Add parallel Print Page Options

Yesu Amefufuka Kutoka Mauti

(Mt 28:1-8; Lk 24:1-12; Yh 20:1-10)

16 Sabato ilipomalizika, Mariamu Magdalena, Maria mama yake Yakobo, na Salome wakanunua manukato yenye harufu nzuri ili kuyapaka kwenye mwili wa Yesu. Alfajiri na mapema Jumapili, mara tu baada ya jua kuchomoza, walienda kwenye kaburi la Yesu. Nao walikuwa wakiambiana wao kwa wao, ni nani atakayelivingirisha jiwe litoke katika mlango wa kaburi kwa ajili yetu?

Kisha wakatazama juu na wakaona kuwa jiwe lile kubwa lilikuwa limevingirishwa tayari litoke mlangoni mwa kaburi la Yesu. Walipoingia kaburini, wakamwona kijana mmoja ameketi upande wa kulia naye alikuwa amevaa vazi jeupe, nao wakastaajabu.

Naye akamwambia, “Usistaajabu. Unamtafuta Yesu wa Nazareti, aliyesulubiwa? Tazama amefufuka! Hayupo hapa. Angalieni mahali walipokuwa wameweka mwili wake. Hata hivyo nendeni na kuwaeleza wafuasi wake pamoja na Petro kwamba: ‘Ametangulia mbele yenu kuelekea Galilaya. Mtamkuta kule, kama alivyowaambia.’”

Kwa hiyo wale wanawake walitoka na kukimbia kutoka kaburini, kwa sababu hofu na mshangao ulikuwa umewajia. Nao hawakusema chochote kwa mtu yeyote kwani waliogopa.[a]

Baadhi ya Wafuasi Wamwona Yesu

(Mt 28:9-10; Yh 20:11-18; Lk 24:13-35)

Baada ya Yesu kufufuka alfajiri na mapema siku ya Jumapili, alimtokea kwanza Maria Magdalena, ambaye awali alifukuza mashetani saba kutoka kwake. 10 Baada ya Mariamu kumwona Yesu, alienda na kuwaeleza wanafunzi wake. Walikuwa wamehuzunishwa sana na walikuwa wakilia. 11 Lakini Mariamu aliwaambia kwamba Yesu yu hai. Aliwaambia ya kwamba yeye amemwona, lakini wao hawakumwamini.

12 Baada ya hayo, Yesu kwa namna tofauti akawatokea wanafunzi wake wawili walipokuwa wakitembea kuelekea mashambani. 13 Hawa kisha walirudi na wakawasimulia wengine wote, lakini nao hawakuwaamini.

Yesu Awatokea Wafuasi Wake

(Mt 28:16-20; Lk 24:36-49; Yh 20:19-23; Mdo 1:6-8)

14 Baadaye, Yesu aliwatokea wale mitume kumi na mmoja walipokuwa wakila. Naye akawakaripia kwa kutokuwa na imani. Walikuwa wakaidi na walikataa kuwaamini wale waliomwona Yesu baada ya kufufuka kwake.

15 Naye akawaambia, “Nendeni ulimwenguni pote, na mkahubiri Habari Njema kwa uumbaji wote. 16 Yeyote atakayeamini na kubatizwa ataokolewa, lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa. 17 Na wale waaminio wataweza kufanya ishara hizi kama uthibitisho: watafukuza mashetani kwa jina langu; watasema kwa lugha mpya wasizojifunza bado; 18 watakamata nyoka kwa mikono yao; na ikiwa watakunywa sumu yoyote, haitawadhuru; wataweka mikono yao kwa wagonjwa, nao watapona.”

Yesu Arudi Mbinguni

(Lk 24:50-53; Mdo 1:9-11)

19 Hivyo baada ya Bwana Yesu kuzungumza nao, alichukuliwa mbinguni, kuketi katika mkono wa kuume wa Mungu. 20 Na mitume wakatoka na kwenda kuhubiri kila mahali, na Bwana alifanya kazi pamoja nao akithibitisha kuwa ujumbe wao ni wa kweli kwa ishara zilizofuatana na mahubiri yao.

Footnotes

  1. 16:8 Kitabu kinaishia hapa katika nakala mbili za zamani za Kiyunani zilizopatikana. Nakala chache nyingine za baadaye zina mwisho huu mfupi: “Lakini mara wakampa maagizo yote Petro na wale waliokuwa pamoja naye. Kisha Yesu mwenyewe akawatuma watoke na kwenda mashariki na magharibi wakiwa na ujumbe mtakatifu ambao kamwe hautabadilika; kwamba watu wataokolewa milele.”