Add parallel Print Page Options

Zakayo

19 Yesu alikuwa anasafiri kupitia katika mji wa Yeriko. Katika mji wa Yeriko alikuwepo mtu aliyeitwa Zakayo. Alikuwa mtoza ushuru mkuu na alikuwa tajiri. Alitaka kumwona Yesu na watu wengine wengi walitaka kumwona Yesu pia. Lakini alikuwa mfupi na hakuweza kuona juu ya watu. Hivyo alikimbia akaenda mahali alipojua kuwa Yesu angepita. Kisha akapanda mkuyu ili aweze kumwona Yesu.

Yesu alipofika mahali alipokuwa Zakayo, alitazama juu na kumwona akiwa kwenye mti. Yesu akasema, “Zakayo, shuka upesi! Ni lazima nikae nyumbani mwako leo.”

Zakayo alishuka chini haraka. Alifurahi kuwa na Yesu nyumbani mwake. Kila mtu aliliona hili na watu wakaanza kulalamika, wakisema, “Tazama aina ya mtu ambaye Yesu anakwenda kukaa kwake. Zakayo ni mwenye dhambi!”

Zakayo akamwambia Bwana, “Sikiliza Bwana nitawapa maskini nusu ya pesa zangu. Ikiwa nilimdhulumu mtu yeyote, nitamrudishia mara nne zaidi.”

Yesu akasema, “Leo ni siku kwa ajili ya familia hii kuokolewa kutoka katika dhambi. Ndiyo, hata mtoza ushuru huyu ni mmoja wa wateule wa Mungu.[a] 10 Mwana wa Adamu alikuja kuwatafuta na kuwaokoa watu waliopotea.”

Simulizi Kuhusu Watumishi Watatu

(Mt 25:14-30)

11 Kundi la watu walipokuwa bado wanamsikiliza Yesu akizungumza mambo haya. Akaongeza kwa kuwasimulia simulizi hii. Na sasa alikuwa karibu na mji wa Yerusalemu na watu walidhani kuwa ufalme wa Mungu ulikuwa unakwenda kutokea haraka. 12 Akasema, “Mtu mmoja maarufu alikuwa anajiandaa kwenda katika nchi ya mbali kutawazwa kuwa mfalme. Kisha arudi nyumbani na kuwatawala watu wake. 13 Hivyo aliwaita watumishi wake kumi kwa pamoja. Akampa kila mtumishi fungu la pesa.[b] Akamwambia kila mtumishi, ‘Zifanyie biashara pesa hizi mpaka nitakaporudi.’ 14 Lakini watu katika ule ufalme walikuwa wanamchukia mtu huyu na hivyo walituma kundi la watu kwenda katika nchi nyingine. Walipofika huko wakasema, ‘Hatutaki mtu huyu awe mfalme wetu.’

15 Lakini mtu yule akatawazwa kuwa mfalme. Aliporudi nyumbani, akaagiza akasema, ‘Waiteni wale watumishi wenye pesa zangu. Ninataka kujua wamezalisha kiasi gani kutokana na pesa hizo.’ 16 Mtumishi wa kwanza alikuja na akasema, ‘Mkuu, nilizalisha mafungu kumi ya pesa kutokana na fungu moja ulilonipa.’ 17 Mfalme akamwambia, ‘Vizuri sana! Wewe ni mtumishi mwema. Nilikuamini kwa vitu vidogo, lakini sasa utakuwa mtawala wa miji yangu kumi.’

18 Mtumishi wa pili akasema, ‘Mkuu, kwa fungu moja la pesa zako, nilizalisha mafungu matano.’ 19 Mfalme akamwambia mtumishi huyu, ‘Utatawala miji yangu mitano.’

20 Kisha mtumishi mwingine akaingia na akasema, ‘Mkuu, fungu lako la pesa hili hapa. Nilizifunga katika kipande cha nguo na kulificha. 21 Niliogopa kwa sababu wewe ni mgumu. Unachukua hata pesa ambazo hukuzizalisha na kukusanya chakula ambacho hukupanda.’

22 Kisha mfalme akamwambia, ‘Wewe ni mtumishi mbaya! Nitatumia maneno yako mwenyewe kukuhukumu. Unasema kuwa mimi ni mtu mgumu, ninachukua hata pesa ambazo sikuzizalisha na nakusanya chakula ambacho sikupanda? 23 Ikiwa hiyo ni kweli, ulipaswa kuweka pesa zangu kwa watoao riba. Ili nitakaporudi pesa hiyo iwe imezalisha faida.’ 24 Kisha mfalme akawaambia watu waliokuwa pale, ‘Mnyang'anyeni mtumishi huyu fungu la pesa na mpeni mtumishi aliyezalisha mafungu kumi ya pesa.’

25 Lakini watu wakamwambia mfalme, ‘Mkuu, yule mtumishi ana mafungu kumi tayari.’

26 Mfalme akasema, ‘Waliozalisha faida watapata zaidi. Lakini ambao hawakuzalisha faida watanyang'anywa kila kitu. 27 Sasa, adui zangu wako wapi? Wako wapi watu ambao hawakutaka niwe mfalme? Waleteni adui zangu hapa na waueni huku nikiangalia wanavyokufa.’”

Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme

(Mt 21:1-11; Mk 11:1-11; Yh 12:12-19)

28 Baada ya Yesu kusema mambo haya, aliendelea kusafiri kuelekea Yerusalemu. 29 Akakaribia Bethfage na Bethania, miji iliyo karibu na kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. Kisha akawatuma wawili miongoni mwa wafuasi wake, 30 akawaambia, “Nendeni kwenye mji mnaoweza kuuona pale. Mtakapoingia mjini, mtamwona mwanapunda amefungwa ambaye bado mtu yeyote hajampanda. Mfungueni na mleteni hapa kwangu. 31 Kama mtu yeyote akiwauliza, ‘Kwa nini mnamfungua?’ Semeni, ‘Bwana anamhitaji.’”

32 Wafuasi wawili wakaenda kwenye mji ule. Wakamwona punda kama Yesu alivyowaambia. 33 Wakamfungua, lakini wamiliki wa punda wakatoka. Wakawauliza wafuasi wa Yesu, “Kwa nini mnamfungua punda wetu?”

34 Wafuasi wakajibu, “Bwana anamhitaji.” 35 Hivyo wafuasi wakampeleka punda kwa Yesu. Wakatandika baadhi ya nguo zao juu ya mwanapunda, kisha wakampandisha Yesu juu yake. 36 Yesu akaanza kwenda Yerusalemu. Wafuasi walikuwa wanatandaza nguo zao njiani mbele yake.

37 Yesu alipokaribia Yerusalemu. Alipokuwa katika njia inayotelemka kutoka kwenye Mlima wa Mizeituni, kundi lote la wafuasi wake wakaanza kumsifu Mungu kwa kupaza sauti. Walimsifu Mungu kwa furaha kwa sababu ya miujiza yote waliyoiona. 38 Walisema,

“Karibu! Mungu ambariki mfalme
    ajaye kwa jina la Bwana!(A)
Amani iwe mbinguni,
    na utukufu kwa Mungu!”

39 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika kundi wakamwambia Yesu, “Mwalimu, waambie wafuasi wako wasiseme mambo haya!”

40 Lakini Yesu akawajibu, “Ninawaambia ikiwa wafuasi wangu wasingesema, mawe haya yangesema kwa kupaza sauti!”

Yesu Aulilia Mji wa Yerusalemu

41 Yesu alipoukaribia mji wa Yerusalemu, akautazama kisha akaanza kuulilia, 42 akisema, “Laiti ungelijua leo kile kinachokuletea amani. Lakini kimefichwa kwako usikijue sasa. 43 Wakati unakuja, ambao adui zako watajenga ukuta kukuzunguka na kukuzingira pande zote. 44 Watakuteketeza wewe na watu wako wote. Hakuna jiwe hata moja katika majengo yako litaachwa juu ya jiwe jingine. Haya yote yatatokea kwa sababu hukujua wakati ambao Mungu alikuja kukuokoa.”

Yesu Asafisha Eneo la Hekalu

(Mt 21:12-17; Mk 11:15-19; Yh 2:13-22)

45 Yesu aliingia katika eneo la Hekalu. Akaanza kuwafukuza watu waliokuwa wanauza vitu humo. 46 Akasema, “Maandiko yanasema, ‘Hekalu langu litakuwa nyumba ya sala.’(B) Lakini mmeligeuza kuwa ‘maficho ya wezi.’”(C)

47 Yesu aliwafundisha watu kila siku katika eneo la Hekalu. Viongozi wa makuhani, walimu wa sheria na baadhi ya viongozi wa watu walikuwa wakitafuta namna ya kumwua. 48 Lakini hawakujua namna ambavyo wangefanya, kwa sababu alikuwa anazungukwa na watu kila wakati waliokuwa wakimsikiliza. Kila mtu alifurahia yale ambayo Yesu alikuwa anasema, hawakuacha kumsikiliza.

Footnotes

  1. 19:9 mmoja wa wateule wa Mungu Kwa maana ya kawaida, “mwana wa Ibrahimu”.
  2. 19:13 fungu la pesa Fungu moja la pesa kwa Kiyunani liliitwa mina, ambayo ni sarafu 100 za fedha, uliotosha kumlipa mtu mshahara kwa miezi mitatu. Pia katika mstari wa 16,18,20,24 na 25.