Kushtakiana Kati Ya Ndugu

Kama mmoja wenu ana mashtaka kumhusu ndugu, anathubutuje kupeleka mashtaka yake mbele ya mahakimu wasio mcha Mungu, badala ya kuyapeleka mbele ya watu wa Mungu? Hamjui kwamba watu wa Mungu watahukumu ulimwengu? Na kama ninyi mtahukumu ulimwengu, hamwezi kuhukumu mambo madogo madogo? Hamjui kwamba tutawahu kumu malaika? Je, si zaidi mambo ya maisha haya? Kwa hiyo kwa nini kama kuna kutokuelewana kati yenu kuhusu mambo kama haya, mnachagua kama mahakimu watu ambao hata hawaheshimiwi na kanisa? Nasema hivi ili muone aibu. Je, inawezekana kuwa hakuna mtu kati yenu mwenye hekima ya kutosha kuamua mashtaka kati ya ndugu mmoja na mwenzake? Badala yake ndugu mmoja anampeleka ndugu mwingine mahakamani, tena mbele ya watu wasioamini!

Kwamba mnashtakiana kati yenu ni dalili kuwa mmeanguka. Badala ya kushtakiana, kwa nini msikubali kutendewa ubaya? Kwa nini msikubali kudanganywa? Lakini ninyi wenyewe mnakoseana na kudhulumiana, na mnafanya hivyo hata kwa ndugu zenu!

Je, hamjui kwamba wasio na haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike, waasherati hawataurithi Ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wapotoshaji; 10 wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyang’anyi. 11 Na baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho wa Mungu wetu.

Dhambi Za Zinaa

12 “Kila kitu ni halali kwangu,”lakini si kila kitu kina faida. “Kila kitu ni halali kwangu,”lakini sitatawaliwa na cho chote. 13 “Chakula ni kwa ajili ya tumbo, na tumbo ni kwa ajili ya chakula,” lakini Mungu ataviharibu vyote viwili. Mwili wa mwanadamu haukuumbwa kwa ajili ya zinaa bali kwa ajili ya Bwana, na Bwana kwa ajili ya mwili.

14 Mungu alimfufua Bwana na atatufufua na sisi pia kwa uwezo wake. 15 Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni sehemu ya Kristo? Je, naweza kuchukua sehemu ya mwili wa Kristo na kuiunganisha na mwili wa kahaba? Hata kidogo! 16 Hamjui kwamba mtu aushirikishaye mwili wake na kahaba ana kuwa mmoja naye kimwili? Maandiko yanasema, “Hao wawili watakuwa mwili mmoja.” 17 Lakini mtu anayejiunga na Bwana ana kuwa mmoja naye kiroho.

18 Kimbieni dhambi ya zinaa. Dhambi nyingine zote anazotenda mwanadamu hufanyika nje ya mwili wake, lakini anayezini, ana tenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. 19 Hamjui kwamba miili yenu ni Hekalu la Roho Mtakatifu anayekaa ndani yenu, ambaye mme pewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe; 20 mmenunuliwa kwa bei kubwa. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.