Add parallel Print Page Options

Hazina ya kiroho katika Vyungu vya Udongo

Mungu, kwa rehema zake, alitupa sisi huduma hii ili tuifanye, hivyo hatukati tamaa. Lakini tumekataa mambo ya aibu ya siri. Hatumdanganyi mtu yeyote, na hatuyabadilii mafundisho ya Mungu. Tunaifundisha kweli wazi wazi. Na hivi ndivyo watu wanaweza kutambua mioyoni mwao sisi ni watu wa namna gani mbele za Mungu. Habari Njema tunazowahubiri watu hazijafichika kwa yeyote isipokuwa kwa waliopotea. Mtawala[a] wa dunia hii amezitia giza akili za wasioamini. Hawawezi kuona nuru ya Habari Njema; ujumbe juu ya uungu wa Kristo, taswira halisi ya Mungu. Hatuwaambii watu habari zetu wenyewe. Lakini tunawaambia habari za Kristo Yesu kuwa ni Bwana, na tunawaambia kuwa sisi ni watumwa wenu kwa ajili ya Yesu. Kuna wakati Mungu alisema, “Na nuru ing'ae gizani”[b] na huyu ni Mungu yule yule anayesababisha nuru ing'ae katika mioyo yetu ili tutambue utukufu wa uungu wake mkuu unaongaa katika sura ya Kristo.

Tuna hazina hii kutoka kwa Mungu, lakini sisi ni kama vyombo vya udongo tu vinavyobeba hazina. Hii ni kuonesha kuwa nguvu ya kustaajabisha tuliyo nayo inatoka kwa Mungu, si kwetu. Tunasumbuliwa kila upande, lakini hatushindwi. Mara kwa mara hatujui tufanye nini, lakini hatukati tamaa. Tunateswa, lakini Mungu hatuachi. Tunaangushwa chini wa nyakati zingine, laki hatuangamizwi. 10 Hivyo tunashiriki kifo cha Yesu katika miili yetu kila wakati, lakini haya yanatokea ili uzima wa Yesu udhihirishwe katika miili yetu. 11 Tuko hai, lakini kwa ajili ya Yesu tupo katika hatari ya kifo kila wakati, ili kwamba uzima wa Yesu udhihirishwe katika miili yetu ya kufa. 12 Kwa hiyo kifo kinafanya kazi ndani yetu, lakini matokeo yake ni kwamba uzima unafanya kazi ndani yenu.

13 Maandiko yanasema, “Niliamini, hivyo nikasema.”(A) Tuna Roho huyo huyo anayetupa imani kama hiyo. Tunaamini, na hivyo tunasema pia. 14 Mungu alimfufua Bwana Yesu kutoka kwa wafu, nasi tunajua kuwa atatufufua pamoja na Yesu. Mungu atatukusanya pamoja nanyi, na tutasimama mbele zake. 15 Mambo yote haya ni kwa ajili yenu. Na hivyo neema ya Mungu inatolewa kwa watu wengi zaidi na zaidi. Hili litaleta shukrani nyingi zaidi na utukufu kwa Mungu.

Kuishi kwa Imani

16 Hii ndiyo sababu hatukati tamaa. Miili yetu inazidi kuzeeka na kuchoka, lakini roho zetu ndani zinafanywa upya kila siku. 17 Tuna masumbufu, lakini ni madogo na ni ya muda mfupi. Na masumbufu haya yanatusaidia kuupata utukufu wa milele ulio mkuu kuliko masumbufu yetu. 18 Hivyo twafikiri juu ya mambo tusiyoweza kuyaona, si tunayoona. Tunayoyaona ni ya kitambo tu, na yale tusiyoyaona yanadumu milele.

Footnotes

  1. 4:4 Mtawala Kwa maana ya kawaida, “Mungu”. Lakini usemi huu hapa unamaanisha “Shetani”.
  2. 4:6 Tazama Mwa 1:3.