Add parallel Print Page Options

Rafiki wapendwa, tuna ahadi hizi toka kwa Mungu. Hivyo tujitakase maisha yetu na kuwa huru kutoka kwa kila kinachofanya miili yetu ama roho zetu kuwa najisi. Heshima yetu kwa Mungu itufanye tujaribu kuwa watakatifu kabisa kwa namna tunavyoishi.

Furaha ya Paulo

Fungueni mioyo yenu kwetu. Hatujamtendea vibaya wala kumwumiza mtu yeyote. Na hatujamdanganya mtu yeyote. Sisemi haya kuwalaumu. Nimekwishawaeleza kuwa tunawapenda sana kiasi kwamba hakuna chochote katika maisha ama katika kifo kitakachotutenganisha na ninyi. Ninajisikia kwamba ninaweza kuwaambia lolote. Ninajivunia sana ninyi. Licha ya matatizo yote tuliyoyapata, nimetiwa moyo sana na ninajisikia kuwa mwenye furaha sana.

Tulipokuja Makedonia, hatukupumzika. Tulisumbuliwa kwa kila namna. Tulikuwa na vita kwa nje na hofu ndani yetu. Lakini Mungu huwapa moyo wale wanaosumbuliwa, na kwa hakika na sisi alitupa moyo kwa kumleta Tito kwetu. Ilikuwa furaha kumwona, lakini tulitiwa moyo zaidi tuliposikia jinsi nanyi mlivyomtia moyo yeye pia. Naye alitueleza kuwa mlikuwa na shauku ya kuniona mimi na kwamba mnayajutia yale mlivyofanya. Na akatueleza jinsi mlivyokuwa na shauku ya kusimama upande wangu. Niliposikia hili, nilifurahishwa sana.

Hata kama barua nilyowaandikieni iliwahuzunisha, sijutii kuiandika. Nafahamu kuwa barua ile iliwatia huzuni, ninasikitika kwa hilo. Lakini iliwapa huzuni kwa muda mfupi. Sasa ninafurahi, si kwa sababu mlipata huzuni, bali kwa sababu huzuni yenu iliwasababisha mkaamua kubadilika. Hilo ndilo ambalo Mungu alilitaka, hivyo hatukuwaumiza kwa namna yo yote. 10 Aina ya huzuni ambayo Mungu anaitaka inawafanya watu waamue kubadili maisha yao. Hili linawaelekeza kwenye wokovu, nasi hatuwezi kulijutia hilo. Lakini huzuni dunia huleta mauti. 11 Mlikuwa na huzuni ambayo Mungu alitaka muwe nayo. Sasa mmetambua kile ambacho huzuni hiyo imewaletea: Imewafanya muwe makini sana. Imewafanya mtafute kuthibitisha kuwa hamkufanya makosa. Iliwafanya mkasirike na mwogope. Imewafanya muwe na shauku ya kuniona. Imewafanya muwe na azma ya kufanya kile nilichowaagiza. Imewafanya muwe na shauku ya kuona kuwa haki inatendeka. Mlithibitisha kuwa hamkuwa na hatia katika sehemu yoyote ya tatizo hilo. 12 Sababu kubwa ya kuandika barua ile haikuwa kwa sababu ya yule aliyefanya kosa au aliyeumia. Niliandika ili mtambue, mbele za Mungu, jinsi mnavyotujali sana sisi. 13 Na hili ndilo lililokuwa faraja kwetu sisi.

Tulitiwa moyo sana, lakini hasa tulifurahishwa kuona jinsi Tito alivyokuwa mwenye furaha. Ninyi nyote mlimfanya apate utulivu moyoni. 14 Nilijisifu juu yenu kwake Tito, na ninyi hamkuniaibisha. Siku zote tumewaambia ninyi kweli, na sasa yale tuliyomwambia Tito kwa habari zenu yamedhihirika kuwa ni kweli. 15 Na upendo wake kwenu una nguvu anapokumbuka kuwa mlikuwa tayari kutii. Mlimpokea kwa heshima na hofu. 16 Ninafuraha sana kwa kuwa ninaweza kuwaamini kikamilifu.