Mitume Wa Kristo

Basi, mtuhesabu sisi kuwa watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za Mungu. Zaidi ya hayo, mawakili wanatakiwa wawe waaminifu. Mimi sijali kama ninyi mkinihukumu au nikihukumiwa na mahakama ya wanadamu; kwa kweli hata mimi mwenyewe sijihukumu Dhamiri yangu hainishitaki; lakini hilo halinifanyi nisiwe na hatia. Bwana ndiye anayenihukumu. Kwa hiyo msitoe hukumu kabla ya wakati wake, kabla Bwana hajaja. Yeye atafichua mambo yaliyof ichwa gizani na kwa kuweka wazi nia za mioyo ya watu. Ndipo kila mtu atapokea sifa anayostahili kutoka kwa Mungu.

Basi ndugu zangu nimetumia mfano wa Apolo na mimi kwa faida yenu ili muweze kujifunza kutoka kwetu maana ya usemi, “Usivuke mpaka wa yale yaliyoandikwa.” Na hivyo hamtajivunia mtu fulani na kumdharau mwingine. Ni nani aliyewafanya kuwa tofauti na watu wengine wote? Mna kitu gani ambacho hamkupokea? Basi ikiwa mmepokea, mbona mnajivuna kana kwamba hayo mliyonayo si zawadi?

Mmekwisha pata kila kitu mnachohitaji! Mmekuwa matajiri! Mmekuwa wafalme pasipo msaada wetu! Lakini laiti kama mngekuwa wafalme kweli ili na sisi tuwe wafalme pamoja nanyi! Kwa sababu inaonekana kwamba Mungu ametuweka sisi mitume katika nafasi ya mwisho kabisa katika msafara wa maonyesho kama watu waliohukumiwa kufa hadharani, kwa sababu tumekuwa maonyesho kwa ulimwengu wote, kwa malaika na kwa wanadamu pia.

10 Kwa ajili ya Kristo sisi ni wajinga, lakini ninyi mna hekima ndani ya Kristo. Sisi ni dhaifu, lakini ninyi mna nguvu. Tunadharauliwa, lakini ninyi mnaheshimiwa. 11 Mpaka wakati huu tuna njaa na kiu, tumevaa matambara, tumeteswa, hatuna makao. 12 Tunafanya kazi ngumu kwa mikono yetu. Tunapolaaniwa, tunabar iki; tunapoteswa tunavumilia. 13 Tunaposingiziwa tunajibu kwa maneno ya upole. Tumekuwa kama takataka ya dunia hii, na uchafu wa ulimwengu mpaka leo hii.

14 Nawaandikia mambo haya, si kwa sababu nataka muone aibu, bali nataka niwaonye kama wanangu wapendwa. 15 Ingawa mnao viongozi wasiohesabika katika Kristo, lakini hamna baba wengi. Mimi nilikuwa baba yenu katika Kristo Yesu kwa kuwaletea Injili. 16 Basi nawasihi mfuate mfano wangu. 17 Kwa sababu hii ninam tuma Timotheo, mwanangu mpendwa na mwaminifu katika Bwana. Yeye atawakumbusha kuhusu maisha yangu katika Kristo ambayo yanakubal iana na mafundisho yangu katika kila kanisa ninalotembelea.

18 Baadhi yenu mmekuwa na kiburi mkidhani kuwa sitafika kwenu. 19 Lakini kama Bwana akipenda, nitafika kwenu mapema, nami nitapenda kujua, zaidi ya maneno yao hawa watu wenye kiburi wana uwezo gani? 20 Kwa kuwa Ufalme wa Mungu si maneno matupu bali ni nguvu. 21 Ninyi amueni. Nije kwenu na fimbo kuwaadhibu, au nije na upendo kwa roho ya upole?