Add parallel Print Page Options

Sisi ni watenda kazi pamoja na Mungu. Hivyo tunawasihi: Neema mliyoipokea kutoka kwa Mungu iwe na manufaa kwenu. Mungu anasema,

“Nilikusikia kwa wakati sahihi,
    na nikakusaidia siku ya wokovu.”(A)

Ninawaambia kwamba “wakati uliokubalika” ni huu sasa. Na “Siku ya wokovu” ni leo.

Hatutaki watu waone makosa katika kazi yetu. Hivyo hatutendi jambo lolote litakalokuwa kikwazo kwa wengine. Lakini kwa kila njia tunaonesha kuwa sisi ni watumishi wa Mungu. Hatukati tamaa, ingawa tunakutana na matatizo, mambo magumu na matatizo ya kila namna. Tumepigwa na kutupwa gerezani. Watu wameanzisha fujo dhidi yetu. Tumefanya kazi kwa bidii, mara nyingi pasipo kula ama kulala. Tunadhihirisha kuwa sisi tu watumishi wa Mungu kutokana na maisha yetu safi, kwa ufahamu wetu, kwa subira yetu na kwa upole wetu. Tunadhihirisha hilo kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo wetu wa kweli, kwa kusema iliyo kweli, na kwa kuzitegemea nguvu za Mungu. Njia hii iliyo sahihi ya kuishi imetuandaa kujitetea wenyewe kinyume na kila aina ya shambulizi.

Baadhi ya watu wanatuheshimu, lakini wengine wanatudhihaki. Wengine wanasema mema juu yetu, lakini wengine wasema mabaya juu yetu. Wengine wanatusema kuwa tu waongo, lakini tunasema kweli. Kwa wengine hatufahamiki, lakini twajulikana sana. Tunaonekana kama watu wanaostahili kufa, lakini angalia! Twadumu kuishi. Tunaadhibiwa, lakini hatuuawi. 10 Tuna huzuni nyingi, lakini tunafuraha kila siku. Tu maskini, lakini tunawafanya watu wengi kuwa matajiri katika imani. Hatuna kitu, lakini tunakila kitu.

11 Tumesema kwa uhuru kwenu ninyi watu wa Korintho. Tumefungua mioyo yetu kwenu. 12 Upendo wetu kwenu haujakoma. Ninyi ndiyo mliouzuia upendo wenu kwetu. 13 Ninawaambia kama watoto wangu. Fanyeni vivyo hivyo kama sisi tulivyotenda kwenu; fungueni mioyo yenu pia.

Sisi ni Hekalu la Mungu

14 Ninyi hamko sawa na wale wasioamini. Hivyo msifungwe nira pamoja nao. Wema na ubaya havikai pamoja. Nuru na giza haviwezi kukaa pamoja katika chumba kimoja. 15 Itawezekanaje kuwe na mapatano kati ya Kristo na beliali?[a] Je, mwamini anashirika gani na asiye amini? 16 Hekalu la Mungu halina mapatano yoyote na sanamu, na sisi tu hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu anavyosema,

“Nitakaa kati yao
    na kutembea nao;
Nitakuwa Mungu wao,
    na watakuwa watu wangu.”(B)
17 “Hivyo tokeni nje kati yao
    na jitengeni nao, asema Bwana.
Msishike chochote kilicho kichafu,
    nami nitawakaribisha.”(C)
18 “Nitakuwa baba yenu,
    nanyi mtakuwa wana wangu na binti zangu,
    asema Bwana Mwenyezi.”(D)

Footnotes

  1. 6:15 beliali Kwa maana ya kawaida, “beliali”, mojawapo ya neno la Kiebrania “belial”, inamaana ya “kutokustahili” na lilitumika kumlenga Shetani au adui wa Kristo.