Add parallel Print Page Options

Salamu kutoka kwa Paulo, Mtume wa Kristo Yesu.[a] Mimi ni mtume kwa sababu ndivyo Mungu alitaka. Na Timotheo ndugu yetu katika Kristo.

Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho na kwa watakatifu wote wa Mungu walio jimbo lote la Akaya.

Neema na Amani iwe kwenu kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.

Paulo Anamshukuru Mungu

Sifa na zimwendee Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye ni baba aliyejaa rehema, Mungu aliye mwingi wa faraja. Hutufariji kila wakati tunapokuwa katika hali ya matatizo ili wengine wawapo katika matatizo, tuweze kuwafariji kwa namna ile ile ambayo Mungu ametufariji sisi. Twashiriki katika mateso mengi ya Kristo. Na kwa namna hiyo hiyo, faraja nyingi hutujia kwa njia ya Kristo. Ikiwa tuko katika mateso, tuko kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu. Na ikiwa tunafarijika, ni kwa sababu tuweze kuwafariji ninyi. Hili huwasaidia katika kuyakubali mateso yale yale tunayopata kwa uvumilivu. Tumaini letu kwenu liko imara. Tunafahamu kuwa mnashiriki katika mateso yetu. Hivyo tunafahamu pia kuwa mnashiriki katika faraja yetu pia.

Ndugu zangu, tunapenda mfahamu juu ya mateso tuliyoyapata hapa Asia. Tulikuwa na mzigo sana huko, ulikuwa mzito kuliko hata nguvu zetu. Hata tulipoteza tumaini la kuishi. Ukweli ni kuwa, ilionekana kana kwamba Mungu alikuwa anatuambia kuwa tunakwenda kufa. Lakini haya yalitokea ili tusizitumainie nguvu zetu bali tumtumainie Mungu, ambaye huwainua watu toka mautini. 10 Yeye alituokoa toka katika hatari hizi kubwa za mauti, na ataendelea kutuokoa. Twajisikia kuwa na hakika kuwa ataendelea kutuokoa. 11 Nanyi mnaweza kutusaidia kwa njia ya maombi. Ndipo watu wengi wataweza kumshukuru Mungu kwa ajili yetu; kwamba Mungu alitubariki kutokana na maombi yao mengi.

Mabadiliko katika Mipango ya Paulo

12 Hili ndilo tunalojivunia, na naweza kusema kwa dhamiri safi kwamba ni kweli: Katika kila kitu tulichofanya duniani, Mungu ametuwezesha kukifanya kwa moyo safi. Na hili ni kweli zaidi katika yale tuliyowatendea ninyi. Tulifanya hivyo kwa neema ya Mungu, si kwa hekima ambayo ulimwengu unayo. 13 Tunawaandikia mambo mnayoweza kusoma na kuyaelewa. Na nina matumaini kuwa mtayaelewa inavyopasa 14 kama ambavyo tayari mmekwisha kuyafahamu mambo mengi kuhusu sisi. Natumaini mtaelewa kuwa mnaweza kuona fahari juu yetu, kama nasi tutakavyoona fahari juu yenu wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja.

15 Nilikuwa na uhakika sana juu ya haya yote. Ndiyo maana niliweka mpango wa kuwatembelea kwanza. Kisha mngebarakikwa mara mbili. 16 Nilipanga kuwatembelea nilipokuwa nikienda Makedonia na nilipokuwa ninarudi. Na nilipanga kuwaomba mniletee kutoka huko hadi Yudea chochote ambacho nilihitaji kwa ajili ya safari yangu. 17 Je! Mnadhani nilipanga mipango hii bila kufikiri? Au mnadhani ninafanya mipango kama vile dunia inavyofanya, lugha yetu kwenu si ndiyo na hapana kwa wakati mmoja.

18 Kama ambavyo kwa hakika mnaweza kumwamini Mungu, basi mnaweza kuamini kuwa lile tunalowaambia kamwe haliwezi kuwa ndiyo na hapana kwa pamoja. 19 Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, Yeye ambaye Sila, Timotheo, na mimi tuliwaeleza habari zake, hakutokea kuwa ni ndiyo na hapana kwa ahadi za Mungu. Kinyume chake ndiyo ya Mungu imethibitika daima katika Kristo kuwa ni ndiyo. 20 Ndiyo kwa ahadi zote za Mungu katika Kristo. Na hii ndiyo maana twasema “Amina” Katika Kristo kwa utukufu wa Mungu. 21 Na Mungu ndiye anayewafanya ninyi na sisi kuwa imara katika Kristo. Mungu pia ndiye aliyetuchagua kwa ajili ya kazi yake.[b] 22 Aliweka alama yake juu yetu ili kuonesha kuwa tu mali yake. Ndiyo, amemweka roho wake ndani ya mioyo yetu kama malipo ya awali yanayotuhakikishia mambo yote atakayotupa.

23 Ninawaambia hili, na ninamwomba Mungu awe shahidi wangu kuwa ni la kweli: Sababu iliyonifanya nisirudi tena Korintho ni kuwa nilitaka niepuke kuwapa karipio lenye nguvu. 24 Sina maana ya kuwa tunataka kuitawala imani yenu. Ninyi mpo imara katika imani. Lakini tunatenda kazi pamoja nanyi kwa ajili ya furaha yenu wenyewe.

Footnotes

  1. 1:1 Kristo Yesu Au “Mfalme Yesu”. Neno “Kristo” ni tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi”, ambao ni wadhifa wa kifalme. Tazama Mk 15:32: Lk 23:2. Tazama pia Kristo na Masihi katika Orodha ya Maneno.
  2. 1:21 aliyetuchagua … kazi yake Kwa maana ya kawaida, “alitupaka mafuta.” Kwa Kiyunani neno hili linahusiana na “Kristo” ambalo linatafsiriwa kama “mpakwa mafuta.” Tazama Kristo katika Orodha ya Maneno.