Mfano Wa Mbegu

Wakati mwingine tena Yesu alianza kufundisha kando ya ziwa. Watu wengi walikusanyika wakasongamana mpaka ukingoni mwa ziwa. Ikambidi Yesu aingie kwenye mashua, akaketi humo. Akawafundisha mambo mengi kwa kutumia mifano na katika mafundisho yake akasema:

“Sikilizeni! Mkulima mmoja alikwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akipanda, baadhi ya mbegu zilianguka njiani; ndege wakaja wakazila. Nyingine zilianguka kwenye mwamba ambapo kuli kuwa na udongo haba; zikaota haraka. Kwa kuwa udongo haukuwa na kina, jua kali lilipowaka zilinyauka na kukauka kwa kuwa hazi kuwa na mizizi. Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, miiba hiyo ikakua ikazisonga kwahiyo hazikuzaa matunda.

Na mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri, zikaota vizuri na kukua; zikazaa matunda; moja thelathini, nyingine sitini na nyingine mia moja.” Kisha Yesu akasema, “Mwenye nia ya kusikia na asikie.”

Kwa Nini Yesu Alitumia Mifano

10 Alipokuwa peke yake, baadhi ya wale waliokuwepo, pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili, walimwuliza kuhusu mifano yake. 11 Akawaambia, “Siri ya Ufalme wa Mungu imefunuliwa kwenu, lakini kwa wale walioko nje ya Ufalme wa Mungu, kila kitu husemwa kwa mifano 12 ili: ‘Kutazama watazame lakini wasione, kusikia wasikie lakini wasielewe. Kwa maana kama wangesikia na kuelewa wangegeuka na kutubu, wakasamehewa.’ ”

Yesu Afafanua Maana Ya Mfano Wa Mbegu

13 Kisha Yesu akawauliza, “Hamwelewi maana ya mfano huu? Mtaelewaje basi mifano mingine? 14 Yule mtu aliyepanda mbegu, alipanda neno la Mungu. 15 Mbegu zilizoanguka njiani ni sawa na watu ambao husikia neno la Mungu na shetani akaja mara moja na kulichukua lile neno lililopandwa ndani yao. 16 Hali kadhalika, mbegu iliyoanguka kwenye mwamba ni sawa na watu ambao hulisikia neno na kulipokea kwa furaha. 17 Lakini kwa kuwa neno halipenyi ndani, linadumu kwa muda mfupi. Taabu au mateso yanapotokea kwa ajili ya hilo neno, wao hupoteza imani yao. 18 Na wengine, ni kama mbegu zile zilizoanguka kwenye miiba. Wao hulisikia neno, 19 lakini mahangaiko ya dunia, udanganyifu wa mali na tamaa za mambo mbalimbali hulisonga lile neno, lisizae matunda.

20 “Bali wengine ni kama ile mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri. Wao hulisikia neno wakalipokea na kuzaa matunda: wengine thelathini, wengine sitini, na wengine mia moja.”

Mfano Wa Taa

21 Akawaambia tena, “Je, mtu anapowasha taa, huifunika kwa bakuli au kuiweka mvunguni? Si anaiweka mahali pa wazi? 22 Hali kadhalika, kila kilichofichwa kitatolewa hadharani; na kila siri itafichuliwa. 23 Mwenye nia ya kusikia, na asikie.”

24 Akaendelea kuwaambia, “Myaweke maanani haya mnayosikia. Kipimo mnachotumia kwa wengine ndicho kitakachotumiwa kuwapima na ninyi, hata na zaidi. 25 Kwa maana aliye na kitu ataongezewa, na asiye na kitu atanyang’anywa hata kile kidogo alicho nacho.”

Mfano Wa Jinsi Mbegu Inavyoota

26 Akawaambia tena, “Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu apandaye mbegu shambani. 27 Akishazipanda, usiku hulala na mchana huamka, wakati huo mbegu huota na kukua pasipo yeye kujua inakuaje. 28 Udongo wenyewe huwezesha mimea hiyo kuchipua, kukua na kukomaa. 29 Mavuno yanapokuwa tayari, bila kupoteza wakati, yule mkulima huleta mtu akaikata hiyo mimea kwa kuwa wakati wa kuvuna umefika.”

Mfano Wa Mbegu Ya Haradali

30 Akawaambia tena, “Tuufananishe Ufalme wa Mungu na nini? Au tutumie mfano gani ili kuuelezea? 31 Tunaweza kuufa nanisha na punje ya haradali, ambayo ni mbegu ndogo sana kuliko mbegu zote zinazopandwa ardhini. 32 Lakini ikishaota, hukua ikawa mmea mkubwa kuliko yote katika bustani, ikawa na matawi makubwa hata ndege wa angani wakaweza kujenga viota kwenye kiv uli chake.”

33 Yesu alitumia mifano mingine mingi kama hii kuwaelezea neno la Mungu, kwa kadiri walivyoweza kuelewa. 34 Hakuwafundisha lo lote kuhusu Ufalme wa Mungu pasipo kutumia mifano. Lakini ali pokuwa na wanafunzi wake, aliwafafanulia kila kitu.

Yesu Atuliza Dhoruba

35 Siku hiyo, ilipokaribia jioni, aliwaambia wanafunzi wake, “Tuvuke, twende ng’ambo ya pili.” 36 Wakawaacha wale watu wakaingia katika ile mashua ambamo Yesu alikuwa amekaa. Pia palikuwa na mashua nyingine.

37 Pakatokea dhoruba kali, mawimbi yakaipiga ile mashua waliyokuwa wakivukia, ikaanza kujaa maji. Yesu alikuwa amelala akiegemea mto sehemu ya nyuma kwenye ile mashua. 38 Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kwamba tuna zama?’ 39 Akaamka, akaukemea ule upepo, akaiambia ile bahari, “Kaa kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari.

40 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa? Je, bado hamna imani?”

41 Lakini wao walikuwa wamejawa na hofu wakaulizana, “Ni nani huyu ambaye hata upepo na mawimbi vinamtii?”