Marko 4:13-20
Neno: Bibilia Takatifu
Yesu Afafanua Maana Ya Mfano Wa Mbegu
13 Kisha Yesu akawauliza, “Hamwelewi maana ya mfano huu? Mtaelewaje basi mifano mingine? 14 Yule mtu aliyepanda mbegu, alipanda neno la Mungu. 15 Mbegu zilizoanguka njiani ni sawa na watu ambao husikia neno la Mungu na shetani akaja mara moja na kulichukua lile neno lililopandwa ndani yao. 16 Hali kadhalika, mbegu iliyoanguka kwenye mwamba ni sawa na watu ambao hulisikia neno na kulipokea kwa furaha. 17 Lakini kwa kuwa neno halipenyi ndani, linadumu kwa muda mfupi. Taabu au mateso yanapotokea kwa ajili ya hilo neno, wao hupoteza imani yao. 18 Na wengine, ni kama mbegu zile zilizoanguka kwenye miiba. Wao hulisikia neno, 19 lakini mahangaiko ya dunia, udanganyifu wa mali na tamaa za mambo mbalimbali hulisonga lile neno, lisizae matunda.
20 “Bali wengine ni kama ile mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri. Wao hulisikia neno wakalipokea na kuzaa matunda: wengine thelathini, wengine sitini, na wengine mia moja.”
Read full chapterCopyright © 1989 by Biblica