Add parallel Print Page Options

Msaada kwa Watu wa Mungu Katika Uyahudi

Na sasa, kaka na Dada zetu, tunataka kuwaambia kile ambacho neema ya Mungu imefanya katika makanisa ya makedonia. Waamini hawa wamepitia katika masumbufu makubwa, na ni maskini sana. Lakini furaha yao kubwa iliwafanya kuwa wakarimu zaidi katika kutoa kwao. Ninaweza kuwaambia kwamba walitoa kulingana na uwezo wao na hata zaidi ya uwezo wao. Hakuna mtu yeyote aliyewaambia kufanya hivyo. Hilo lilikuwa wazo lao. Walituuliza tena na tena na walitusihi tuwaruhusu kushiriki katika huduma hii kwa ajili ya watu wa Mungu. Na walitoa kwa namna ambayo sisi wenyewe hatukutegemea: kwanza walijitoa wenyewe kwa Mungu na kwetu kabla ya kutoa fedha zao. Hili ndilo Mungu anataka. Kwa hiyo tulimwomba Tito awasaidie ninyi kuikamilisha kazi hii maalum ya kutoa. Tito ndiye aliyeianzisha kazi hii kwanza miongoni mwenu. Ninyi ni matajiri kwa kila kitu; katika imani, katika uwezo wa kuzungumza, katika maarifa, katika utayari wa kusaidia kwa njia yo yote, na katika upendo mliojifunza kutoka kwetu. Hivyo sasa tunawataka muwe matajiri katika kazi hii ya kutoa pia.

Siwashurutishi ninyi kutoa, ila nataka niujaribu upendo wenu kuona ni wa kiasi gani kuwalinganisha na wengine ambao wamekuwa tayari na wana hiari ya kusaidia. Mnaifahamu neema ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mnafahamu kuwa aliacha utajiri wake mbinguni na kufanyika maskini kwa ajili yenu. Aliacha kila kitu ili ninyi mbarikiwe kwa wingi zaidi.

10 Hili ndilo ninafikiri mnapaswa kufanya: mwaka jana mlikuwa wa kwanza kutaka kutoa, na mkawa wa kwanza kutoa. 11 Hivyo sasa ikamilisheni kazi mliyoianzisha. Kisha kutenda kwenu kutakuwa sawa na “kutaka” kwenu “kutenda”. Toeni kutokana na kile mlicho nacho. 12 Ikiwa mnataka kutoa, sadaka yenu itapokelewa. Sadaka yenu itahukumiwa kutokana na kile mlicho nacho, si kwa kile msichonacho. 13 Hatupendi muwe na mizigo wakati wengine wanastarehe. Tunataka kila kitu kiwe katika hali ya usawa. 14 Wakati huu mnavyo vingi na kuzidi na mnaweza kuwapa kila wanachohitaji. Kisha baadaye, watakapokuwa navyo vingi, wataweza kuwapa mnavyohitaji. Kisha kila mmoja atakuwa na mgao ulio sawa. 15 Kama Maandiko yanavyosema,

“Wale waliokusanya vingi hawakuwa na vingi zaidi,
    na wale waliokusanya kidogo hawakuwa na vichache zaidi.”(A)

Tito na Wale Watakaosafiri Pamoja Naye

16 Namshukuru Mungu kwa sababu alimpa Tito upendo ule ule nilionao mimi kwenu. 17 Tito alikubali kufanya vile tulivyomwomba. Yeye mwenyewe alitamani sana kuja kwenu. 18 Tunamtuma Tito pamoja ndugu anayekubalika katika makanisa yote. Anasifiwa kwa sababu ya huduma yake ya Habari Njema. 19 Pia, alichaguliwa na makanisa kuambatana nasi tunapoleta sadaka hii. Tunafanya huduma hii kumpa Bwana heshima[a] na kuonesha kuwa tunapenda kusaidia.

20 Tunajitahidi kuwa waangalifu ili asiwepo mtu wa kutukosoa kwa namna ambavyo tunashugulika na sadaka hii kubwa. 21 Tunajaribu kutenda lililo jema. Tunataka kufanya kile ambacho Bwana anakubali kuwa sahihi na kile ambacho watu wanafikiri kuwa ni sahihi.

22 Pia, tunawatuma pamoja nao kaka yetu ambaye yuko tayari siku zote kutoa msaada. Amethibitisha hili kwetu mara nyingi na kwa njia nyingi. Na anataka kusaidia zaidi sasa kwa sababu ana imani zaidi nanyi.

23 Na sasa kuhusu Tito, yeye ni mshirika mwenzangu. Anafanya kazi pamoja nami kuwasaidia ninyi. Na kuhusu hawa kaka wawili wengine: wao wametumwa kutoka katika makanisa mengine, na wanaleta heshima kwa Kristo. 24 Hivyo waonesheni watu hawa kuwa mna upendo. Waonesheni kwa nini tunajisifia ninyi. Ndipo makanisa yote yatakapo tambua hili.

Footnotes

  1. 8:19 heshima Au “utukufu”. Tazama Utukufu katika Orodha ya Maneno.