Luka 16:19-31
Neno: Bibilia Takatifu
Mfano Wa Tajiri Na Maskini Lazaro
19 Akasema, “Palikuwa na tajiri mmoja aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, nguo za gharama kubwa, kila siku. 20 Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima, alikuwa akiletwa mlangoni kwa huyo tajiri kila siku. 21 Lazaro alikuwa akitamani kula makombo yaliyodondoka mezani kwa tajiri. Hata mbwa walikuwa wakiramba vidonda vyake.
22 “Hatimaye, yule maskini alikufa. Malaika wakamchukua akakae pamoja na Ibrahimu mbinguni. Yule tajiri naye pia akafa, akazikwa. 23 Alipokuwa kuzimuni ambapo alikuwa akiteseka, alita zama juu, akamwona Ibrahimu kwa mbali na Lazaro karibu yake. 24 Akaita, ‘Baba Ibrahimu, nionee huruma umtume Lazaro achovye japo ncha ya kidole chake katika maji aupoze ulimi wangu maana ninateseka kwenye moto huu.’ 25 Lakini Ibrahimu akamjibu, ‘Mwa nangu, kumbuka kwamba ulipokuwa hai ulipata kila kitu kizuri uli chotaka, ambapo Lazaro alipokea mabaya. Lakini sasa anafarijika hapa na wewe unateseka. 26 Isitoshe, kati yetu na ninyi huko, kumewekwa bonde kubwa lisilopitika ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko au kutoka huko kuja huku wasiweze.’ 27 Akasema, ‘Basi, baba, tafadhali umtume Lazaro aende nyumbani kwa baba yangu, 28 awaonye ndugu zangu, wasije wao pia wakaletwa mahali hapa pa mateso watakapokufa.’ 29 Ibrahimu akamjibu, ‘Ndugu zako wanazo sheria za Musa na maandiko ya Manabii. Itawapasa watii hayo.’ Lakini yule tajiri akazidi kumsihi, 30 ‘Hapana baba Ibrahimu, ndugu zangu hawatashawishiwa na hayo. Lakini mtu kutoka kuzimu akitumwa kwao watatubu na kuziacha dhambi zao.’
31 “Ibrahimu akamwambia, ‘Wasiposikiliza na kutii sheria za Musa na Maandiko ya manabii, hawatashawishika kutubu hata kama mtu akifufuka kutoka kuzimu.”’
Read full chapterCopyright © 1989 by Biblica