Paulo Atetea Huduma Yake

10 Mimi Paulo nawaandikia nikiwasihi kwa unyenyekevu na upole wa Kristo, mimi ambaye ni mpole ninapokuwa pamoja nanyi, lakini mwenye ujasiri nikiwa mbali nanyi! Nawaomba msinifanye niwe mkali nitakapofika kwenu, kama ninavyotarajia kuwa mkali kwa watu fulani, ambao wanadhani kwamba nafuata kawaida za dunia katika mwenendo wangu. Ingawa tunaishi duniani lakini hatupigani kama watu wa ulimwengu. Silaha zetu si za kidunia, bali silaha zetu zina nguvu ya kimungu iwezayo kubomoa ngome. Tunaharibu hoja na mabishano yaliyo kinyume cha kumjua Mungu. Tunateka mawazo yote na kuyafanya yamtii Kristo, na tutakuwa tayari kuadhibu uasi wo wote baada ya kuhakikisha utii wenu. Tazameni vizuri mambo yaliyo mbele ya macho yenu. Kama mtu ye yote anaamini kuwa yeye ni wa Kristo, basi ajiangalie tena, kwa maana na sisi pia ni wa Kristo kama yeye alivyo. Kwa sababu hata kama tunajivunia mno madaraka tuliyo nayo, ambayo Bwana ametupatia kwa ajili ya kuwa jenga na sio kuwagandamiza, sitaona haya kuyatumia. Sitaki ionekane kama nataka kuwatisha kwa barua zangu. 10 Kwa maana wengine wanasema, “Barua zake zina uzito na ni kali lakini mtu mwenyewe ni mdhaifu na kuzungumza kwake hakuvutii.” 11 Watu kama hao wajue ya kuwa, wanavyotuona katika barua tukiwa hatupo nanyi, ndivyo tulivyo, na ndivyo tutakavyofanya tutakapo kuwa pamoja nanyi. 12 Hatuthubutu kujiweka kwenye kundi moja au kujilinganisha na hao wanaojiona kuwa wao ni wa maana sana. Wana pojilinganisha wenyewe kwa wenyewe, wanaonyesha ya kuwa hawana busara. 13 Lakini sisi hatujajivuna kupita kiasi, bali majivuno yetu yatakuwa katika mipaka ambayo Mungu ametuwekea, na mipaka hiyo inawafikia hata na ninyi. 14 Kwa maana hatupiti mipaka tunapowajumlisha katika huduma yetu kwa sababu tulikuwa wa kwanza kuwaletea Injili ya Kristo. 15 Hatupiti mipaka na kujivunia kazi ya watu wengine. Lakini matumaini yetu ni kwamba, imani yenu inavyozidi kukua, huduma yetu kwenu itaendelea kupanuka, 16 ili tuweze kuhubiri Injili hata nchi zilizopakana nanyi, bila kujivu nia kazi iliyokwisha fanywa katika sehemu ya mtu mwingine. 17 “Anayejivuna na ajivune katika Bwana.” 18 Kwa maana sio mtu anayejisifu ambaye anapata kibali, bali ni mtu ambaye Bwana anamsifu.