Ukoo Wa Yesu Kristo

Kumbukumbu ya vizazi vya ukoo wa Yesu Kristo mwana wa Daudi na wa Abrahamu: Abrahamu alikuwa baba yake Isaka; Isaka alikuwa baba yake Yakobo; na Yakobo alikuwa baba yake Yuda na ndugu zake. Yuda alikuwa baba yake Peresi na Zera ambao mama yao alikuwa Tamari; Peresi alikuwa baba yake Esroni; Esroni alikuwa baba yake Aramu; Aramu alikuwa baba yake Aminadabu; Aminadabu alikuwa baba yake Nashoni; Nashoni alikuwa baba yake Salmoni; Salmoni alikuwa baba yake Boazi na mama yake Salmoni alikuwa Rahabu. Boazi alikuwa baba yake Obedi, ambaye mama yake alikuwa Ruti; Obedi alikuwa baba yake Yese; Yese alikuwa baba yake Daudi ambaye alikuwa mfalme. Daudi alikuwa baba yake Solomoni ambaye mama yake ni yule aliyekuwa mke wa Uria; Solomoni alikuwa baba yake Rehoboamu; Rehoboamu alikuwa baba yake Abiya; Abiya alikuwa baba yake Asa; Asa alikuwa baba yake Yehoshafati; Yehoshafati alikuwa baba yake Yoramu; Yoramu alikuwa baba yake Uzia; Uzia alikuwa baba yake Yothamu; Yothamu alikuwa baba yake Ahazi; Ahazi alikuwa baba yake Hezekia; 10 Hezekia alikuwa baba yake Manase; Manase alikuwa baba yake Amoni; Amoni alikuwa baba yake Yosia; 11 wakati wa uhamisho wa Babiloni, Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake; 12 na baada ya uhamisho wa Babiloni Yekonia alimzaa Shealtieli; Shealtieli alikuwa baba yake Zerubabeli; 13 Zeru babeli alikuwa baba yake Abihudi; Abihudi alikuwa baba yake Eliakimu ; Eliakimu alikuwa baba yake Azori; 14 Azori alikuwa baba yake Zadoki; Zadoki alikuwa baba yake Akimu; Akimu alikuwa baba yake Eliudi; 15 Eliudi alikuwa baba yake Elieza; Elieza alikuwa baba yake Matani; Matani alikuwa baba yake Yakobo; 16 Yakobo alikuwa baba yake Yosefu ambaye alikuwa mumewe Mar ia, aliyemzaa Yesu anayeitwa Kristo. 17 Basi, kulikuwepo vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka wakati wa mfalme Daudi; na vizazi kumi na vinne tangu mfalme Daudi hadi wakati wa uhamisho wa Babiloni na vizazi kumi na vinne tangu wakati wa uhamisho hadi Kristo.

Kuzaliwa Kwa Yesu Kristo

18 Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi: Maria mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla ya ndoa yao, Mar ia akiwa bado bikira, alipata mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 19 Kwa kuwa Yosefu alikuwa mtu mwema hakutaka kumwaibisha mchumba wake Maria hadharani. Kwa hiyo aliamua kuvunja uchumba wao kwa siri. 20 Lakini alipokuwa bado anawaza juu ya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto akasema, “Yosefu mwana wa Daudi, usisite kumwoa Maria mchumba wako kwa maana mimba aliyo nayo ameipata kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 21 Naye atamzaa mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yesu; kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao.”

22 Hayo yote yalitokea ili kutimiza maneno ya Mungu yaliyos emwa na nabii wake: 23 “Tazama bikira atachukua mimba, naye atamzaa mtoto wa kiume nao watamwita Imanueli,” maana yake, “Mungu pamoja nasi”. 24 Yosefu alipoamka usingizini, alifanya kama alivyoagizwa na malaika wa Bwana; akamchukua mkewe Maria nyumbani kwake, 25 lakini hawakukaribiana mpaka Maria alipoji fungua mtoto wa kiume. Yosefu akamwita jina lake Yesu.