Yesu Awabariki Watoto Wadogo

13 Kisha watoto wadogo wakaletwa kwa Yesu ili aweke mikono yake juu yao na awaombee. Lakini wanafunzi wake wakawakemea wali owaleta. 14 Yesu akawaambia, “Waacheni watoto waje kwangu, msiwazuie; kwa maana Ufalme wa mbinguni ni wa walio kama hawa. 15 Alipokwisha wawekea mikono akaondoka.

Mtu Tajiri

16 Mtu mmoja alikuja kwa Yesu akamwuliza, “Mwalimu, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?”

17 Yesu akamjibu, “Mbona unaniuliza kuhusu jambo jema? Kuna mmoja tu aliye mwema . Lakini kama unataka kuingia uzimani, tii amri.”

18 Yule mtu akamwuliza, “Amri zipi?” Yesu akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, 19 waheshimu baba yako na mama yako na umpende jirani yako kama nafsi yako.”

20 Yule kijana akasema, “Zote hizi nimezitii. Ninapungukiwa na nini zaidi?”

21 Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda kauze vitu vyote ulivyo navyo na fedha utakazopata uwape maskini, nawe utakuwa umejiwekea hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.” 22 Yule kijana aliposikia hayo aliondoka kwa masikitiko, kwa sababu alikuwa tajiri sana.

Hatari Za Utajiri

23 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi, “Nawaambieni kweli, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni. 24 Tena nawaambieni, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni.” 25 Wanafunzi wake waliposikia haya walishangaa sana, wakamwuliza, “Ni nani basi anaweza kuokoka?” 26 Lakini Yesu akawatazama akawaambia, “Kwa binadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu kila kitu kinawezekana.” 27 Ndipo Petro aka mwambia, “Na sisi tulioacha kila kitu tukakufuata tutapata nini?”

28 Yesu akawajibu, “Ninawahakikishia kwamba, katika dunia mpya, wakati mimi Mwana wa Adamu nitakapoketi kwenye kiti changu cha utukufu cha enzi, ninyi mlionifuata pia mtaketi katika viti vya enzi kumi na viwili, mkiyahukumu yale makabila kumi na mawili ya Israeli. 29 Na kila mtu aliyeacha nyumba au ndugu zake au dada zake au baba au mama au watoto wake au mashamba kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia zaidi ya hayo, na atarithi uzima wa milele. 30 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.”

Read full chapter