Add parallel Print Page Options

Msiwe Kama Mafarisayo

12 Maelfu wengi wa watu walikusanyika. Walikuwepo watu wengi sana kiasi ambacho walikuwa wakikanyagana. Kabla Yesu hajaanza kuzungumza na watu wale, aliwaambia wafuasi wake, “Iweni waangalifu dhidi ya chachu ya Mafarisayo. Ninamaanisha kuwa hao ni wanafiki. Kila kitu kilichofichwa kitawekwa wazi, na kila kitu kilicho sirini kitajulikana. Mnachokisema sirini kitasemwa mbele za watu. Na mliyonong'onezana katika vyumba vyenu, yatahubiriwa sehemu za wazi ambako kila mtu atasikia.”

Mwogopeni Mungu, Siyo Watu

(Mt 10:28-31)

Kisha Yesu akawaambia watu, “Ninawaambia ninyi, rafiki zangu, msiwaogope watu. Wanaweza kuua mwili, lakini baada ya hilo hawawezi kufanya chochote cha kuwaumiza. Mwogopeni Mungu maana Yeye ndiye mwenye nguvu ya kuwaua na kuwatupa Jehanamu. Ndiyo, mnapaswa kumwogopa yeye.

Ndege wanapouzwa, ndege watano wadogo wanagharimu senti mbili tu za shaba. Lakini Mungu hasahau hata mmoja wao. Ndiyo, Mungu anajua hata idadi ya nywele mlizonazo kwenye vichwa vyenu. Msiogope ninyi ni wa thamani kuliko ndege wengi.

Msiionee Haya Imani Yenu

(Mt 10:32-33; 12:32; 10:19-20)

Ninawaambia, mkinikiri mbele za watu, ndipo nami[a] nitakiri kuwa ninyi ni wangu mbele za Mungu na malaika. Na atakayenikataa mimi mbele za watu, nami nitamkataa mbele za Mungu na malaika.

10 Kila asemaye neno kinyume na Mwana wa Adamu atasamehewa. Lakini atakayesema kinyume na Roho Mtakatifu hatasamehewa.

11 Watakapowapeleka ninyi katika masinagogi mbele ya viongozi na wenye mamlaka, msihangaike mtasema nini. 12 Roho Mtakatifu atawafundisha wakati huo huo mnachopaswa kusema.”

Yesu Aaonya Kuhusu Ubinafsi

13 Mmoja wa watu katika kundi akamwambia Yesu, “Mwalimu, baba yetu amefariki hivi karibuni na ametuachia vitu, mwambie kaka yangu anigawie baadhi ya vitu hivyo!”

14 Lakini Yesu akamwambia, “Nani amesema mimi ni mwamuzi wa kuwaamulia namna ya ninyi wawili kugawana vitu vya baba yenu?” 15 Ndipo Yesu akawaambia, “Iweni waangalifu na jilindeni dhidi ya kila aina ya ulafi. Maana uhai wa watu hautokani na vitu vingi wanavyomiliki.”

16 Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Alikuwepo tajiri mmoja aliyekuwa na shamba. Shamba lake lilizaa mazao sana. 17 Akasema moyoni mwake, ‘Nitafanya nini? Sina mahali pa kuyaweka mazao yangu yote?’

18 Kisha akasema, ‘Ninajua nitakachofanya. Nitabomoa ghala zangu na kujenga ghala kubwa zaidi! Nitahifadhi nafaka zangu zote na vitu vingine vizuri katika ghala zangu mpya. 19 Kisha nitajisemea mwenyewe, nina vitu vingi vizuri nilivyotunza kwa ajili ya kutumia kwa miaka mingi ijayo. Pumzika, kula, kunywa na furahia maisha!’

20 Lakini Mungu akamwambia yule mtu, ‘Ewe mpumbavu! Leo usiku utakufa. Sasa vipi kuhusu vitu ulivyojiandalia? Nani atavichukua vitu hivyo?’

21 Hivi ndivyo itakavyokuwa kwa mtu anayeweka vitu kwa ajili yake yeye peke yake. Mtu wa namna hiyo si tajiri kwa Mungu.”

Utangulizeni Kwanza Ufalme wa Mungu

(Mt 6:25-34,19-21)

22 Yesu akawaambia wafuasi wake, “Hivyo ninawaambia, msisumbuke juu ya vitu mnavyohitaji kwa ajili ya kuishi, mtakula nini au mtavaa nini. 23 Maisha ni muhimu zaidi ya chakula mnachokula na mwili ni zaidi ya mavazi mnayovaa. 24 Waangalieni kunguru, hawapandi, hawavuni au kuweka katika majumba au ghala, lakini Mungu huwalisha. Ninyi ni wa thamani sana kuliko ndege. 25 Hakuna mmoja wenu anayeweza kujiongezea muda katika maisha yake kwa kujihangaisha na maisha. 26 Na ikiwa hamwezi kufanya mambo madogo, kwa nini mnajihangaisha kwa mambo makubwa?

27 Yatafakarini maua yanavyoota. Hayafanyi kazi wala kujitengenezea mavazi. Lakini ninawaambia hata Sulemani, mfalme mkuu na tajiri, hakuvikwa vizuri kama maua haya. 28 Ikiwa Mungu huyavika vizuri namna hii majani ya porini, mnadhani atawafanyia nini ninyi? Hilo ni jani tu, siku moja li hai na siku inayofuata linachomwa moto. Lakini Mungu huyajali kiasi cha kuyapendezesha. Hakika atafanya zaidi kwa ajili yenu. Imani yenu ni ndogo!

29 Hivyo daima msijihangaishe na kile mtakachokula ama mtakachokunywa. Msisumbukie mambo haya. 30 Hayo ndiyo mambo ambayo watu wote wasiomjua Mungu huyafikiria daima. Lakini Baba yenu anajua ya kuwa mnayahitaji mambo haya. 31 Mnapaswa kufikiri kuhusu ufalme wa Mungu. Naye Mungu atawapa mambo mengine yote mnayohitaji.

Msitumainie Fedha

32 Msiogope, enyi kundi dogo. Kwa kuwa imempendeza Baba yenu kuwapa ninyi ufalme wake. 33 Uzeni vitu mlivyo navyo, wapeni fedha wale wanaohitaji. Hii ni njia pekee mnayoweza kufanya utajiri wenu usipotee. Mtakuwa mnaweka hazina isiyoisha mbinguni, mahali ambapo wezi hawawezi kuiba na hakuna wadudu wa kuharibu. 34 Kwa kuwa mahali ilipo hazina yako, ndipo roho yako itakapokuwa.

Iweni Tayari Daima

(Mt 24:42-44)

35 Iweni tayari! Vaeni kikamilifu na taa zenu zikiwaka. 36 Iweni tayari kama watumishi wanaomngojea bwana wao anayerudi kutoka kwenye sherehe ya harusi. Bwana wao anaporudi na kubisha mlangoni, watumishi huweza kumfungulia mlango haraka. 37 Bwana wao atakapoona kuwa wako tayari na wanamsubiri, itakuwa siku ya furaha kwa watumishi hao. Ninawaambia bila mashaka, bwana wao atavaa nguo, atawakaribisha kwenye chakula kisha atawahudumia. 38 Watumishi hao wanaweza kumsubiri bwana wao mpaka usiku wa manane. Lakini watafurahi sana kwa sababu aliporudi aliwakuta bado wanamsubiri.

39 Mwenye nyumba angefanya nini ikiwa angejua ni lini mwizi atakuja? Mnajua kuwa asingeruhusu mwizi akavunja na kuingia ndani. 40 Hivyo, iweni tayari ninyi nanyi, kwa kuwa Mwana wa Adamu atakuja wakati msiotarajia!”

Mtumwa Mwaminifu ni Yupi?

(Mt 24:45-51)

41 Petro akasema, “Bwana, mfano ule ulikuwa kwa ajili yetu au kwa ajili ya watu wote?”

42 Bwana akamjibu, “Fikiria kuhusu mtumishi mwenye hekima na mwaminifu, ambaye bwana wake anamwamini na kumweka kuwa msimamizi wa kuwapa watumishi wengine chakula kwa wakati uliokubalika? Mtumishi huyo ataoneshaje kuwa yeye ni msimamizi makini na anayeweza kujisimamia? 43 Mkuu[b] wake atakaporudi na kumkuta akifanya kazi aliyompa, siku hiyo itakuwa siku ya furaha sana kwa mtumishi huyo. 44 Ninawaambia ukweli bila mashaka yo yote, mkuu wake atamweka kuwa msimamizi wa vitu vyake vyote anavyomiliki.

45 Lakini itakuwaje ikiwa mtumishi huyo ni mwovu na akadhani bwana wake hatarudi mapema? Ataanza kuwapiga watumishi wengine, wanaume na wanawake. Atakula na kunywa mpaka atalewa. 46 Ndipo bwana wa mtumishi huyo atakuja wakati usiotarajiwa, wakati ambapo mtumishi hajajiandaa. Ataadhibiwa bila huruma[c] na bwana wake na kumpeleka anakostahili, mahali waliko watumishi wengine wasiotii.

47 Mtumishi huyo alijua kitu ambacho bwana wake alimtaka afanye. Lakini hakuwa tayari kufanya au kujaribu kufanya kile bwana wake alichotaka. Hivyo mtumishi huyo ataadhibiwa sana! 48 Lakini vipi kuhusu mtumishi asiyejua kile ambacho bwana wake anataka? Yeye pia anafanya mambo yanayostahili adhabu, lakini ataadhibiwa kidogo kuliko mtumishi aliyejua alichotakiwa kufanya. Yeyote aliyepewa vingi atawajibika kwa vingi. Hivyo vingi vitategemewa kutoka kwa yule aliyepewa vingi zaidi.”

Kumfuata Yesu Kunaleta Matatizo

(Mt 10:34-36)

49 Yesu aliendelea kusema: “Nimekuja kuleta moto ulimwenguni. Ninatamani ungekuwa unawaka tayari! 50 Kuna aina ya ubatizo[d] ambao ni lazima niupitie na niteseke. Ninajisikia kusumbuka mpaka pale utakapotimizwa. 51 Mnadhani nilikuja kuleta amani ulimwenguni? Hapana, nilikuja kuugawa ulimwengu! 52 Kuanzia sasa, familia ya watu watano itagawanyika, watatu watakuwa kinyume cha wawili, na wawili kinyume cha watatu.

53 Kina baba watakuwa kinyume cha wana wao:
    na wana nao watakuwa kinyume cha baba zao.
Kina mama watakuwa kinyume cha binti zao:
    na binti nao watakuwa kinyume cha mama zao.
Mama wakwe watakuwa kinyume cha wake za wana wao,
    na wake za wana wao watakuwa kinyume cha mama wakwe zao.”[e]

Kuzielewa Nyakati

(Mt 16:2-3)

54 Ndipo Yesu akawaambia watu, “Mnapoona wingu likikua upande wa magharibi, mnasema, ‘Mvua inakuja,’ na muda si mrefu huanza kunyesha. 55 Mnapoona upepo unaanza kuvuma kutoka kusini mnasema, ‘Kutakuwa joto,’ na huwa hivyo. 56 Enyi wanafiki! Mnaweza kuiona nchi na anga na mkajua hali ya hewa itakavyokuwa. Kwa nini hamwelewi kinachotokea sasa?

Malizeni Matatizo Yenu

(Mt 5:25-26)

57 Kwa nini ninyi wenyewe hamwezi kujiamulia ninyi wenyewe kilicho haki? 58 Ikiwa mtu anakushtaki na ninyi nyote mnaongozana kwenda mahakamani. Jitahidi kadri inavyowezekana kupatana naye mkiwa njiani. Usipopatana naye, atakupeleka kwa hakimu. Na hakimu atakutia hatiani na maofisa wa mahakama watakutupa gerezani. 59 Ninawaambieni, hautatoka humo, mpaka ulipe kila senti unayodaiwa.”

Footnotes

  1. 12:8 nami Kwa maana ya kawaida, “Mwana wa Mtu” (Yesu Kristo).
  2. 12:43 Mkuu Yaani, “bwana wake”. Si Bwana ikimaanisha Yesu Kristo.
  3. 12:46 Ataadhibiwa bila huruma Kwa maana ya kawaida, “Kukatwa nusu”.
  4. 12:50 ubatizo Neno hili ambalo maana yake ni kuzamishwa katika maji, limetumika hapa likiwa na maana maalumu ya tofauti, yaani kufunikwa au “kuzikwa” katika matatizo.
  5. 12:53 Tazama Mik 7:6.