Add parallel Print Page Options

Watumishi wa Agano Jipya la Mungu

Je, mnadhani tunaanza kujitafutia sifa? Je, tunahitaji barua za utambulisho kuja kwenu au kutoka kwenu kama wengine? Hapana, ninyi wenyewe ni barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu. Inafahamika na kusomwa na watu wote. Mnaonyesha kuwa ninyi ni barua toka kwa Kristo aliyoituma kupitia sisi. Barua ambayo haikuandikwa kwa wino bali kwa Roho wa Mungu aliye hai. Haikuandikwa katika mbao za mawe[a] lakini katika mioyo ya wanadamu.

Tunaweza kusema hili, kwa sababu Kristo ndiye anayetupa uhakika huu mbele za Mungu. Simaanishi kuwa tuna uwezo wa kufanya jambo lolote jema kwa uwezo wetu wenyewe. Mungu ndiye anatuwezesha kufanya yote tunayoyafanya. Ametuwezesha pia kuwa watumishi wa agano jipya lililotoka kwake kwenda kwa watu wake. Si agano la sheria zilizoandikwa, ni la Roho. Sheria zilizoandikwa huleta mauti, bali Roho huleta uzima.

Namna Nzuri ya Kumtumikia Mungu

Agano la kale lililoleta mauti, lililoandikwa kwenye mawe, lilikuja na utukufu wa Mungu. Kwa kweli, uso wa Musa ulikuwa unang'aa utukufu (Utukufu uliokuwa na ukomo) hata watu wa Israel hawakuweza kuendelea kumtazama usoni. Hivyo kwa hakika zaidi huduma ya agano jipya linalokuja kutoka kwa Roho anayeleta uzima lina utukufu zaidi. Maana yangu ni kuwa: utaratibu wa zamani wa kumtumikia Mungu uliwaweka watu katika hatia ya dhambi na kuwapa hukumu, lakini lilikuwa na utukufu. Hivyo kwa hakika utaratibu mpya wa kumtumikia Mungu unaowaweka huru watu kutoka hukumu una utukufu mkubwa zaidi. 10 Utaratibu wa zamani wa utumishi kwa Mungu ulikuwa na utukufu. Lakini kwa hakika unapoteza utukufu wake unapolinganishwa na utukufu mkubwa zaidi wa utaratibu mpya wa utumishi kwa Mungu. 11 Ikiwa utumishi ule wa muda ulikuja na utukufu, basi utumishi wa kudumu umekuja na utukufu mkubwa zaidi.

12 Kwa sababu tuna tumaini hili tunatenda kwa ujasiri mkubwa. 13 Hatuko kama Musa, ambaye alifunika uso wake ili watu wa Israel wasiendelee kuona kuwa utaratibu wa zamani wa kumtumikia Mungu ulikuwa unaelekea mwisho. 14 Lakini mioyo yao ilikuwa imefungwa. Na hata leo, watu wale wanapolisoma agano la kale, fahamu zao zinakuwa zimefunikwa. Ni kwa kupitia Yesu Kristo tu agano la kale linaondolewa. 15 Ndiyo, hata leo, wanaposoma sheria ya Musa, fahamu zao zimefunikwa. 16 Lakini, kama maandiko yanavyosema juu ya Musa, “Kila anapomgeukia Bwana, ufahamu wake unafunuliwa.” 17 Katika maandiko hayo Bwana ni Roho, na palipo na Roho wa Bwana, pana uhuru. 18 Na sura zetu hazikufunikwa. Sote tunaendelea kuutazama utukufu wa Bwana, na tunabadilishwa na kufanana na mfano huo huo tunaouona. Badiliko hili linatuletea utukufu zaidi na zaidi, na linatoka kwa Bwana, ambaye ni Roho.

Footnotes

  1. 3:3 mbao za mawe Ina maana ya sheria ambayo Mungu aliitoa kwa Musa, iliyoandikwa kwenye mbao za mawe. Pia katika mstari wa 7. Tazama Kut 24:12; 25:16.