Add parallel Print Page Options

Hekima ya Mungu

Tunafundisha hekima kwa watu ambao macho yao yamefunguliwa ili waione hekima ya siri ya Mungu. Si hekima ya watawala wa ulimwengu huu wanaobatilika. Tunaisema hekima ya Mungu katika namna ambayo baadhi wanaweza kuiona na wengine hawawezi. Ni hekima iliyofichwa mpaka wakati huu na Mungu aliipanga hekima hii kabla ya kuumba ulimwengu, kwa ajili ya utukufu wetu. Hakuna mtawala yeyote wa ulimwengu huu aliyeielewa hekima hii. Ikiwa wangeielewa, wasingemwua Bwana wetu mkuu na mwenye utukufu mwingi msalabani. Lakini kama Maandiko yanavyosema,

“Hakuna aliyewahi kuona,
    hakuna aliyewahi kusikia,
hakuna aliyewahi kufikiri
    kuhusu kile ambacho Mungu amewaandalia wanaompenda.”(A)

10 Lakini Mungu ametuonesha mambo haya kupitia Roho.

Roho anaweza kuchunguza mambo yote. Anajua hata siri za ndani kabisa za Mungu. 11 Hakuna mtu anayejua mawazo ya mtu mwingine. Ni roho inayoishi ndani ya mtu huyo ndiyo inajua mawazo ya mtu huyo. Ndivyo ilivyo hata kwa Mungu, ni Roho wa Mungu peke yake ndiye anayeyajua mawazo ya Mungu. 12 Tulipokea Roho wa Mungu, si roho wa ulimwengu. Tulimpokea Roho wa Mungu ili tuweze kujua yote aliyotupa Mungu.

13 Tunapozungumza, hatutumii hoja tulizofundishwa na wenye hekima. Bali hoja tulizofundishwa na Roho. Tunatumia hoja za Roho kuelezea kweli za Roho. 14 Watu wasio na Roho wa Mungu, hawakubali vitu vinavyotoka kwa Roho. Hudhani kuwa ni vitu vya kipuuzi. Hawavielewi, kwa sababu havieleweki pasipo msaada wa Roho. 15 Aliye na Roho anaweza kujua mambo yote anayofundisha Roho. Na hatutahukumiwa kuwa na hatia na mtu yeyote.[a] 16 Kama Maandiko yanavyosema,

“Nani anaweza kujua anachokiwaza Bwana?
    Nani anaweza kumshauri?”(B)

Lakini sisi tumepewa tunawaza kama Kristo.

Walimu ni Watumishi tu wa Mungu

Ndugu zangu, nilipokuwa kwenu, sikuzungumza nanyi kama ninavyozungumza na watu wanaoongozwa na Roho. Nilizungumza nanyi kama watu wa kawaida wa duniani. Mlikuwa kama watoto katika Kristo. Mafundisho niliyowafundisha yalikuwa kama maziwa, siyo chakula kigumu. Nilifanya hivi kwa kuwa hamkuwa tayari kwa chakula kigumu. Na hata sasa hamjawa tayari. Bado hamwenendi katika Roho, mnaoneana wivu na mnabishana ninyi kwa ninyi kila wakati. Hii inaonesha kuwa bado mnazifuata tamaa zenu wenyewe. Mnaenenda kama watu wa kawaida wa ulimwengu huu. Mmoja wenu anasema, “Mimi ninamfuata Paulo,” na mwingine anasema, “Ninamfuata Apolo.” Mnaposema mambo kama haya, mnaenenda kama watu wa ulimwengu.

Footnotes

  1. 2:15 hatutahukumiwa … mtu yeyote Ina maana kuwa, Mungu hatafuti kututia katika hatia. Tazama Rum 8:1,33. Wazo kuu hapa ni lile linalofanana na Rum 8:1, “Hakuna hukumu kwao wao walio ndani ya Kristo Yesu.”