungu alimpenda Daudi.[g] Na Daudi akamwomba Mungu amruhusu ajenge Hekalu kwa ajili ya watu wa Israeli[h] 47 Lakini Sulemani ndiye aliyemjengea Mungu Hekalu.
48 Lakini Mungu Aliye Juu sana hahitaji yumba zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu ili aishi ndani yake. Nabii aliandika hivi:
49 ‘Bwana asema, Mbingu ni kiti changu cha enzi,
na dunia ni sehemu ya kuweka miguu yangu.
Hivyo mnadhani mnaweza kunijengea nyumba?
Je, ninahitaji mahali pa kupumzika?
50 Kumbukeni, niliumba vitu vyote hivi?’”(K)
51 Kisha Stefano akasema, “Enyi viongozi wa Kiyahudi mlio wakaidi! Mnakataa kumpa Mungu mioyo yenu na mnakataa hata kumsikiliza. Daima mko kinyume na Roho Mtakatifu. Baba zenu walikuwa vivyo hivyo, nanyi mko kama wao! 52 Walimtesa kila nabii aliyewahi kuishi. Waliwaua hata wale ambao zamani zilizopita walisema kwamba Mwenye Haki ilikuwa aje. Na sasa mmekuwa kinyume na Mwenye Haki na mmemwua. 53 Ninyi ndiyo mliipokea Sheria ya Mungu,[i] aliyoitoa kupitia malaika zake. Lakini hamtaki kuitii!”
Stefano Auawa
54 Waliokuwa kwenye mkutano wa baraza waliposikia maneno haya, walikasirika sana na wakamsagia meno Stefano kwa hasira. 55 Lakini Stefano, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alitazama juu mbinguni, na kuuona utukufu wa Mungu. Alimwona Yesu amesimama upande wa kulia wa Mungu. 56 Stefano akasema, “Tazama! Naona mbingu zimefunguka. Na ninamwona Mwana wa Adamu amesimama upande wa kulia wa Mungu.”
57 Kila mmoja pale akaanza kupiga kelele, wakaziba masikio yao kwa mikono yao. Wote kwa pamoja wakamvamia Stefano. 58 Wakamtoa nje ya mji na kuanza kumpiga kwa mawe. Mashahidi walioshuhudia uongo kinyume cha Stefano waliacha makoti yao kwa kijana aliyeitwa Sauli. 59 Walipokuwa wanampiga kwa mawe, Stefano aliomba, akisema, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” 60 Alianguka kwa magoti yake na kupaza sauti, akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii!” Haya yalikuwa maneno yake ya mwisho kabla ya kufa.
8 1-3 Sauli aliridhia kuwa kuuawa kwa Stefano lilikuwa jambo jema. Baadhi ya wacha Mungu walimzika Stefano, wakaomboleza na kumlilia kwa sauti kuu.
Matatizo Kwa waamini
Kuanzia siku hiyo Wayahudi walianza kulitesa sana kanisa na waamini katika mji wa Yerusalemu. Sauli pia alijaribu kuliharibu kanisa. Aliingia katika nyumba za waamini, akawaburuta wanaume na wanawake, na kuwafunga gerezani. Waamini wote walikimbia kutoka Yerusalemu, mitume peke yao ndiyo walibaki. Waamini walikwenda mahali tofauti tofauti katika Uyahudi na Samaria. 4 Walitawanyika kila mahali, na kila walikokwenda waliwahubiri watu Habari Njema.
Filipo Ahubiri Katika Samaria
5 Filipo[j] alikwenda katika mji mkuu wa jimbo la Samaria na kuwahubiri watu kuhusu Masihi. 6 Watu wa Samaria walimsikiliza Filipo na kuona miujiza aliyotenda. Wote walisikiliza kwa makini yale aliyosema. 7 Watu wengi miongoni mwao walikuwa na mapepo, lakini Filipo aliyakemea mapepo na yaliwatoka watu. Mapepo yalipiga kelele nyingi yalipokuwa yanawatoka watu. Walikuwepo pia watu wengi waliopooza na walemavu wa miguu pale. Filipo aliwaombea na wote walipona. 8 Kulikuwa furaha kubwa katika mji ule wa Samaria siku ile!
9 Mtu mmoja aliyeitwa Simoni alikuwa anaishi katika mji huo. Kabla Filipo hajaenda huko, Simoni alikuwa akifanya uchawi na kuwashangaza watu wote wa Samaria. Alijigamba na kujiita mtu mkuu. 10 Watu wote, kuanzia mdogo hadi mkubwa, waliamini yale aliyosema Simoni. Walisema, “Mtu huyu ndiye anayeitwa ‘Nguvu Kuu ya Mungu.’” 11 Simoni aliwashangaza watu kwa muda mrefu kwa uchawi wake na watu wote wakawa wafuasi wake. 12 Lakini Filipo alipowahubiri watu Habari Njema kuhusu Ufalme wa Mungu na Nguvu za Yesu Kristo. Wanaume na wanawake waliamini alichosema Filipo na wakabatizwa. 13 Simoni mwenyewe aliamini, na baada ya kubatizwa, alikaa karibu na Filipo. Alipoona miujiza na matendo makuu ya ajabu yaliyofanyika kupitia Filipo, alishangaa.
14 Mitume mjini Yerusalemu, waliposikia kuwa watu wa Samaria wameupokea Ujumbe wa Mungu, waliwatuma Petro na Yohana kwenda kwa watu wa Samaria. 15 Petro na Yohana walipofika, waliomba ili Roho Mtakatifu awashukie waamini wa Samaria. 16 Watu hawa walikuwa wamebatizwa katika jina la Bwana Yesu, lakini Roho Mtakatifu alikuwa bado hajamshukia hata mmoja wao. Na hii ndiyo sababu Petro na Yohana waliomba. 17 Mitume hawa wawili walipoweka mikono yao juu ya watu, Roho Mtakatifu aliwashukia.
18 Simoni aliyekuwa mchawi alipoona Roho Mtakatifu anatolewa kwa watu kwa kuweka mikono juu yao. Aliwapa pesa mitume. 19 Akasema, “Nipeni na mimi nguvu hii ili nitakapoweka mikono yangu juu ya mtu yeyote, atampata Roho Mtakatifu.”
20 Petro akamwambia Simoni, “Wewe pamoja na pesa zako mwangamie kwa sababu unadhani unaweza kununua karama kutoka kwa Mungu kwa pesa. 21 Huwezi kushirikiana nasi katika kazi hii. Moyo wako si safi mbele za Mungu. 22 Badili moyo wako! Achana na mawazo haya maovu na umwombe Bwana. Yumkini atakusamehe! 23 Kwa kuwa ninaona umejaa wivu mwingi nawe ni mfungwa wa uovu.”
24 Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Bwana, ili haya uliyosema yasinipate.”
25 Ndipo wale mitume wawili waliwaambia watu waliyoona Yesu akitenda. Wakawaambia ujumbe wa Bwana. Kisha wakarudi Yerusalemu. Wakiwa njiani kurudi, walipitia katika miji mingi ya Wasamaria na kuwahubiri watu Habari Njema.
Filipo Amfundisha Mtu Kutoka Ethiopia
26 Malaika wa Bwana alimwambia Filipo, “Jiandae na uende kusini katika barabara ya jangwani inayoteremka kutoka Yerusalemu kwenda Gaza.”
27 Filipo alijiandaa na kwenda. Akiwa njiani alimwona mwanaume kutoka Ethiopia. Alikuwa towashi na ofisa muhimu wa Kandake, malkia wa Ethiopia. Alikuwa na mweka hazina mkuu wa malkia. Mtu huyu alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu. 28 Na alikuwa anarudi Ethiopia. Alikuwa ameketi katika gari lake la kukokotwa na farasi akiwa anasoma kitabu cha nabii Isaya.
29 Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye gari hilo na uwe karibu yake.” 30 Hivyo Filipo akaenda karibu na gari, akamsikia mtu yule akisoma kutoka katika kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamwuliza, “Unaelewa unachosoma?”
31 Yule mtu akajibu, “Nitaelewaje? Ninahitaji mtu wa kunifafanulia.” Ndipo akamwomba Filipo apande garini na aketi pamoja naye. 32 Sehemu ya Maandiko aliyokuwa anasoma ilikuwa hii:
“Alikuwa kama kondoo
anayepelekwa kwa mchinjaji.
Alikuwa kama mwana kondoo asivyopiga kelele
anapokatwa manyoya yake.
Hakusema kitu.
33 Alidhalilishwa,
na kunyimwa haki zake zote.
Maisha yake duniani yamekoma.
Hivyo hakutakuwa simulizi yoyote kuhusu wazaliwa wake.”(L)
34 Afisa[k] akamwambia Filipo, “Tafadhali niambie, nabii anazungumza kuhusu nani? Anazungumza kuhusu yeye mwenyewe au mtu mwingine?” 35 Filipo akaanza kuzungumza. Alianzia na Andiko hili na kumwambia mtu yule Habari Njema kuhusu Yesu.
36 Walipokuwa wanasafiri waliyakuta maji mahali fulani. Afisa akasema, “Tazama! Hapa kuna maji! Nini kinanizuia nisibatizwe?” 37 [l] 38 Ndipo Afisa akaamuru gari lake lisimame. Wote wawili, Filipo na Afisa, wakatelemka wakaingia kwenye maji na Filipo akambatiza towashi. 39 Walipotoka kwenye maji, Roho wa Bwana akamchukua Filipo; afisa hakumwona Filipo tena. Afisa aliendelea na safari yake kurudi nyumbani, akiwa mwenye furaha sana. 40 Lakini Filipo alionekana katika mji ulioitwa Azoto. Alikuwa akienda kwenye mji wa Kaisaria. Aliwahubiri watu Habari Njema katika miji yote wakati anasafiri kutoka Azoto kwenda Kaisaria.
Sauli Awa Mfuasi wa Yesu
9 Huko Yerusalemu Sauli aliendelea kuwatisha wafuasi wa Bwana, na hata kuwaambia kuwa angewaua. Alikwenda kwa kuhani mkuu, 2 na kumwomba aandike barua kwenda kwenye masinagogi yaliyokuwa katika mji wa Dameski. Sauli alitaka kuhani mkuu ampe mamlaka ya kuwatafuta watu katika mji wa Dameski waliokuwa wafuasi wa Njia ya Bwana.[m] Ikiwa angewapata waamini huko, wanaume au wanawake, angewakamata na kuwaleta Yerusalemu.
3 Hivyo Sauli alikwenda Dameski. Alipoukaribia mji, ghafla mwanga mkali kutoka mbinguni ukaangaza kumzunguka. 4 Akadondoka chini na akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli! Kwa nini unanitesa?”
5 Sauli akasema, “Wewe ni nani, Bwana?”
Sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu, unayemtesa. 6 Simama sasa na uingie mjini. Mtu mmoja huko atakueleza unachopaswa kufanya.”
7 Wanaume waliokuwa wanasafiri pamoja na Sauli walisimama pale kimya. Waliisikia sauti, lakini hawakumwona yeyote. 8 Sauli alisimama kutoka chini na kufumbua macho yake, lakini hakuweza kuona. Hivyo wale aliokuwa nao wakamshika mkono na kumwongoza kuingia Dameski. 9 Kwa siku tatu Sauli hakuweza kuona; hakula wala kunywa.
10 Alikuwepo mfuasi wa Yesu katika mji wa Dameski aliyeitwa Anania. Katika maono Bwana alimwita, “Anania!”
Anania alijibu, “Niko hapa, Bwana.”
11 Bwana akamwambia, “Amka na uende katika mtaa unaoitwa Mtaa Ulionyooka. Tafuta nyumba ya Yuda[n] na uliza kuhusu mtu anayeitwa Sauli anayetoka katika mji wa Tarso. Yuko katika nyumba hiyo sasa, anaomba. 12 Ameoneshwa katika maono kuwa mtu anayeitwa Anania anamwendea na kuweka mikono juu yake ili aweze kuona tena.”
13 Lakini Anania akajibu, “Bwana, watu wengi wameniambia kuhusu mtu huyu. Wameniambia kuhusu mambo mengi mabaya aliyowatendea watu wako watakatifu katika mji wa Yerusalemu. 14 Na sasa amekuja hapa Dameski. Viongozi wa makuhani wamempa mamlaka ya kuwakamata watu wote wanaokuamini wewe.”[o]
15 Lakini Bwana Yesu akamwambia Anania, “Nenda, nimemchagua Sauli kwa kazi maalumu. Ninataka ayahubiri mataifa mengine, watawala na watu wa Israeli kuhusu mimi. 16 Nitamwonyesha yote ambayo lazima atateseka kwa ajili yangu.”
17 Hivyo Anania aliondoka na kwenda nyumbani kwa Yuda. Akaweka mikono yake juu ya Sauli na kusema, “Sauli, ndugu yangu, Bwana Yesu amenituma. Ndiye uliyemwona barabarani wakati ukija hapa. Amenituma ili uweze kuona tena, pia ujazwe Roho Mtakatifu.” 18 Ghafla, vitu kama magamba ya samaki vikaanguka kutoka kwenye macho ya Sauli. Akaanza kuona tena! Kisha akasimama na kwenda kubatizwa. 19 Baada ya kula chakula, akaanza kujisikia kuwa na nguvu tena.
Sauli Aanza Kuhubiri Juu ya Yesu Kristo
Sauli alikaa pamoja na wafuasi wa Yesu katika mji wa Dameski kwa siku chache. 20 Baadaye alianza kwenda katika masinagogi na kuwahubiri watu kuhusu Yesu. Aliwaambia watu, “Yesu ni Mwana wa Mungu!”
21 Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa. Wakaulizana, “Je, huyu si yule aliyekuwa anajaribu kuwaangamiza watu wanaomwamini Yesu[p] katika mji wa Yerusalemu? Na hakuja hapa ili awakamate wafuasi wa Yesu na kuwarudisha kwa viongozi wa makuhani?”
22 Lakini Sauli aliendelea kuwa nguvu katika kuthibitisha kwamba Yesu ndiye Masihi. Uthibitisho wake ulikuwa na nguvu kiasi kwamba Wayahudi walioishi Dameski hawakuweza kubishana naye.
Sauli Awatoroka Wayahudi
23 Baada ya siku nyingi kupita, baadhi ya Wayahudi waliweka mpango wa kumwua Sauli. 24 Waliyalinda malango ya mji usiku na mchana. Walitaka kumwua Sauli, lakini aliambiwa kuhusu mpango wao. 25 Usiku mmoja baadhi ya wafuasi ambao Sauli aliwafundisha walimsaidia kuondoka mjini. Walimweka katika kikapu, wakamtoa kwa kumshusha kupitia kwenye tundu lililokuwa kwenye ukuta wa mji.
Sauli Katika Mji wa Yerusalemu
26 Kisha Sauli alikwenda Yerusalemu. Akajaribu kujiunga na kundi la wafuasi, lakini wote walimwogopa. Hawakuamini kuwa naye amekuwa mfuasi wa Yesu. 27 Lakini Barnaba alimkubali Sauli, akamchukua na kumpeleka kwa mitume. Akawaeleza namna ambavyo Sauli alimwona Bwana akiwa njiani na namna ambavyo Bwana aliongea naye. Kisha akawaambia namna ambavyo Sauli amehubiri kwa ujasiri kuhusu Yesu katika mji wa Dameski.
28 Sauli alikaa na wafuasi na kwenda kila mahali katika mji wa Yerusalemu akihubiri kwa ujasiri kwa ajili ya Bwana. 29 Kila mara alibishana na Wayahudi waliokuwa waliozungumza Kiyunani,[q] ambao walianza kutengeneza mpango wa kumwua. 30 Waamini walipoujua mpango huu, walimchukua Sauli mpaka Kaisaria, na kutoka huko walimsafirisha mpaka katika mji wa Tarso.
31 Kanisa katika Uyahudi yote, Galilaya na Samaria likawa na wakati wa amani. Na kwa msaada wa Roho Mtakatifu, vikundi hivi vya waamini vikawa na nguvu katika imani na kuonesha utii kwa ajili ya Bwana kwa namna walivyoishi. Hivyo kanisa kila mahali liliongezeka kwa idadi.
Petro akiwa Lida na Yafa
32 Petro alikuwa akisafiri katika sehemu zote za Uyahudi, Galilaya na Samaria, na akasimama kuwatembelea waamini[r] walioishi Lida. 33 Huko alikutana na mtu aliyeitwa Ainea, ambaye alikuwa amepooza na hakuweza kutoka kitandani kwa miaka nane. 34 Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo amekuponya. Simama na kiweke kitanda chako vizuri!” Ainea alisimama saa ile ile. 35 Watu wote walioishi Lida na tambarare ya Sharoni walimwona, na wakaamua kumfuata Bwana.
36 Katika mji wa Yafa kulikuwa na mfuasi wa Yesu aliyeitwa Tabitha, Jina lake kwa Kiyunani lilikuwa Dorkasi.[s] Daima aliwatendea watu mambo mema na kuwapa pesa wale wenye mahitaji. 37 Petro alipokuwa Lida, Tabitha aliugua na kufa. Waliusafisha mwili wake na kuuweka chumbani ghorofani. 38 Wafuasi waliokuwa Yafa wakasikia kuwa Petro yuko Lida, mji ambao haukuwa mbali na Yafa. Hivyo waliwatuma watu wawili, waliomsihi Petro wakisema, “Tafadhali njoo kwetu haraka!”
39 Petro alijiandaa na kwenda pamoja nao. Alipofika, walimchukua na kumpeleka kwenye chumba ghorofani. Wajane wote walisimama wakamzunguka huku wakilia na wakamwonesha mavazi ambayo Tabitha alitengeneza alipokuwa hai. 40 Petro akawatoa watu wote chumbani. Akapiga magoti na kuomba. Kisha akaugeukia mwili wa Tabitha na kusema, “Tabitha! Simama.” Akafumbua macho yake. Alipomwona Petro akaketi. 41 Petro akamshika mkono na akamsaidia kusimama. Ndipo akawaita waamini na wajane chumbani. Akawaonyesha Tabitha; akiwa hai!
42 Watu kila mahali katika mji wa Yafa wakatambua kuhusu hili, na wengi wakamwamini Bwana. 43 Petro alikaa Yafa siku nyingi nyumbani kwa mtu mmoja aitwaye Simoni, aliyekuwa mtengenezaji wa ngozi.
Petro na Kornelio
10 Kulikuwa mtu aliyeitwa Kornelio katika mji wa Kaisaria. Mtu huyu alikuwa ofisa wa kikosi kilichoitwa “Kikosi cha Kiitalia” katika jeshi la Rumi. 2 Alikuwa mcha Mungu. Yeye na watu wengine wote walioishi katika nyumba yake walikuwa wanamwabudu Mungu wa kweli. Alitoa pesa zake nyingi kuwasaidia maskini miongoni mwa Wayahudi na daima alimwomba Mungu kwa kufuata utaratibu kama ilivyokuwa. 3 Mchana mmoja yapata saa tisa, kwa uwazi na dhahiri Kornelio aliona maono. Alimwona malaika kutoka kwa Mungu akimwendea na akamwambia, “Kornelio!”
4 Akiwa anashangaa na kuogopa, Kornelio akasema, “Unataka nini, bwana?”
Malaika akamwambia, “Mungu amesikia maombi yako na ameona sadaka zako unazowapa maskini. Anakukumbuka kwa yote uliyotenda. 5 Tuma baadhi ya watu sasa waende katika mji wa Yafa wakamlete mtu anayeitwa Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. 6 Anakaa kwa mtu ambaye naye pia anaitwa Simoni, mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko kwenye ufukwe wa bahari.” 7 Malaika aliyeongea na Kornelio akaondoka. Ndipo Kornelio aliita watumishi wake wawili na askari mmoja. Askari alikuwa mcha Mungu, mmoja wa wasaidizi wake wa karibu. 8 Kornelio akawaelekeza kila kitu watu hawa watatu kisha akawatuma kwenda Yafa.
9 Siku iliyofuata wakati wa adhuhuri walipokuwa wanaukaribia mji wa Yafa, Petro alipanda juu ya paa[t] kuomba. 10 Alihisi njaa na akataka chakula. Lakini walipokuwa wanamwandalia chakula ili ale, aliona maono. 11 Aliona mbingu zikifunguka na kitu kama shuka kubwa kikishushwa chini kutoka mbinguni kwa pembe nne. 12 Ndani yake mlikuwa aina zote za wanyama, watambaao na ndege. 13 Kisha sauti ikamwambia, “Petro simama uchinje chochote hapa kisha ule.”
14 Lakini Petro akasema, “Siwezi kufanya hivyo, Bwana! Sijawahi kula kitu chochote kisicho safi au kisicho stahili kutumiwa kwa chakula.”
15 Lakini sauti ikamwambia tena, “Mungu amekwisha vitakasa vitu vyote hivi. Usiseme havistahili kuliwa.” 16 Hili lilimtokea mara tatu. Kisha likachukuliwa mbinguni. 17 Petro alijiuliza maono haya yalikuwa na maana gani.
Watu ambao Kornelio aliwatuma walishaiona nyumba ya Simoni na walikuwa wamesimama mlangoni. 18 Waliuliza, “Je, Simoni Petro yuko hapa?”
19 Petro akiwa bado anafikiri kuhusu maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Sikiliza, kuna watu watatu wanakutafuta. 20 Inuka na ushuke chini. Nenda nao, usisite, kwa sababu nimewatuma.” 21 Hivyo Petro akashuka chini na kuwaambia, “Nafikiri mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja hapa?”
22 Wale watu wakasema, “Malaika mtakatifu amemwambia Kornelio akualike nyumbani mwake. Ni mtu mwema na hutenda kwa haki, na anamwabudu Mungu na Wayahudi wote wanamheshimu. Malaika alimwambia akualike nyumbani kwake ili asikilize yale utakayosema.” 23 Petro akawakaribisha ndani watu wale ili walale usiku huo.
Siku iliyofuata Petro alijiandaa na kuondoka na wale watu watatu. Baadhi ya waamini katika mji wa Yafa walikwenda pamoja naye. 24 Siku iliyofuata walifika katika mji wa Kaisaria. Kornelio alikuwa anawasubiri na alikuwa amewakusanya jamaa na rafiki zake wa karibu nyumbani mwake.
25 Petro alipoingia ndani ya nyumba, Kornelio alimlaki kisha akaanguka miguuni kwa Petro na akamwabudu. 26 Lakini Petro akamwambia asimame. Petro akasema, “Simama! Mimi ni mtu tu kama wewe.” 27 Petro aliendelea kuzungumza na Kornelio. Ndipo Petro akaingia ndani na kuona kundi kubwa la watu wamekusanyika pale.
28 Petro akawaambia watu wale kuwa, “Mnaelewa kuwa ni kinyume na sheria yetu kwa Myahudi kushirikiana au kumtembelea mtu ambaye si Myahudi. Lakini Mungu amenionyesha kuwa nisimchukulie mtu yeyote kuwa yu kinyume na desturi za Kiyahudi. 29 Ndiyo sababu sikubisha watu wenu waliponiambia kuja hapa. Sasa, tafadhali niambieni kwa nini mmeniita hapa.”
30 Kornelio akasema, “Siku nne zilizopita, kama saa tisa mchana nilikuwa ninaomba ndani ya nyumba yangu. Ghafla akawepo mtu mmoja amesimama mbele yangu amevaa mavazi meupe yanayong'aa. 31 Akasema, ‘Kornelio, Mungu amesikia maombi yako na ameona sadaka zako kwa maskini. Anakukumbuka wewe na yote uliyofanya. 32 Hivyo tuma baadhi ya watu kwenye mji wa Yafa na wamwambie Simoni Petro kuja. Anakaa na mtu mwingine anayeitwa Simoni, mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko pembeni mwa bahari.’
Footnotes
- 6:5 Filipo Siyo mtume aliyeitwa Filipo.
- 6:9 Watu Huru Wayahudi waliokuwa watumwa au ambao baba zao walikuwa watumwa, lakini wao walikuwa huru.
- 7:4 Ukaldayo Au “Babeli”, nchi iliyo kusini mwa Mesopotamia. Tazama mstari wa 2.
- 7:35 Hapa inamaanisha kuwa Musa aliambatana na nguvu za Mungu na ulinzi wa malaika.
- 7:42 nyota na sayari Ama jeshi lililoko angani. Nyakati za kale watu waliamini kuwa nyota na sayari zilikuwa miungu au malaika.
- 7:42 Kitabu cha manabii Hiki ni kitabu cha manabii wadogo kumi na mbili: Kuanzia Hosea mpaka Malaki.
- 7:46 Mungu alimpenda Daudi Au “alipendelewa na Mungu”.
- 7:46 watu wa Israeli Kwa maana ya kawaida, “nyumba ya Yakobo”. Nakala zingine za Kiyunani zina “Mungu wa Yakobo”.
- 7:53 Sheria ya Mungu Yaani Torati.
- 8:5 Filipo Siyo mtume aliyeitwa Filipo.
- 8:34 Afisa Kwa maana ya kawaida, “towashi”. Pia katika mstari wa 36,38,39.
- 8:37 Nakala zingine za baadaye za Matendo zimeongeza mstari wa 37: Filipo akajibu, “Ikiwa unaamini kwa moyo wako wote unaweza kubatizwa. Ofisa akasema, ‘Ninaamini kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu.’”
- 9:2 Njia ya Bwana Ni maneno yaliyotumika ili kuainisha tabia na mafundisho ya Yesu.
- 9:11 Yuda Huyu si mmoja wa mitume aliyeitwa Yuda.
- 9:14 wanaokuamini wewe Kwa maana ya kawaida, “wanaoliitia jina lako”, ikimaanisha kumwamini Yesu kwa kumwabudu au kumwomba Yeye.
- 9:21 wanaomwamini Yesu Kwa maana ya kawaida, “wanaoliitia jina lake”.
- 9:29 Kiyunani Au “Kigiriki”.
- 9:32 waamini Kwa maana ya kawaida, “watakatifu”, jina kwa ajili ya watu waliomwamini Yesu. Pia katika mstari wa 41.
- 9:36 Dorkasi Maana yake ni mnyama aitwaye paa.
- 10:9 paa Nyakati za Biblia, nyumba zilikuwa na paa zilizosawa kama sakafu, zilizotumika kama vyumba vya ziada au sehemu za kufanyia mazungumzo.
© 2017 Bible League International