Marko 1:1-8
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Yohana Atayarisha Njia kwa Ajili ya Yesu
(Mt 3:1-12; Lk 3:1-9,15-17; Yh 1:19-28)
1 Mwanzo wa Habari Njema za Yesu Masihi,[a] Mwana wa Mungu,[b] 2 zilianza kama vile Nabii Isaya alivyosema zitaanza, aliandika,
“Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako.
Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.”(A)
3 “Kuna mtu anayeipaza sauti yake toka nyikani:
‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana;
nyoosheni njia kwa ajili yake.’”(B)
4 Naye Yohana akaja, akiwabatiza watu huko nyikani huku akiwahubiri watu ujumbe kutoka kwa Mungu. Aliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa wamekubali kubadili maisha yao ndipo dhambi zao zitasamehewa. 5 Watu kutoka Yerusalemu na maeneo yote ya Uyahudi walikwenda kwa Yohana Mbatizaji; huko waliungama matendo yao mabaya kwake naye akawabatiza katika Mto Yordani.
6 Huyo Yohana alivaa mavazi yaliyofumwa kutokana na manyoya ya ngamia. Naye alijifunga mkanda wa ngozi kuzunguka kiuno chake, na alikula nzige na asali mbichi.
7 Yeye alitangaza yafuatayo: “Yupo mwingine ajaye baada yangu, mwenye nguvu zaidi kuliko mimi. Nami niliye mtumwa wa chini kabisa sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake.[c] 8 Mimi nawabatiza katika maji, lakini yeye huyo atawabatiza katika Roho Mtakatifu.”
Read full chapterFootnotes
- 1:1 Masihi Yaani “Kristo”, tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi”. Tazama Kristo na Masihi katika Orodha ya Maneno. Pia katika mstari wa 20 na katika kitabu chote hiki.
- 1:1 Mwana wa Mungu Nakala zingine za Kiyunani hazina maneno haya.
- 1:7 viatu vyake “Mimi sistahili kuwa hata kama mmoja wa watumishi wake anayeinama kumfungua kamba za viatu vyake.”
© 2017 Bible League International