Maono Ya Paulo Na Mwiba Aliokuwa Nao

12 Inanibidi nijisifu. Ingawa hakuna faida, nitawaeleza juu ya maono na mafunuo niliyopata kutoka kwa Bwana. Namfahamu mtu aliyekuwa ndani ya Kristo ambaye miaka kumi na minne iliyopita alijikuta katika mbingu ya tatu. Kama alikuwa katika mwili au katika roho mimi sijui, Mungu anajua. Na ninafahamu ya kuwa huyu mtu alijikuta yuko Paradiso, kama alikuwa katika mwili au katika roho mimi sijui, Mungu anajua. Naye alisikia mambo ambayo hayawezi kusimuliwa, ambayo mtu hawezi kuyatamka. Kwa niaba ya mtu huyu nitajisifu, lakini kwa ajili yangu mwenyewe sitajisifu isipokuwa kuhusu udhaifu wangu. Lakini ningependa kujisifu, sitakuwa mjinga kwa maana nitakuwa nasema kweli. Ila najizuia, ili mtu ye yote asije akaniona mimi kuwa bora zaidi kuliko ninavyoonekana katika yale ninayotenda na kusema.

Na ili nisijione bora kuliko nilivyo, kutokana na mafunuo haya makuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mtumishi wa she tani, ili anitese. Nimemsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uwezo wangu unakamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu ili uwezo wa Kristo ukae juu yangu. 10 Basi, kwa ajili ya Kristo, naridhika na udhaifu, mat usi, taabu, mateso na maafa; kwa maana ninapokuwa mdhaifu ndipo nina nguvu.

Upendo Wa Paulo Kwa Wakorintho

11 Nimekuwa mjinga, lakini ninyi mmenilazimisha niwe hivyo. Kwa kuwa ninyi ndio ambao mngenisifu. Kwa sababu sikuwa wa chini kuliko hawa “mitume wakuu,” hata ingawa mimi si kitu. 12 Mambo yanayomtambulisha mtume wa kweli, yaani ishara, miujiza na maaj abu, yalifanywa miongoni mwenu kwa uvumilivu wote. 13 Je, kuna kitu ambacho hamkupewa sawa na wengine, isipokuwa mimi sikuwa mzigo kwenu? Nisameheni kwa kosa hili.

14 Na sasa niko tayari kuwatembelea kwa mara ya tatu, nami sitahitaji msaada wenu kwa sababu sitaki mnipe mali yenu, ninaowahitaji ni ninyi. Kwa kuwa si sawa watoto waweke akiba kwa ajili ya wazazi wao bali wazazi waweke akiba kwa ajili ya watoto wao. 15 Nitafurahi kutumia kila nilicho nacho hata mwili wangu pia, kwa ajili yenu. Je kama nawapenda zaidi, mtanipenda kidogo tu kwa sababu hiyo? 16 Hata kama mnakubali kwamba sikuwa mzigo kwenu, wengine watasema nilikuwa mjanja nikawanasa kwa hila. 17 Je, niliwahi kuwadanganya kupitia mmojawapo wa hao watu nil iowatuma kwenu? 18 Nilimsihi Tito aje kwenu nikamtuma ndugu mwingine waje pamoja. Je, Tito aliwatoza cho chote? Je, sisi sote hatukutenda kwa kuongozwa na Roho mmoja na kufuata njia moja?

19 Pengine mnafikiri wakati wote kwamba sisi tunajaribu kujitetea mbele yenu. Sisi tunajitetea mbele ya Mungu katika Kristo, na yote haya ni kwa nia ya kuwajenga ninyi, wapendwa wetu. 20 Kwa maana nina hofu kwamba nitakapokuja nitawakuta hamko kama ambavyo ningependa muwe, na ninyi mtakuta siko kama ambavyo mngependa niwe. Nina hofu kwamba kati yenu huenda kuna ugomvi, wivu, hasira, ubinafsi, uzushi, usengenyaji, majivuno na machafuko. 21 Nina hofu kuwa nitakapokuja tena Mungu wangu ata ninyenyekeza mbele yenu, na huenda nikaomboleza kuhusu wengi wenu ambao walitenda dhambi na hawajatubu na kuacha hayo matendo machafu, uasherati na ufisadi ambao walikuwa wakitenda.